WAZIRI NCHIMBI AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI KWA BIDII. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAZIRI NCHIMBI AWATAKA VIJANA KUFANYA KAZI KWA BIDII.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi akizungumza na vijana 400 wa mkoa wa Pwani na wilaya ya Korogwe (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo maalum yaliyoandaliwa na mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwaondoa vijana katika maeneo yanayowadhalilisha na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mantumu Mahiza. 
Vijana 400 kutoka mkoa wa Pwani na Wilaya ya Korogwe wakifuatilia kwa makini hotuba ya Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo wakati akifunga mafunzo maalum yaliyoandaliwa na mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwaondoa vijana katika maeneo yanayowadhalilisha na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa na maisha bora.
Na Lydia Churi, MAELEZO - PWANI.
Vijana wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuacha uvivu ili waweze kujiletea maendeleo.
Akifunga mafunzo ya siku moja ya Vijana wa Mkoa wa Pwani na wilaya ya Korogwe yaliyoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Pwani jana Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Nchimbi alisema vijana wanapaswa kuepuka tabia ya uvivu na badala yake wahakikishe wanakuwa na mtazamo mpya wa kujiletea maendeleo
“Mabadiliko ya kijana yatatokana na uamuzi wa kijana mwenyewe katika mipangilio ya maisha yake, alisema.
Kuhusu suala la mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Nchimbi alisema katiba ya miaka 50 ijayo itawahusu zaidi vijana wa sasa hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yao wakati utakapofika.
Akizungumzia ugonjwa wa ukimwi, Waziri Nchimbi alisema ugonjwa huo haujaisha na dawa zote zinazotangazwa kutibu maradhi hayo hakuna iliyofanikiwa kutibuhivyo aliwataka vijana kuzungumzia kwa Uwazi na bila ya aibu njia za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo yakiwemo matumizi sahihi ya kondomu.
Alisema kuwa taifa lijalo litawategemea sana vijana na hakutakuwa na taifa iwapo vijana wote watapotea kutokana na ugonjwa wa ukimwi. Aliongeza kuwa nchi imepoteza wataalamu wengi hivyo vijana hawana budi kuhakikisha kuwa hawapati maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema uamuzi wa kijana kuishi maisha marefu kwa kukwepa maambukizi ya virusi vya ukimwi ni wa kijana mwenyewe. Aliongeza kuwa Asilimia 90 ya maambukizi ya Ukimwi yanatokana na ngono zisizo salama na kwamba vijana ndiyo wanaoongoza kwa kutopenda kufa wakati huohuo wakipenda ngono zisizo salama jambo ambalo haliwezekani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bibi Mwantumu Mahiza alisema Mkoa wake uliamua kuwakutanisha vija na wapatao 400 kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Pwani na wilaya moja ya Mkoa wa Tanga (Korogwe) ili kuwaondoa vijana katika maeneo yanayowadhalilisha na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Alisema, mkakati wa Mkoa wake ni kuwakutanisha vijana wengi zaidi wenye umri wa kati ya miaka 18- 25 katika Kambi ya Maarifa na kuwapatia maarifa na ujuzi watakaoupenda zikiwemo stadi za kilimo cha kisasa ili waweze kujitegemea. Aliongeza kuwa mkoa wa Pwani unazo rasilimali nyingi ambazo haziwasaidii vijana, hivyo kwa kupitia kambi hizo vijana watafaidika.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, wakuu wa wilaya na baadhi ya wabunge.(Picha na Lydia Churi Maelezo)

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages