HOTUBA YA MHE CELINA O. KOMBANI, WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AKIWASILISHA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011 LEO BUNGENI MJINI DODOMA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

HOTUBA YA MHE CELINA O. KOMBANI, WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AKIWASILISHA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011 LEO BUNGENI MJINI DODOMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mh Celina Kombani
--
HOTUBA YA MHE CELINA O. KOMBANI, WAZIRI WA KATIBA
NA SHERIA AKIWASILISHA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO
YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011
__________________________
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Celina O. Kombani, kwa heshima na taadhima, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu sasa lijadili na hatimaye kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2012 yaani, “The Constitutional Review (Amendment) Act, 2012”.
 
Mheshimiwa Spika, Muswada ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Waandishi wa Sheria; Kamati; na baadhi ya Wabunge kutoka vyama vyote vya siasa. Ninawashukuru sana. Ninamshukuru sana Mhe. Pindi Hazara Chana, Mbunge Viti Maalum, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala , Mhe. Angela Jasmine Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na kupitia kwao Wajumbe wote wa Kamati kwa mchango na kazi kubwa waliyoifanya kuuboresha Muswada huu. Maoni na ushauri wao kwa kiasi kikubwa vimesaidia kuuboresha sana Muswada huu. Hii inathibitishwa na marekebisho katika Muswada kama yanavyoonekana katika Jedwali la Marekebisho ambalo waheshimiwa Wabunge wamegawiwa.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Na. 8/2011 ilipitishwa na Bunge hili katika Mkutano wake wa Tano. Tunaleta mapendekezo ya kufanya marekebisho hayo muda mfupi tu baada ya Bunge kutunga Sheria hii na baada ya Mhe. Rais kuiridhia tarehe 29 Novemba, 2011 na kuanza kutumika tarehe 1 Desemba, 2011. 
 
Mantiki ya marekebisho haya, na kama yatakubaliwa na kupitishwa na Bunge hili, yanalenga kuiboresha Sheria hiyo na kuwezesha kuwepo kwa muafaka wa kitaifa katika kuendesha mchakato wa kuipata Katiba Mpya. Jambo lolote linalotuwezesha kuwa na muafaka wa kitaifa katika jambo muhimu kama mchakato wa kupata Katiba Mpya inayokidhi matarajio, matumaini na mahitaji ya Watanzania wengi ni jambo jema na linalopaswa kupewa nafasi kila inapowezekana.
 
Mheshimiwa Spika, historia ya kuupitisha Muswada huo kuwa Sheria hii hapa Bungeni inaeleweka na sina sababu ya kuirudia. Kama mnavyofahamu, kabla na baada ya kusaini Sheria hiyo, Mheshimiwa Rais aliendelea kupokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuiboresha Sheria hiyo ili kuwezesha kuwepo muafaka wa kitaifa. Maoni hayo yalitolewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini. Kwa kuzingatia baadhi ya maoni yaliyotolewa, Serikali imetoa mapendekezo ya kurekebisha Sheria hiyo kama yalivyoainishwa kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na Jedwali la Marekebisho.
 
Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kufanya marekebisho katika vifungu vya 6, 12, 13, 17, 18 na 21 vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Lengo la mapendekezo katika vifungu hivyo ni kuondoa sharti la viongozi wa vyama vya siasa kwa ngazi yoyote kutoteuliwa kuwa wajumbe wa Tume, kumruhusu Rais kualika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, mashirika ya kidini, taasisi, asasi na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana kutayarisha orodha ya majina ya wajumbe ili Rais achague miongoni mwao Wajumbe wa Tume; kuainisha utaratibu wa kumuondoa Kamishna wa Tume na kuruhusu Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa, Wakurugenzi wa Manispaa na Makatibu wa Mabaraza ya Miji au Wilaya kupokea taarifa za programu zitakazoendeshwa katika maeneo yao, badala ya Wakuu wa Wilaya. Aidha, marekebisho hayo yanalenga pia kuruhusu jumuiya, asasi, taasisi au makundi ya watu yenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa ajili ya kukusanya maoni juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwenye Tume.
Mheshimiwa Spika, katika Jedwali la Marekebisho, tunapendekeza kuwa Ibara ya 2 ya Muswada ifanyiwe marekebisho kwa kuiandika upya. Lengo la mapendekezo hayo ni kuondoa kizuizi kwa madiwani kuwa wajumbe wa Tume. Kwa kuwa madiwani hawataingia katika hatua ya Bunge Maalum la Katiba, tunapendekeza kuwa wasizuiwe kuwa wajumbe wa Tume iwapo itaonekana kuwa wapo wenye sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
 
