Kauli
ya CCM juu ya nyongeza ya posho za vikao kwa wabunge ni ya kinafiki,
haionyeshi uongozi thabiti na inalenga chama tawala kujikosha kutokana
na hasira ya umma dhidi ya viongozi waandamizi wa chama hicho na
wabunge wake kutaka nyongeza ya posho za vikao kinyemela.
Aidha, kauli hiyo ni muendelezo wa kauli za CCM za kujikosha mbele ya
umma baada ya wananchi kupinga maamuzi ya serikali inayoongozwa na
chama hicho katika masuala ambayo chama hicho kilikuwa na taarifa nayo
kabla lakini kikashindwa kutoa muongozo unaostahili kwa serikali kama
ilivyokuwa kwenye suala la kupandisha kupindukia kwa ushuru wa mafuta
ya taa na kuongeza bei na gharama za maisha kwa wananchi wa kipato cha
chini au kuhusu malipo ya fidia kwa Dowans.
Kauli
kwamba ‘CCM iliwaomba na kuwasihi wabunge na mamlaka zinazohusika na
mchakato wa swala la nyongeza ya posho za vikao kuliangalia upya na
kutumia busara, ikiwezekana kuachana nalo kwasasa’ inadhihirisha kwamba
kimsingi chama hicho kimepoteza uwezo wa kuwa chama tawala.
Kauli
kama hii ni kama agizo lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM katika kikao
chake cha tarehe 31 Agosti 2011 ya kutaka serikali ipunguze bei ya
mafuta ya taa baada ya kuona wananchi wanaungana na msimamo wa CHADEMA
uliotolewa bungeni na wabunge wake wakati wa kupitishwa kwenye muswada
wa sheria ya fedha mwezi Juni 2011 na kujadiliwa kwa bajeti ya Wizara
ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011.
Hata
hivyo mpaka sasa agizo hilo ambalo limetokana na kikao kilichoongozwa
na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete halijatekelezwa hali
ambayo inadhihirisha ulegelege wa CCM na serikali yake katika
kusimamia masuala ya msingi ya taifa hali ambayo athari zake
zinathibitika hivi sasa katika mjadala huu wa posho za vikao ambapo
ombwe na uongozi linaonekana bayana katika chama hicho na serikali.
Kauli
ya CCM ya kumpongeza Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama
hicho kwa kushindwa kuonyesha uongozi na badala yake kutupa mzigo wa
wabunge kwenye suala ambalo kwa mujibu wa sheria Rais ndiyo mwenye
mamlaka nalo ni ishara ya CCM kulea misingi ya kutowajibika miongoni
mwa viongozi wakuu wa serikali na chama hicho.
Iwapo
CCM ingekuwa na dhamira ya kweli ya kukataa posho za vikao ingefanya
maamuzi ya kukataa kupitia vikao vya chama hicho vya kamati kuu na
halmashauri kuu ambavyo viliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho Rais
Kikwete kwa nyakati mbalimbali wakati ambapo mjadala wa posho za vikao
ukiwa tayari umekolea katika taifa baada ya CHADEMA kuibua suala
husika ndani na nje ya bunge kuanzia wakati wa bunge la bajeti kupitia
pia maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni.
CHADEMA
inaitaka CCM kama kweli inajali maslahi ya wananchi kufanya maamuzi
ndani ya vikao vya chama hicho na kuandaa mapendekezo kwa serikali ya
kufuta posho zote za vikao kwenye mfumo wa utumishi wa umma kama
ilivyoelezwa katika ilani ya CHADEMA ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na
Mpango wa Taifa wa miaka mitano uliopitishwa na bunge mwaka 2011.
Aidha,
badala ya kumpongeza Rais Kikwete kwa kauli iliyotolewa na ikulu ya
kuhamisha lawama kuhusu suala hilo kwa wabunge, CCM itoe mwito kwa Rais
Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kutoa kauli yake
mwenyewe ya kufanya uamuzi wa kufuta posho za vikao katika mfumo wa
utumishi wa umma na kutoa kauli ya wazi ya kukataa nyongeza ya posho za
wabunge.
Pia,
CCM badala ya kutaka tu wabunge kwa ujumla kutafakari ieleze
inachukua hatua gani kwa viongozi wa serikali na bunge wanaotaka na
chama hicho kunukuliwa na vyombo vya habari wakieleza kwamba Rais
Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kuwa amebariki
nyongeza ya posho hizo na hivyo kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja
katika serikali na chama hicho.
Kushindwa
kwa CCM kuchukua hatua za kichama dhidi ya viongozi hao ambao ni
wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho kunadhihirisha kwamba pamoja na
kuwa Rais Kikwete hajasaini masharti mapya ya kazi za wabunge
ameshakubaliana nao kinyemela kuhusu kuanza kutoa nyongeza ya posho za
vikao; kinyume na hapo kauli za CCM zitaendelea kudhihirika kuwa ni za
kinafiki na za kujikosha.
