Ndugu zangu,
Naomba nitwae fursa hii kuwapa pole wale waliofiwa na ndugu zao waliouwawa na Polisi huko Songea. Poleni sana.
Tunaelekea Wapi?
Amani
ya Tanzania sasa inatikiswa na hali si shwari nchini. Hali hii inatia
hofu na mashaka makubwa kwa mtanzania mzalendo kwani matukio ya mauwaji
yanayotokana na wananchi kuaandamana na kuuwawa na Polisi yanadizi
kuongezeka. Polisi wamewauwa raia wasio na hatia katika sehemu
mbalimbali nchini zikiwemo Arusha, Mbeya, na sasa Songea. Mauwaji haya
ni kinyume na maadili na wajibu wa Polisi kwani kazi ya siku zote ni
kulinda usalama wa raia na mali zao. Iweje leo Polisi wanawauwa raia na
kuharibu mali zao? Chuki inayopandikizwa na ukiukwaji huu wa haki za
binadamu ni kubwa dhidi serikali na pia kwa Chama Cha Mapinduzi. Chuki
hii ni kubwa sana miongoni mwa vijana na hata watu wazima, na jambo la
hatari zaidi ni kwamba inasambaa kwa kasi zaidi kila pembe ya nchi -
mijini na vijijini. Katika makala haya nitawaongela vijana kwani hawa
ndio wamekuwa wakipambana na Polisi.
Wasifu wa Vijana
Vijana
ninaowaongelea hapa wana umri wa miaka kati ya 16 na 40 (ingawa ujana
unaanzia miaka 18) na ndiyo walio wengi katika nchi yetu. Pili, ndiyo
nguvu kazi ya taifa. Tatu, wengi wao hawana hata elimu ya msingi, na
wale waliobahatika kupata elimu ya sekondari wengi wao wamesomea katika
sekondari za kata ambazo zimewakata. Nne, wengi wao hawana ajira rasmi
yenye pensheni na mafao mengine. Tano, wamekulia katika mazingira ya
ulimwengu wa utandawazi (Profesa Shivji anauita UTANDAWIZI) naTanzania
inayokumbatia sana siasa za uliberali mamboleo zilizojaa unyonyaji,
dhuluma na uonevu. Sita, ni wahanga wa soko huria ambalo limewaacha
wanalia. Saba, wengi wao hawaijui kwa dhati historia ya nchi yetu na
siasa yake ya kuthamini UTU na HAKI ilivyokuwa. Nane, wengi wao si waoga
pale wanapokuwa wadai haki zao. Tisa, wengi wao wamekulia katika
familia zenye hali ngumu ya maisha inayozungukwa na umasikini
uliokithiri na magonjwa katika mitaa ya miji yetu na vijiji vyetu. Kumi,
wengi wao wana afya zilizodhohofika kutokana na kutokupata lishe ya
kutosha na matibabu ya uhakika lakini wanafanya kazi ngumu sana tena kwa
muda mrefu na kulipwa ujira mdogo.
Mtu
anaweza kuwadharau vijana hawa kwamba kwa kuwa wengi wao si wasomi na
wanadhiki, basi ni rahisi kuwadanganya au kuwatisha wakanyamaza kwa
dhana kwamba: hawazijui haki zao za msingi; hawaujui mfumo wa uchumi wa
dunia unavyofanya kazi na unavyowaathiri; hawajui athari za kupanda kwa
bei ya mafuta; hawajui athari za mfumuko wa bei; na hawajui maana halisi
ya demokrasia kwani zipo tuhuma kwamba wengi wao hawapigi kura au
wanauza shahada zao. Na kwamba wanachojua ni kupata mlo wao na siku
ikapita. Lakini si hivyo hata kidogo. Vijana hawa wanazijua haki zao na
mahitaji yao msingi ya kuehishimiwa na kuthaminiwa utu wao, ya chakula,
malazi na mavazi.
