Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando.
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) iliyokutana Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam ilikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kupanga kalenda ya matukio ya mwaka 2012 ambayo chama kinatarajia kuyafanya.
Lakini licha ya kikao kutoa mapendekezo ya matukio mbalimbali, iliiagiza Sekretarieti ya TASWA ndiyo iiweke kalenda hiyo kwenye uhalisia, kulingana na hali halisi pamoja na mfuko wa chama utakavyoruhusu. Kalenda hiyo itakapokamilika itatolewa kwa wanachama wetu na wadau wengine.
Msisitizo mkubwa wa TASWA mwaka 2012 ni mafunzo ya aina mbalimbali kwa waandishi wa habari za michezo na wahariri wa habari za michezo kama njia mojawapo ya kuboresha taaluma ya habari.
Kutokana na hali hiyo TASWA imeandaa mafunzo ya siku tatu kuanzia Februari 20 hadi Februari 22,2012 jijini Tanga yakihusisha washiriki kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Mafunzo yatahusu masuala ya taaluma ya habari na mambo ya michezo mbalimbali ambayo itatangazwa baadaye.
Pia Machi 19, 20 na 21 mwaka huu yatafanyika mafunzo mengine Moshi mkoani Kilimanjaro, ambayo yatahusisha wahariri wa habari za michezo na waandishi waandamizi wa habari za michezo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika mafunzo hayo ya Moshi, pia zitatolewa mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya michezo hapa nchini.
MKUTANO MKUU AIPS
Mkutano Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo(AIPS) unatarajiwa kufanyika kuanzia Januari 12 hadi Januari 16 mwaka huu jijini Innsbruck, Austria.
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kama ilivyo kawaida itashiriki mkutano huo, ambapo mwaka huu itawakilishwa na Katibu Mkuu wa chama, Amir Mhando.
TASWA inamshukuru Mwenyekiti wa chama, Juma Pinto kwa kudhamini safari hiyo na ni matumaini ya chama kwamba mkutano huo utakuwa na manufaa makubwa kwa chama chetu.
MEDIA DAY
Mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusiana na bonanza la vyombo vya habari mwaka 2012 yapo hatua za mwisho, ni matumaini ya chama kwamba bonanza la mwaka huu litakuwa la aina yake.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
08/01/2012
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)