CHADEMA
inaendelea kusisitiza kauli yake kwamba ongezeko la posho ya vikao
lilofanyika linapaswa kusitishwa kwa kuwa limefanyika kinyume na
taratibu na pia halina uhalali wowote kimantiki na halijazingatia
uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla; nyongeza
hiyo ya posho ya vikao ni haramu (Illegitimate).
Aidha,
kauli iliyotolewa kwamba nyongeza hiyo ya posho za vikao ni kwa
sababu ya kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli,
wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo.
Nyongeza
hiyo ya posho ya vikao ni matumizi mabaya ya madaraka na ni dharau
kwa walipa kodi wanaohangaika na kupanda kwa gharama za maisha na
athari za ubadhirifu wa fedha za umma. Ni udhaifu kufikiri kwamba
suluhisho la kupanda kwa gharama za maisha ni kuongeza posho za kikao;
tatizo la kupanda kwa gharama za maisha linapaswa kushughulikiwa kwa
kuchukua hatua dhidi ya matatizo ya kiuchumi katika nchi ili kuweza
kuwa na tija kwa wananchi wengi ambao ni waathirika zaidi wa kupanda
kwa gharama za maisha kuliko wabunge.
CHADEMA
inarejea kuukumbusha umma kwamba Sheria ya Utawala wa Bunge (National
Assembly Administration Act) ya mwaka 2008 kifungu cha 19 kinataja
aina ya posho ambazo zinaweza kutolewa kwa wabunge kama ambavyo Rais
ataeleza kwa maandishi. Katika kipengele (d) sheria imetaja orodha (i)
mpaka (iii) ya posho ambazo wabunge wanastahili kulipwa za usafiri,
kujikimu na wasaidizi. Katika orodha hiyo hakuna Posho ya Kikao
(Sitting Allowance) ambayo inalipwa hivi sasa kwa kuwekwa kwenye
akaunti za wabunge moja kwa moja ambayo kamati ya wabunge wa CHADEMA
tunataka ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo
mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.
Kifungu
19 (d) (iv) kimempa mamlaka Rais ya kutoa posho zingine kwa wabunge
kwa kadiri atakavyoelekeza; kifungu hiki kimetoa mwanya wa kutolewa kwa
waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais wa tarehe 25 Oktoba 2010
wenye kumbukumbu na. CAB111/338/01/83 masharti ya kazi ya mbunge
ambao umeeleza viwango vya posho mbalimbali ikiwemo kutoa posho ya
vikao (Sitting Allowance).
Hivyo,
badala ya Rais Kikwete kukwepa wajibu huo wa kisheria na kuhamisha
mzigo kwa wabunge anapaswa yeye mwenyewe kufanya uamuzi wa kukataa
nyongeza ya posho za vikao na kufuta posho za vikao katika mfumo mzima
wa utumishi wa umma kama ilivyopendekezwa na CHADEMA pamoja na kambi
rasmi ya upinzani bungeni.
Izingatiwe
kwamba uchumi wa nchi hivi sasa unasuasua, serikali ina hali mbaya ya
fedha kutokana na kupungua kwa kiwango cha fedha kinachopatikana
katika kodi na washirika wa kimaendeleo ukilinganisha na mahitaji ya
bajeti; na hivyo kukopa kibiashara kwa ajili ya kuziba nakisi iliyopo.
Kupungua
kwa uzalishaji, kiwango cha fedha pamoja na kuongezeka kwa ubadhirifu
katika matumizi ya rasilimali za umma kunachangia katika mfumuko wa
bei hali inayohitaji mpango wa dharura wa kunusuru uchumi wetu
ukaohusisha pamoja na mambo mengine kubana matumizi ya serikali.
CHADEMA
kwa kurejea tamko la mwanzo wa mwaka 2012 lililotolewa na Katibu Mkuu
Dr Wilbroad Slaa ambalo limetaka kipaumbele kiwe ni kunusuru uchumi
wa nchi na kupanda wa gharama za maisha kwa wananchi, tulitarajia
kwamba CCM na serikali yake watoe kwa umma mpango wa kukabiliana na
hali hiyo badala ya kurushiana mpira kuhusu nyongeza ya posho za vikao
huku mwelekeo wa uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ukiwa
kwenye hali tete na nchi ikiwa kwenye migogoro ya kijamii kuhusu
maslahi ya madaktari, wanafunzi na makundi mengine katika jamii.
CHADEMA inasisitiza msimamo wake kwamba posho za vikao zifutwe kwa kuzingatia kuwa
Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010 imeeleza kwamba lengo la msingi ni
kuondoa posho za vikao (sitting allowance ) hatua ambayo itaambatana na
nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kuendana na ujuzi,
nafasi, wajibu ili wafanyakazi walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya
kwa haki; uamuzi ambao utawezesha pia kuelekeza fedha zaidi katika
miradi ya maendeleo.
Imetolewa tarehe 02/02/2012-Dodoma na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)