Balozi Mpya wa Tanzania Nchini Misri Amtembelea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Balozi Mpya wa Tanzania Nchini Misri Amtembelea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na Balozi mpya wa Tanzania nchini Misri balozi Mohd Hamza aliyefika Ofisini kwake Migombani kwa lengo la kuagana nae wakati akijitayarisha kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi nchini Misri.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimpa nasaha balozi mpya wa Tanzania nchini Misri balozi Mohd Hamza aliyefika Ofisini kwake Migombani kwa lengo la kuagana nae wakati akijitayarisha kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi nchini Misri.Picha, Salmin Said-Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
----
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar na Misri zina uhusiano mkubwa wa kidugu na kihistoria katika nyanja za kiuchumi, kijamii na maendeleo na kuna haja uhusiano huo ukaendelezwa na kuimarishwa zaidi. 


Maalim Seif amesema hayo huko ofisini kwake Migombani, alipokuwa na mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Misri, Balozi Mohammed Hamza aliyefika kwa ajili ya kumuaga baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kushika wadhifa huo.

Maalim Seif amesema hata kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Zanzibar na Misri tayari zilikuwa na ushirikiano katika nyanja tafauti, ushirikiano ambao umeendelezwa kwa nguvu zaidi baada ya Mapinduzi na wananchi wa Zanzibar wananufaika sana kwa kuwepo ushirikiano huo.

Makamu wa Kwanza wa Rais ameyataja miongoni mwa maeneo ambayo Zanzibar inanufaika kufuatia ushirikiano huo, kuwa ni pamoja na sekta ya afya, kilimo, michezo na elimu na kumuhimiza Balozi Hamza kuendeleza mafanikio yaliyokwishapatikana na kutafuta maeneo mengine ya ushirikiano, ambapo Zanzibar na Tanzania zinaweza kunufaika.


“Wenzetu hawa tunashirikiana vizuri, hivi karibuni niliwahi kuzungumza na balozi wao mdogo aliyepo Zanzibar na nikamuomba atutafutie nafasi za masomo kuhusiana na taaluma mbali mbali ikiwemo ya uchimbaji wa mafuta, nashkuru balozi alitukubalia na kutupatia nafasi tatu”, alisema Maalim Seif.

Makamu wa Kwanza wa Rais pia amemtaka balozi Hamza kutumia uwezo wake kutafuta namna nchi hiyo inavyoweza kuisaidia Zanzibar katika mipango yake ya kukabiliana na maafa na uokozi, akieleza kuwa Misri ina uzoefu mkubwa katika masuala hayo.

Licha ya kuteuliwa kuwa balozi wa wa Tanzania nchini Misri, Balozi Hamza pia ataziwakilisha nchi nyengine saba za ukanda huo zikiwemo Syria, Jordan, Lebanon, Iraq, Israel na Libya.
Kwa upande wake, Balozi Hamza aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Misri na Zanzibar, pamoja na Tanzania kwa ujumla, kwa faida ya wananchi wa pande mbili hizo.
Amesema Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Misri yakiwemo utunzaji wa historia pamoja na mipango miji, mambo ambayo ameahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika katika nyanja hizo.

Hassan Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar 

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages