
WADAU WASAIDIE TWIGA STARS
Timu
ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) inaendelea na mazoezi jijini Dar es
Salaam chini ya Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa kujiandaa kwa mechi
ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Namibia
baadaye mwezi ujao.
Mechi
hiyo ya kwanza itachezwa ugenini Januari 14 mwakani jijini Windhoek.
Timu hiyo ambayo sasa inafanya mazoezi kwa wachezaji kutokea majumbani
(off camp) inatarajia kuingia kambini Januari Mosi mwakani.
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linahitaji zaidi ya sh. milioni 50
ikiwa ni gharama za safari, kambi na posho kwa wachezaji na benchi la
ufundi kwa ajili ya mechi hiyo moja tu. Mechi ya marudiano itachezwa
Januari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tunatoa
mwito kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi, kampuni na watu binafsi
kusaidia ushiriki wa Twiga Stars kwenye mechi hiyo na michuano hiyo kwa
ujumla. Twiga Stars kama ilivyo kwa timu nyingine za Taifa ukiondoa
Taifa Stars bado haina mdhamini.
WAAMUZI 14 WAPATA BEJI ZA FIFA
Waamuzi
14 wakiwemo wawili wapya wamefanikiwa kupata beji za Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2012 baada ya kufaulu
mtihani wa waamuzi uliofanyika mwaka huu na kusimamiwa na shirikisho
hilo.
Ferdinand
Chacha na Ali Kinduli ambao ni waamuzi wasaidizi ndiyo wapya katika
jopo hilo la waamuzi wa FIFA kwa Tanzania. Waamuzi wa kati waliopata
tena beji hizo ni Ramadhan Ibada, Orden Mbaga, Israel Mujuni na Sheha
Waziri.
Mbali
ya Chacha na Kinduli, waamuzi wengine wasaidizi kwa upande wa wanaume
ni Josephat Bulali, Hamis Changwalu, Erasmo Clemence, Khamis Maswa na
Samuel Mpenzu. Kwa upande wa wanawake, mwamuzi wa kati ni Judith Gamba
wakati wasaidizi ni Mwanahija Makame na Saada Tibabimale.
Mwamuzi pekee wa FIFA 2011 ambaye jina lake halikurudi ni John Kanyenye ambaye alikuwa mwamuzi msaidizi.
TAIFA STARS, DRC KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI
Timu
ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imeomba kucheza
mechi moja ya kirafiki na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).
Mechi hiyo itafanyika Februari 23 mwakani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
DRC
inatarajia kuwasili nchini Februari 18 mwaka huu ambapo itaweka kambi
yake ya mazoezi hadi Februari 25 mwaka huu kujiandaa kwa mechi yao ya
mchujo ya Kombe la Afrika (CAN) dhidi ya Mauritius.
Mechi
ya DRC na Mauritius itachezwa Februari 29 mwakani nchini Mauritius.
Stars yenyewe itacheza mechi ya kwanza ya mchujo kwa ajili ya fainali
hizo za 2012 zitakazofanyika Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji. Mechi hiyo
itachezwa Februari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
13 WASHIRIKI KOZI YA UKAMISHNA
Kozi
ya siku mbili ya ukamishna iliyomalizika Desemba 29 mwaka huu
imeshirikisha washiriki 13 chini ya ukufunzi wa Stanley Lugenge, Leslie
Liunda na Sunday Kayuni.
Walioshiriki
kozi hiyo ni Abdallah Zungo, Ally Mkomwa, Ally Mozi, Army Sentimea,
Awadi Nchimbi, Beatus Manga, Christopher Mpangala, Hakim Byemba,
Josephat Magazi, Juma Mgunda, Juma Mpuya, Mugisha Galibona, Ramadhan
Mahano, Robert Kalyahe na Said Nassoro.
Wakufunzi
wanaendelea kusahihisha mitihani ya washiriki na baada ya kazi hiyo
kwa ambao watakuwa wamefanya vizuri majina yao yataingizwa katika
orodha ya makamishna kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na
mashindano mengine yanayosimamiwa moja kwa moja na TFF.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHUKA, NGAHYOMA
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya
waandishi wa habari Halima Mchuka wa Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) na John Ngahyoma wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC)
vilivyotokea Desemba 29 na 30 mwaka huu.
Misiba
hiyo ni mikubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa
nyakati tofauti Ngahyoma na Mchuka walishafanya kazi na TFF, hivyo
mchango wao katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima. Ngahyoma baada ya
kumaliza chuo cha uandishi wa habari mwishoni mwa miaka ya 80 alijiunga
na Daily News ambapo alianza kwa kuripoti habari za michezo, hasa
mpira wa miguu.
Mchuka
naye tutamkumbuka kama mtangazaji wa mpira wa miguu ambapo mara ya
mwisho tulifanya naye kazi kwa karibu mwaka 2005 ambapo alikuwa mjumbe
wa Kamati ya Habari ya TFF kwa ajili ya michuano ya klabu bingwa Afrika
Mashariki na Kati iliyofanyika jijini Mwanza.
TFF
inatoa pole kwa familia za marehemu Ngahyoma, Mchuka, BBC na TBC na
kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
misiba hiyo mizito.
Mungu aziweke roho za marehemu Ngahyoma na Mchuka mahali pema peponi. Amina





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)