Mheshimiwa Spika, Jedwali la Marekebisho linapendekeza kuongeza masharti katika Ibara hiyo ya 2 ya Muswada kwa kuongeza masharti mapya katika kifungu cha 6 cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba. Masharti yanayopendekezwa yanalenga kumwezesha Mheshimiwa Rais kualika vyama vya siasa, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, jumuiya, taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana kumpatia orodha ya majina, ambayo miongoni mwao Rais atateua wajumbe wa Tume. Hii itasaidia kuweka uwazi na ushirikishi wa wananchi katika hatua ya uteuzi wa wajumbe wa Tume. Aidha, masharti mengine yanayoongezwa katika kifungu hicho yanalenga kuweka bayana kuwa pamoja na kualika vyama vya siasa, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, jumuiya na taasisi na kuteua wajumbe kutoka miongoni mwa majina hayo, Rais hatazuiwa kuteua wajumbe wengine ambao ataona wanafaa kuwemo kwenye Tume.
Mheshimiwa Spika, aya B ya Jedwali la marekebisho inapendekeza kuingiza masharti mapya katika kifungu 12 ili kuainisha jinsi mjumbe wa Tume atakavyoondolewa kwenye Tume. Inapendekezwa kuwa iwapo suala la kumwondoa mjumbe wa Tume litajitokeza, basi Rais awateue Wajumbe wa Kamati kuchunguza suala hilo. Kamati hiyo itakuwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar atakayeteuliwa na Chama cha Wanasheria cha Zanzibar na Wakili wa Mahakama Kuu atakayeteuliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika. Aidha, inapendekezwa kuwa Kamati hiyo ipewe mamlaka ya kutengeneza taratibu zitakazoingoza katika kufanya uchunguzi. Marekebisho mengine yanapendekezwa katika kifungu cha 13 cha Sheria hiyo katika kifungu kidogo cha (6) kwa azma ya kuifanya Tume kuwa mamlaka ya nidhamu kwa wajumbe wa Sekretarieti. Sheria ya sasa haionyeshi mamlaka ya nidhamu kwa wajumbe hao.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 17 cha Sheria ili kuwezesha Tume kufanya kazi na Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara, na Mkurugenzi wa Manispaa na Makatibu wa Mabaraza ya Miji au Wilaya kwa upande wa Tanzania Zanzibar katika uandaaji wa mikutano na hadhira zenye kufanana na hizo badala ya Wakuu wa Wilaya walioanishwa kwenye Sheria. Marekebisho mengine yanapendekezwa katika kifungu hicho hicho ili kuruhusu mtu binafsi, taasisi au kikundi cha watu wenye malengo yanayofanana kuendesha progamu ya elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya Katiba baada ya kutoa taarifa, kusajiliwa na kuanisha chanzo cha mapato ya kuendeshea programu hiyo kwa Tume. Inapendekezwa pia kuwa asasi, taasisi, jumuiya au vikundi vyenye malengo yanayofanana viruhusiwe kuandaa mikutano kwa lengo la kukusanya maoni ya wanachama wao kuhusu Katiba na kisha kuyawailisha kwenye Tume. Hata hivyo, endapo asasi, taasisi, jumuiya au vikundi hivyo vitataka kufanya mikutano au mikusanyiko ya hadhara, watalazimika kutoa taarifa kwenye mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria husika za Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar.
Marekebisho ya Mwisho yanapendekezwa kufanywa katika kifungu cha 21(3) ili kupunguza adhabu kwa watu watakaokiuka masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Adhabu inayopendekezwa ni faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na uziozidi miaka mitatu badala ya faini isiyopungua milioni tano na isiyozidi milioni kumi na tano au kifungo kwa muda usiopungua miaka mitatu na uziozidi miaka saba inayoanishwa kwenye Sheria ya sasa.
 
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya ninapenda, kupitia kwako, kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, kuujadili Muswada huu na kuupitisha katika hatua mbili, yaani, Kusomwa Mara ya Pili na Kusomwa Mara ya Tatu. Nina imani kwamba Bunge lako litaridhia marekebisho yote yanayopendekezwa na litakubali marekebisho haya yawe sehemu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka, 2011.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages