Bendi
ya African Stars "Twanga Pepeta" inataraji kufanya ziara ya maonyesho
katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara mwishoni mwa mwezi huu wa
tatu. ziara hiyo inataraji kuanzia Mkoa wa Mwanza siku ya Ijumaa tarehe 30-03-2012.
Kesho yake siku ya Jumamosi tarehe 31-03-2012 kundi
zima la Twanga Pepeta litakuwa mkoani Mara katika ukumbi wa Musoma Club
na watamalizia ziara kwa kufanya onyesho la nguvu Wilayani Kahama Mkoa
wa Shinyanga siku ya Tarehe 01-04-2012 katika ukumbi wa Club Dimpoz.
Matayarisho yote muhimu kwa ajili
ya ziara hii yamekwisha kukamilika na Bendi inataraji kuondoka na
wanamuziki wake wote ambao wataondoka siku ya Alhamisi alfajiri mara
baada ya onyesho la Club Billicanas linalofanyika kila siku za Jumatano.
Twanga Pepeta wanatumia ziara hii kwa ajili ya kutambulisha albamu yao inayotamba sasa hivi ya Dunia Daraja yenye nyimbo za'Dunia Daraja', 'Mapenzi Hayana Kiapo', 'Kauli', 'Umenivika Umasikini', 'Mtoto wa Mwisho' na'Penzi la Shemeji' pia
watatambulisha baadhi ya wasanii waliojiunga hivi karibuni wakiongozwa
na Prince Mwinjuma Muumini Kocha wa Dunia, Venance Geuza, Jumanne Said,
Grayson Semsekwa na Mshindi wa Shindano la 'BSS Second Chance' Hajji
Ramadhani ambae anakuja rasmi kwa ajili ya kuwapa shukrani wapenzi wa
Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kumpigia kura mpaka kufanikiwa kupata ushindi
wa kwanza katika shindano.
Twanga Pepeta itarudi Jijini Dar es salaam siku ya Jumatatu tarehe02-04-2012 kwa ajili ya kujitayarisha na maonyesho ya Sikukuu ya Pasaka inayotaraji kusherehekewa siku ya tarehe 08-04-2012.
Twanga pepeta imejiandaa vilivyo
ili kuwapa burudani nzuri na iliyosheheni kila aina ya utamu kwa wapenzi
watakaohudhuria maonyesho katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na inatoa wito
kwa wapenzi kujitokeza kwa wingi ili kujionea wenyewe ubunifu mkubwa wa
kutoa burudani kwa mashabiki.
Ziara hii ni mfululizo wa mkakati
wa Twanga Pepeta wa kufanya ziara kwa ajili ya maonyesho maeneo
mbalimbali kwa ajili ya kuitangaza albamu ya Dunia daraja iliyozinduliwa
Novemba mwaka jana, kabla ya kwenda mikoa ya kanda ya Ziwa twanga
pepeta imeshafanya ziara katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Kilimanjaro,
Mbeya na Iringa na inataraji kwenda katika mikoa ya Ruvuma, Dodoma,
Tanga, Morogoro, Pwani, Arusha, Tabora, Zanzibar na Kigoma hapo baadae.
Martini Sospeter
Meneja
Twanga Pepeta.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)