Balozi wa Pakistan nchini Tanzania Amtembelea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Balozi wa Pakistan nchini Tanzania Amtembelea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad

Balozi wa Pakistan nchini Tanzania Bw. Tajammul Altaf akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad baada ya mazungumzo yao na kumkabidhi CDs zinazohusiana na hali ya uchumi wa Pakistan.Picha, Salmin Said-Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
----
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Rais amekutana na Balozi wa Pakistan nchini Tanzania na kuelezea haja ya kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbali mbali zikiwemo elimu, biashara na utafiti wa kilimo.

Amesema Zanzibar inafuarahia uhusiano mzuri wa muda mrefu uliopo kati yake na Pakistan na kutaka uhusiano huo uendelezwe kwa maslahi ya pande hizo mbili.Amefahamisha kuwa Pakistan ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika masuala ya ulinzi ya usalama pamoja na utafiti wa kilimo, na kumtaka balozi huyo kuangalia uwezekano kwa nchi yake kuongeza nafasi za masomo kwa Zanzibar katika fani hizo ili nayo iweze kupiga hatua za maendeleo.

“Kwa sasa tutajifunza kutoka kwenu kutokana na uzoefu mlionao katika nyanja hizo, na si vibaya ikiwa tutapata fursa zaidi kwa vijana wetu kwenda kujifunza nchini Pakistan”, alifafanua Maalim Seif.

Aidha amesema Zanzibar inaweza kushirikiana na Pakistan katika kilimo cha umwagiliaji kutokana na nchi hiyo kuwa na uzowefu mkubwa katika kilimo cha mpunga ambacho ndio zao kuu la chakula kwa Zanzibar.

Nae Balozi wa Pakistan nchini Tanzania Bw.Tajammul Altaf, ameahidi kuwashauri wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Pakistan kuja kuwekeza Zanzibar hasa katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya nguo na kuingiza saruji nchini ambayo bei yake itakuwa nafuu.

Amesema yapo maeneo mengi ya ushirikiano lakini kwa sasa ameshawishika zaidi kukuza biashara kati ya Zanzibar na Pakistan sambamba na kuziunganisha Jumuiya za wafanyabiashara za pande hizo mbili “Chamber of Commerce” kufanya kazi pamoja na kubadilishana uzowefu juu ya masuala ya biashara.

Pia balozi Altaf amesema ofisi yake itatoa pendekezo maalum kwa nchi yake katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inapatiwa fursa mara mbili za masomo nchini Pakistan, ili kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kujifunza taaluma mbali mbali zikiwemo za ulinzi “Navy”, kilimo, utafiti na diplomasia.

Amefahamisha kuwa Pakistan ina historia ndefu katika taaluma hizo hasa ile ya diplomasia ambapo imefanikiwa kusomesha wanadiplomasia wengi duniani, na kwamba Zanzibar inaweza kunufaika na taaluma hizo.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages