Mtaalam wa matumizi ya teknolojia ya simu katika utoaji wa elimu kutoka chuo kikuu cha Stanford kilichoko Calfonia
nchini Marekani Dkt. Paul Kim akiwaonesha washiriki waliohudhuria
mkutano wa uliojadili umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya simu katika
utoaji wa elimu moja ya darasa alilolifanyia utafiti ambalo wanafuzi wake wanatumia simu katika masomo yao na kuonyesha ufanisi mkubwa katika mitihani yao.
Mtaalam wa Elimu na Mafunzo Bi. Zamaradi Saidi akitoa utangulizi kwa
washiriki waliohudhuria mkutano wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano
ya simu katika utoaji wa elimu jijini Dar es salaam.Picha na Aron Msigwa –MAELEZO
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Imeelezwa
kuwa Tanzania itapiga hatua katika sekta ya elimu na kuongeza uelewa
miongoni mwa wanafunzi iwapo matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta
katika kufundishia yatazingatiwa kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo
vikuu.
Akizungumza
na wadau wa elimu na mawasiliano leo jijini Dar es salaam mtaalam wa
matumizi ya teknolojia ya simu katika utoaji wa elimu kutoka chuo kikuu
cha Stanford kilichoko Calfonia nchini Marekani Dkt. Paul Kim amesema hivi
sasa dunia inabadilika kutoka hatua moja kwenda nyingine na kusisitiza
kuwa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta katika sekta ya elimu
hayaepukiki.
Amesema
matumizi ya teknolojia hiyo yameendelea sana katika nchi zilizoendelea
za bara la Ulaya , Amerika na baadhi ya nchi za Asia huku akisisitiza
kuwa matumizi ya teknolojia hiyo katika bara la Afrika yanaendelea kuongezeka kwa kasi ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Ufanisi wa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta pamoja na mabadiliko yake kwa maendeleo ya elimu duniani kote unahitaji utayari na ushiriki wa watu, viongozi wa nchi husika na taifa kwa ujumla” amesema Dkt. Kim.
Amefafanua kuwa yeye kama mtaalam wa matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta kwa kushirikiana na Shirika la Seed Empowerment yuko nchini Tanzania kushirikiana na kufanya kazi pamoja na
wadau mbalimbali wa elimu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na
binafsi, vyuo vya elimu na sayansi, vyuo vikuu, shule za msingi na
sekondari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inapatikana na matumizi
yake yanakuwa endelevu nchini.
Amesema
pamoja na Tanzania kukabiliwa na changamoto mbalimbali za matumizi ya
teknolojia hii atatumia uzoefu wake na utaalam wake kwa kushirikiana na
mamlaka husika za elimu katika kuhakikisha kuwa teknolojia ya matumizi
ya simu katika utoaji wa elimu nchini inaendelea na kukua kwa kasi.
“
Ninajua matumizi ya teknolojia ya Kompyuta na simu katika kufundishia
hapa Tanzania bado yako chini lakini kwa kutumia uzoefu wangu wa chuo
kikuu Stanford, Marekani na uzoefu wa nchi yangu ya Korea ya Kusini
nilikozaliwa ambayo maendeleo yake katika matumizi ya teknolojia hii
yalianza taratibu kwa kushirikiana kikamilifu na wadau wa Tanzania tutaweza kuinua kiwango cha elimu kwa matumizi ya teknolojia hii”.
Kwa upande wake Bi. Zamaradi Saidi mdau
na mshiriki wa mkutano huo ambaye ni mtaalam wa Elimu na mafunzo
amesema mpango huo kwa Tanzania unalenga kuingia katika mfumo wa elimu
kuleta teknolojia ya kufundishia katika sekta ya elimu katika ngazi zote
na kuusifu mpango huo kuwa utawawezesha wanafunzi kujifunza kutokana
na programu zilizoandaliwa ambazo zitawafaa wanafunzi wenye ulemavu.
Pia
amefafanua kuwa mpango huo utawawezesha wanafunzi na walimu kuwa na
uelewa wa matumizi ya vifaa vya kompyuta kutokana na tatizo la kuwepo
kwa baadhi ya shule na vyuo ambavyo vimekuwa vikipatiwa misaada ya kompyuta lakini hazitumiki kutokana na uelewa mdogo wa wanafunzi na walimu.
Ameongeza
kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kuboresha mfumo wa
ufundishaji na kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa wabunifu na kuepuka tabia
ya kukariri masomo hivyo kuongeza uelewa wao na kuwafanya walimu
kubaki kama wawezeshaji.
Naye
mkufunzi na kaimu mkuu wa kitengo cha teknolojia maalum (ASTU) kutoka
Taasisi ya Elimu na Teknolojia ya Chuo Kikuu Huria Tanzania Bw. Cosmas
Mnyanyi amesema kuwa licha ya mpango huo kuwa na manufaa makubwa na
mchango mkubwa wa maendeleo ya elimu endapo utatumika hapa nchini bado
mfumo wetu wa elimu una vikwazo mbalimbali vikiwemo ukatazaji wa
matumizi ya simu kwa wanafunzi hivyo mkakati huo unahitaji kutolewa
elimu ili kuleta ufanisi utakaporuhusiwa kutumika nchini.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)