Kama
ilivyo kwa binadamu yeyote awaye, vijana hawa hawataki kuishi katika
maisha duni ya kimaskini. Wanataka ustawi na maisha bora kwao na vizazi
vyao. Pia tufahamu kwamba vijana hawa, kwa jitihada zao binafsi, ni
wajuzi katika fani mbalimbali kuanzia ufundi mekanika hadi ujenzi wa
nyumba. Wana maarifa ya kuendesha biashara tena kwa faida. Wanajua fika
wafanye nini ili wastawi. Ni wafanyakazi hodari ndio maana wanaweza
kujilisha na si wezi. Lakini ni bahati mbaya sana katika safari yao ya
maisha, njia yao imejaa vikwazo vya kila namna - dhuluma na uonevu;
rushwa na ufisadi. Kutokana na hali hii vijana hawa wamekata tamaa.
Wengi
wao hawana tena tumaini la maisha bora. Ndoto zao zimekufa. Sasa
wanazivuta hisia na wameanza kuandamana wakiungwa mkono na wazee,
wafanyakazi maofisini na jamii inayowazunguka wanawake kwa wanaume.
Nilifuatilia maandamano ya Mwanza na taarifa nilizozipata zinasema
kwamba wanawake katika maeneo ya jiji hilo walikuwa na ndoo za maji
tayari kuwapatia vijana wanawe nyuso zao pindi mabomu ya machozi
yakipingwa. Mapambano ya Mbeya nasikia yalikuwa ni makali kweli. Katika
maandamano ya vijana kudai haki zao tumeiona ‘NGUVU YA VIJANA’
ikitembea. NGUVU hii ya vijana ikiachwa bila kupewa majibu na suluhisho
la matatizo yao ITAUMA NA TAIFA LITAUMIA. Tumeiona mifano duniani kote
na hivi karibuni katika nchi za Kiarabu. Tusifike huko.
Kuwauwa Waandamanaji ni Kuitia Amani Kitanzi
Kuwauwa
waandamanaji ni sawa na kuiwekea kitanzi amani. Hali hii inaweza
kusababisha maandamano yenye ghasia kuibuka nchi nzima. Nayo serikali
ikajikuta inatumia mabavu zaidi kuyazima maandamano haya. Katika
kuyazima maandamano ipo nafsi kubwa sana ya watu wengi kupoteza maisha.
Watu wakipoteza maisha chuki itaongezeka na damu nyingi zaidi itazidi
kumwagika kutokana na mapambano kati raia na vyombo vya dola. Huo ndio
wakati ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wasioitakia mema Tanzania. Hapo
litatolewa tamko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu
umwagaji damu huo na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Serikali
itaingia katika mgogoro mkubwa ndani na nje katika jumuiya ya
kimataifa. Matamko yatatolewa na wananchi ndani ya nchi na pia mataifa
makubwa ya nje kwamba serikali ijiuzulu na CCM kama chama tawala kiachie
ngazi. Hatujui nini itakuwa ni hatima hali hii. Lakini ukweli ni kwamba
amani haitakuwepo tena. Watu wengi wasio na hatia watauwawa na wengine
watakuwa wakimbizi. Uchumi na ustawi utavurugika. Kwa hiyo basi Polisi
ijitahidi sana kuepuka kuuwa raia wasio na hatia. Itumike busara zaidi
na nguvu za kadri na kadri za “piga lakini chunga usiuwe” na si risasi
za moto. Tukumbuke kuwa Tanzania ni katika nchi chache sana Afrika
ambayo hijaingia katika machafuko. Na yapo mataifa yanataka siku moja
Tanzania itikiswe ili waone nini kitatokea. Mungu atuepushe balaa hili.
Nini Chanzo?
Wengi
watakubaliana nami kuwa kiini hasa cha watu kuandamana ni kukithiri kwa
umaskini nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana, uonevu, kutokuthaminiwa
kwa UTU wa watu na kuheshimiwa HAKI zao, maisha kuwa ghali, unyonyaji na
dhuluma. Katika hotuba yake ya “Wasia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM”
Hayati Baba wa Taifa aliyachambua vema mambo haya aliposema hivi:
“Tanzania isikosee ikaacha msimamo wake wa kuhakikisha kwamba uko usawa
wa binadamu, kuna usawa wa msingi katika hali ya maisha ya kila mtu, na
kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania.
