Waziri
wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka ( Mb) akimkabidhi kwa
niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkurugenzi wa
Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari,
Sergei Tarassenko, kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Andiko la kudai nyongeza ya maili
61,000 nje ya eneo la maili 200 la Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari wakati
wa hafla fupi iliyofanyika jana jumatano katika ofisi za Idara hiyo zilizopo katika Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani
NA MWANDISHI MAALUM
NEW YORK
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, imewasilisha katika Umoja wa Mataifa, Andiko
la kudai eneo la nyongeza lenye ukubwa wa maili 16,000 nje ya eneo la sasa la maili 200 za Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari. Waziri
wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anna Tibaijuka (Mb) ndiye
aliyewasilisha Andiko hilo, kwa niaba ya serikali, katika hafla fupi na
ya kihistoria iliyofanyika siku ya jumatano katika ofisi za Idara ya
Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Bahari na Sheria ya Bahari.
Andiko
hilo limepokelewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bw. Sergei Tarassenko
kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. ambaye aliipongeza
Tanzania kwa hatua hiyo muhimu na kuahidi kwamba Idara yake kupitia,
Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mipaka ya baharÃ
italifanyika kazi Andiko hili.
Aidha
Mkurugenzi huyo ameielezea Tanzania, kama moja kati ya nchi
inayoheshima sana na yenye historia nzuri katika Umoja wa Mataifa. Akizungumza
wakati wa kuwasilisha Andiko hilo, Waziri Anna Tibaijuka, amesema kwa
kuwasilisha Andiko hilo, Tanzania si tu kwamba imefanya kazi ya uhakika
ya maandalizi na hatimaye uwasilishaji lakini ni hatua kubwa kwa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania.
Akabanisha kwamba mchakato wa maandalizi ya Andiko hilo ambao umechukua miaka mitano,
umewashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo wa ndani na nje , ikiwa
ni pamoja na kuzihusisha nchi ambazo zinapakana kibahari na Tanzania.
Akizungumza
manufaa ya kudai nyongeza ya eneo hilo, Waziri Tibaijuka anasema. “
Tanzania itanufaika kwa kuongeza ukubwa wa eneo la mipaka ya nchi lakini
la msingi zaidi ni unufaikaji wa rasilimali zikiwamo za mafuta na gesi
na madini ambazo zitakuwamo katika eneo hilo jipya, rasilimali ambazo
kwa sasa zinaelekea kutoweka katika eneo la maili 200”.
Eneo ambalo Tanzania inadai liongezwe la maili 61, 000 ukubwa wake ni sawa na eneo la mikoa mitatu ikiunganishwa kwa pamoja.
Aidha
kuongezwa kwa eneo hilo kutaisaidia pia serikali katika masuala ya
ulinzi na usalama hasa katika kipindi hiki ambacho vitendo vya uharamia
wa baharini vikiwa vimeongeza katika eneo la bahari ya Hindi. “
Pamoja na kuwasilisha Andiko hilo, lakini nchi yangu inapenda pia kutoa
ombi la pekee kwa idara yako, kuangalia uwezekano wa kuharakisha
mchakato wa kupitia nyaraka na vielelezo tulivyowasilisha katika Andiko
letu, kwani itatusaidia sana katika ulinzi wa eneo la mipaka yetu dhidi
ya uharamia” akasisitiza Waziri .
Na
kuongeza kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo
zinaendelea zinatajitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali
ikiwamo Idara ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya bahari na sheria ya
bahari katika kuukabili uharamia.
Faida
nyingine ukiacha za kiuchumi ni kwa wataalamu wa fani mbalimbali kuwa
na fursa ya kufanya utafiti katika eneo hilo hapo litakapokuwa
limeridhiwa rasmi na kuwa sehemu ya Tanzania.
Baada
ya kuwasilisha Andiko hilo, hatua inayofuatia ni kwa Tanzania kupitia
wataalamu wake, itatakiwa kulitetea Andiko hilo mbele ya Makamishna wa
Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Mipaka ya Bahari utetezi
huo utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Tanzania
imewasilisha Andiko hilo kwa kuzingatia Sheria ya kimataifa ya Bahari
namba 76 kifungu kidogo cha 4, sheria hiyo inaziruhusu nchi ambazo ziko
kando kando ya bahari kudai eneo la nyongeza iwapo zitakidhi vigezo
vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa. Mchakato wa kuanda
Andiko hilo ulianza mwaka 2007 ukiwashirikisha wataalamu wa kada
mbalimbali kutoka Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu
cha Ardhi na Mazingira, Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Shirika la
Maendeleo ya Petroli ( TPDC).
Sehemu kubwa ya Mradi imefadhiliwa na Serikali Kuu na kwa kusaidiwa na Serikali ya Norway. Hafla
ya kuwasilisha Andiko hilo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania katika
Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue, na waheshimiwa wabunge, Zakhia
Meghji na Abulrahman Hassan Shah ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira. Wengine
waliohudhuri hafla hiyo ni baadhi ya wataalamu waliohusika na
maandalizi ya Andiko hilo ambao ni Dr. Sellasie Mayunga, Prof. Evelyne
Mbende, Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Bw. Kelvin Komba na Bi. Verdiana Mashingia.
Tanzania
inakuwa nchi ya 59 kuwasilisha Andiko la kudai nyongeza ya eneo la
bahari na ikiwa ni nchi 10 kutoka Afrika kufanya hivyo.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)