Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akifunua pazia
kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara ya
Uvuvi na Mifugo huko Maruhubi mjini Zanzibar. Nyumani kwake ni Waziri wa
Wizara hiyo Mheshimiwa Said Ali Mbarouk
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza
katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Wizara ya
Uvuvi na Mifugo huko Maruhubi mjini Zanzibar. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Mjini Magharibi Mheshimiwa Abdallah Mwinyi Khamis.
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Said Ali Mbarouk akitoa maelezo mafupi
kuhusiana na ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya Wizara hiyo
lililoko Maruhubi katika hafla ya ufunguzi uliofanywa na Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
---
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
utekelezaji wa sheria za uvuvi hauna lengo la kuwakomoa wavuvi na
wananchi bali ni kuleta ustawi kwa jamii na taifa kwa jumla.
Maalim
Seif ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua jengo la Makao Makuu ya
Wizara ya Mifugo na Uvuvi huko Maruhubi mjini Zanzibar ikiwa ni katika
shamra shamra za maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema
wakati serikali ikiandaa mipango yake ya maendeleo katika sekta ya
uvuvi, wananchi hawanabudi kuunga mkono mipango hiyo kwa kufuata sheria
zilizowekwa na wasione vibaya au kuhisi wameonewa wakati serikali
inaposimamia sheria hizo.
Ameitaka
wizara ya mifugo na uvuvi kuwaelimisha wavuvi juu ya umuhimu wa kufuata
sheria hasa katika maeneo ya hifadhi ya bahari na kuondokana na dhana
kuwa serikali inawaonea.
Amefahamisha
kuwa lengo la serikali ni kuwawezesha wananchi na kwamba juhudi za
kuanzisha benki ya mikopo kwa ajili ya wakulima, wavuvi, wafugaji na
wajasiriamali wengine iko mbioni, ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi
kujikwamua na umaskini.
“Si muda mrefu tunataka kiwepo chombo cha aina hiyo ili tuweze kuwasaidia wazanzibari”, alidokeza Maalim Seif.
Maalim
Seif amesema kuwa mkazo wa serikali kwenye sekta ya uvuvi na mifugo ni
kuzitanua sekta hizo ili ziweze kuleta tija kwao ikiwa ni pamoja na
kuongeza nafasi za ajira, ikizingatiwa kuwa sekta hizo zinawahusisha
watu wengi zaidi.
Makamu
wa Kwanza wa Rais ametumia fursa hiyo hiyo kuwaasa wavuvi kufanya
shughuli zao bila kuleta athari za kimazingira ya bahari.
Kwa
Upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Said Ali Mbarouk
amesema Wizara hiyo inakusudia kufanya Mapinduzi ya uvuvi na mifugo kwa
kuwawezesha wavuvi kuvua katika bahari kuu na kuepukana na uvuvi haramu.
“tunakusudia
kuufanya mwaka huu wa 2012 kuwa mwaka wa mapinduzi katika sekta zetu
hizi na utakuwa mwaka wa kutokomeza uvuvi haramu” alisema Mhe. Mbarouk.
Ameongeza
kuwa Wizara hiyo inashirikiana kwa karibu na Wizara ya Biashara,
Viwanda na Masoko kuitafutia ufumbuzi bei ya mwani duniani ili iendane
na mahitaji ya wakulima na gharama za uendelezaji, na kwamba kuna
matumaini ya mafanikio.
Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Bwana Kassim Gharib Juma amesema Wizara inajipanga
ili kuifanya sekta ya uvuvi iwe na tija zaidi kwa wavuvi ikiwa ni pamoja
na kuharakisha mipango ya kuwawezesha kuvua katika bahari kuu.
Ujenzi
wa jengo hilo lijuikanalo kwa jina la “Nyangumi House” umegharimu dola
za kimarekani milioni mbini na nusu na umetekelezwa na mradi wa MACEMP
chini ya ufadhili wa mkopo kutoka Benki ya Dunia WB.
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)