Tukifanya
kosa kama hilo tutavuruga msingi wote wa utulivu na amani katika nchi
yetu. Maana yake ni kwamba tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za
‘Sisi’na ‘Wao’. Tutaacha watu wachache wawe na mali nguvu, na fidhuli ya
kuwa na mali na nguvu; watu wengi wawe ni maskini na wanyonge; na wana
maning’uniko na ghadhabu za umaskini na unyonge.
Mgawanyiko
wa namna hiyo ni hatari sana. Utaratibu wa vyama vingi katika mazingira
na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauiti kubwa sana za
mapato na hali ya maisha au hata matumaini tu ya maisha mema ya baadaye
haziwezi kuzaa utulivu. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga
amani na utulivu wa kudumu katika nchi masikini bila kuheshimu misingi
ya haki na usawa. Na ‘unyang’au’ kwa hulka yake hauheshimu misingi ya
haki na usawa.”
Suluhisho
Hatima
ya maisha ya vijana si suala dogo la kuacha lijimalize lenyewe.
Linataka kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Suluhisho la kweli
ni kurudi katika miongozo ya Mwalimu Nyerere ya kuthamini UTU na USAWA
wa watu na kuheshimu HAKI zao. Tuonyeshe kwa vitendo kwamba kweli
tunazijua, tunazitambua na kuguswa na shida za watu. Na kwamba kwa
uhakika kabisa kabisa tunazifanyia kazi. Na matunda au matokeo ya kazi
hiyo yanaonekana. Shaaban Robert aliandika, “Matendo hukidhi haja
maridhawa kuliko maneno.” Vijana wanataka matendo. Wanataka ajira.
Wanataka huduma bora ya afya. Wanataka elimu bora kwao na vizazi vyao.
Wanataka kunufaika utajiri wa raslimali za nchi. Wanataka rushwa
idhibitiwe. Dhuluma, uonevu na unyonyaji vikomeshwe.
Kazi
hizi zinafanywa na serikali. Lakini serikali ina wajibu wa kuyafanyia
kazi mambo haya na kuleta majibu ya kuwaridhisha vijana na wananchi.
Matokeo yake imani ya vijana na wananchi kwa CCM na serikali yake
itarudi. Nayasema haya kwa upendo na moyo mweupe kabisa kama mfuasi wa
siasa na mafunzo ya Mwalimu ya Nyerere na kada wa CCM (nje ya chama ndani ya umma). Chama Cha Mapinduzi kiliijengea
Tanzania heshima katika Afrika na kote duniani. Chama kilisimamia na
kutetea haki za wanyonge ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Wakati
umefika sasa wa kuirejesha hadhi ya CCM.
Kinyume
chake basi kauli aliyoitoa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Bila CCM
Madhubuti Nchi Itayumba” itatimia siku si nyingi. Pia nitumie fursa
kuwasihi vijana na wananchi kwa ujumla kuepuka matumizi ya nguvu, jaziba
na hasira pale wanapoandamana kwani hasira haimalizi hasira. Amani
ikishapotea ni vigumu sana kuirejesha.
Hitimisho
Nimalizie
kwa kusema kwamba kuiuwa nafsi isiyo na hatia ni dhambi kubwa sana
mbele ya Mwenyezi Mungu muumba wa mbigu na ardhi. Katika Quran Mwenyezi
Mungu anasema katika SURAT AL MAIDA (Sura ya 5: Aya 32) kwamba: “Kwa
sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu
bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi (ufisadi) katika nchi, basi ni
kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama
amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo
wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika
nchi.” Pia katika Biblia Mwenyezi Mungu katika Amri ya sita anasema
“USIUWE”. Iweje leo tunaanza kuuwana? Tutaiua Tanzania.
Namuomba
Mungu azidi kuibariki Tanzania. Adumishe Uhuru na Umoja kati ya
wanawake, wanaume na watoto wa Tanzania kwani Uhuru na Umoja wetu ndizo
ngao zetu za kuilinda na kuikinga amani yetu isitoweke.
Ndugu yenu
Amani Millanga
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)