Hamad Rashid ‘kizimbani’ kesho - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Hamad Rashid ‘kizimbani’ kesho

MBUNGE wa Wawi kwa tiketi ya CUF, Hamad Rashid Mohamed na wanachama wenzake 13, kesho watapanda katika ‘kizimba’ cha chama hicho kujitetea.

Taarifa ya Kurugenzi ya Habari, Uenezi na Haki za Binadamu ya Chama hicho iliyotolewa jana, iliwataja wengine watakaojitetea mbele ya Baraza Kuu kutokana na tuhuma tofauti zinazowakabili, ni Doyo Hassan Doyo na Shoka Khamis Juma.

Wanachama wengine ni Juma Said Saanani, Yasin Mrotwa, Mohamed Albadawi, Mohamed
Masaga, Doni Waziri, Yusuf Mbungiro, Haji Nanjase, Ahmed Issa, Tamim Omar, Amir Kirungi na Ayub Kimangare.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanachama hao watajitetea katika ukumbi wa hoteli ya Mazsons mjini Unguja kuanzia saa 3 asubuhi kulingana na Katiba ya Chama ya mwaka 1992 kifungu cha 62 (1), kifungu cha 63 (1) (d) na kifungu cha 63 (1) (j).

“Kila mmoja atapata fursa ya kujitetea mbele ya Baraza Kuu kutokana na tuhuma tofauti zinazomkabili na kisha Baraza Kuu litaamua masuala husika kwa kadri litakavyoona inafaa na kwa mujibu wa Katiba,” ilisema taarifa.

Katika siku za karibuni umekuwapo msuguano wa ndani ya CUF hususan kwa upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na mbunge huyo wa Wawi na wanachama wengine, huku Hamad Rashid akitangaza wazi kuwania ukatibu mkuu wa chama hicho muda utakapojiri.
Desemba 30 kikao cha Kamati Tendaji ya Taifa ya chama hicho ilikutana kwa siku mbili kuwajadili wanachama hao wanaotuhumiwa kula njama za kukivuruga chama akiwamo Hamad Rashid.

Kikao hicho kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu, Julius Mtatiro, kiliongozwa na Maalim Seif na kilipokea taarifa ya hali ya kisiasa kutoka kamati ndogo ya Ulinzi na Usalama ya chama hicho.

Hamad Rashid na watuhumiwa wenzake, wanadaiwa kulalamikia chama hicho kukosa mwelekeo na kupoteza nguvu za kisiasa kwa kasi kubwa huku pia kikikabiliwa na matumizi mabaya ya fedha.
Tuhuma hizo ziliwafanya wanachama hao kutaka baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya CUF waondolewe, kwa kuwa wanakabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa; hilo likielekezwa waziwazi kwa Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
chanzo na habarileo

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages