ZAIDI ya watu 80,000 wakiwemo wa wanasiasa mashuhuri na watoto wao, watumishi wa umma, wafanyabiashara na wanasheria, wametajwa katika orodha ya wadaiwa sugu wa mikopo iliyotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) ili kufanikisha masomo yao katika vyuo mbalimbali nchini.
Katika orodha hiyo, BLOG HII imefanikiwa kuyaona majina ya vigogo katika taasisi mbalimbali, na watoto wa vigogo serikali katika vyama vya siasa.
Mbali ya kuanika majina hayo kwenye mtandao wa bodi, www.heslb.go.tz, pia bodi hiyo inakusudia kuwachukulia hatua za kisheria kwa watakaoshindwa `kujisalimisha’ na tayari kampuni nne za udalali zimeshapewa jukumu hilo.
Idadi kubwa ya watakaoingia katika `mshikemshike’ na bodi ni wale walionufaika na mikopo hiyo na kuhitimu kati ya mwaka 1994 na 2009 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo cha Usimamisi wa Fedha Zanzibar.
Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Cosmas Masobwa aliyesisitiza kuwa, lazima walionufaika wabanwe kwa kuwa walichokuwa wamepewa hakikuwa msaada au ruzuku.
“Sheria iko wazi kwamba baada ya kuhitimu, mnufaika anapewa mwaka mmoja wa kupumua, na baadaye anaanza kulipa bila riba.
“Kwa kuwa tumeshasumbuana vya kutosha, sasa hatutaki kusumbuana tena na wadaiwa hawa ninaoweza kuwaita ni sugu kwa sababu zaidi ya mara tatu tumeshawakumbusha kulipa, lakini hakuna mwitikio,” alisema Masobwa.
Alifafanua kuwa, wakati Bodi inaanzishwa mwaka 2005, ilirithi madeni ya serikali kiasi cha sh bilioni 51 kilichokuwa kimekopeshwa tangu mwaka 1992/3.
Na ili kuokoa kiasi hicho cha fedha na madeni mengine, sasa imelazimika kutumia nguvu ya ziada, kwa kuingia mkataba wa kukusanya madeni na makampuni ya Msolopa Investment Co. Ltd, Nakara Auction Mart na Sikonge International Co. Ltd ya Dar es Salaam na nyingine ya Dodoma, Dodoma Universal Trading Co. Ltd.
“Kazi ya makampuni haya itakuwa kuwachimbua huko wasikotaka kutoka, na tumekubaliana kwamba wadaiwa ndio watakaobeba gharama za usumbufu wa wakusanya madeni kuwafuata huko waliko.
“Na ikumbukwe baada ya muda huo, madeni yatakwenda sambamba na riba, ingawa kwa watakojitokeza sasa na kuweka wazi utaratibu wa malipo, hawataguswa,” alisema.
Akifafanua juu ya wahitimu ambao hawana ajira, alisema hilo si tatizo, bali mdaiwa anapaswa kuiarifu bodi kwa maandishi akielezea jina alilotumia akiwa chuoni, chuo alichohitimu, kozi aliyohitimu, mwaka aliohitimu, anuani yake na namba yake ya simu.
“Mara baada ya kupata taarifa za mdaiwa Bodi itampa maelezo yahusuyo deni lake na kujadiliana naye jinsi atakavyolipa deni. Endapo mdaiwa atashindwa kulipa deni lake atashtakiwa kwa mujibu wa sheria.
“Na endapo atachelewa kuanza kulipa deni lake atapewa adhabu ya ongezeko la asilimia 10 ya mkopo wake, ndiyo mwongozo wetu unavyosema,” alisema.
Akizungumzia suala la wadaiwa waliojiriwa, alisema nao wanapaswa kuwasiliana na bodi ili kupata maelezo sahihi ya mkopo na kueleza jinsi watavyolipa deni, huku wakiwajibika kuhakikisha makato kwenye mishahara yao yanawasilishwa HESLB.
Pamoja na kukatwa marejesho ya mkopo kwenye mshahara, wadaiwa pia wanaweza kuweka kiasi chochote cha fedha kwenye akaunti ya bodi ikiwa ni marejesho ya mkopo, kwa lengo la kupunguza haraka deni lake.
“Vivyo hivyo kwa aliyejiajiri, anapaswa kuwasiliana na bodi ikiwa pamoja na kueleza aina ya shughuli anayoifanya na mahali ilipo, na ndipo bodi itampa maelezo yahusuyo deni lake na namna ya kulipa deni,” alisema.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa kwa sheria ya Bunge Namba 9 ya mwaka 2004 na ilianza kufanya kazi mnamo mwezi Julai mwaka 2005.
Kwa mujibu wa sheria hii, baadhi ya majukumu makuu ya Bodi ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika masomo ya shahada au stashahada ya juu katika taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa na Serikali hapa nchini na nje ya nchi.
Aidha, sheria hii imeipa Bodi mamlaka ya kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu walionufaika na mikopo hiyo kuanzia mwaka 1994 ili pesa hizo ziweze kukopeshwa kwa wanafunzi wengine watakaohitaji.
Tangu mwaka 1994, kumekuwa na awamu tatu za ukopeshaji, ya kwanza ikianza kutekelezwa mwaka 1992/93 ambapo wanafunzi walitakiwa kujilipia gharama za usafiri kwenda chuoni na kurudi nyumbani, gharama za udahili na usajili pamoja na michango ya serikali za wanafunzi. Gharama hizi zilikuwa ni ndogo na kila mwanafunzi aliweza kuzimudu.
Katika awamu ya pili, mwanafunzi pamoja na kuchangia gharama zilizoainishwa katika awamu ya kwanza, alilazimika pia gharama za chakula na malazi. Gharama hizi ambazo kwa wakati huo zilifikia sh 350,000.00 kwa mwaka zilionekana kuwa kubwa kwa wanafunzi walio wengi.
Lakini, serikali katika kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa katika utoaji elimu ya juu, ilianzisha utaratibu wa mikopo ili wanafunzi ambao hawana uwezo wa kujigharamia waweze kukopeshwa moja kwa moja kutoka Serikalini. Utaratibu huu ulianza kutumika mwaka 1994/95 na uliendelea kutumika hadi mwaka 2004/2005.
Na katika awamu ya tatu iliyoanza utekelezaji wake mwaka wa masomo wa 2005/06 baada ya kuanzishwa kwa Heslb, mwanafunzi anapaswa kujigharamia pamoja na gharama zilizotajwa kwenye awamu ya kwanza na pili, gharama zote zingine za masomo, ama kwa njia ya mkopo kutoka kwenye Bodi au kwa njia zake mwenyewe.Kwa hisani ya http://heavytalio.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)