MAJADILIANO YA MADAKTARI YALISHINDWA KUANZAJANA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MAJADILIANO YA MADAKTARI YALISHINDWA KUANZAJANA

Majadiliano baina ya Serikali na Madaktari kuhusu madai yao yaliyowasababisha wagome mwezi uliopita, yameshindikana kuanza jana (Alhamisi, Machi 1, 2012) baada ya madaktari kutoka nje ya mkutano wakikataa kujumuishwa na makundi mengine ya watumishi wa kada nyingine za afya wanaofanya kazi nao pamoja. 
 
Baada ya madaktari hao kukataa kuanza majadiliano na kutoka nje ya ukumbi wa mkutano, makundi mengine yaliyobaki nayo yalikataa kuanza majadiliano bila ya kuwepo madaktari.
Madaktari hao wametoa sababu kwamba wasingependa kufanya majadiliano hayo na Serikali katika kikao kinachojumuisha kada nyingine za afya kama wauguzi, wafamasia, wanasayansi wa maabara za afya, wafiziotherapia na wataalamu wa mionzi kwa sababu wakiwa pamoja madai yao hayatopewa uzito stahiki. 
 
Majadiliano hayo yaliitishwa na Serikali kufuatia maombi ya madaktari kwa Serikali ya kujadiliana nao kwa pamoja kuhusu utekelezaji wa madai yao baada ya Mkutano wao na Waziri Mkuu Februari 9, 2012 na kukamilika kwa kazi ya kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Wakati akihutubia Taifa jana (29 Februari 2012), Rais Jakaya Kikwete alieleza kwamba amepokea taarifa kuwa Kamati aliyounda Waziri Mkuu kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa kwake. Kuanzia leo (01 Machi 2012) Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo. 
 
Serikali bado inafanya jitihada za kuzungumza na madaktari na kada nyingine za Afya ili waweze kurejea kwanye meza ya mazungumzo na kuanza majadiliano mapema iwezekanavyo.
 
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
01 Machi 2012

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages