Mwaka wa migomo, maandamano na vurugu vyuo vikuu vya umma - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Mwaka wa migomo, maandamano na vurugu vyuo vikuu vya umma

Na Fredy Azzah
MWAKA 2011 ulianza na umemalizika kwa  maandamano na migomo katika taasisi  mbalimbali za elimu ya juu hususan vyuo vikuu vya umma.

Mara nyingi migomo hiyo iliambatana na vurugu zilizofanywa na wanafunzi, hivyo kulazimisha askari wa kikosi cha  kuzuia fujo kutumia nguvu kutuliza hali ya mambo katika vyuo hivyo, hali iliyosababisha wanafunzi kadhaa kukamatwa na kusekwa rumande.

Pamoja na mambo mengine, chanzo kikubwa cha maandamano na migomo hiyo  ilikuwa kuishinikiza Serikali kuyafanyia kazi madai yao mbalimbali,  ikiwamo kuongezewa posho za kujikimu, usawa katika utoaji wa mikopo na uhaba wa  wahadhiri vyuoni.

 Makala haya yanadurusu baadhi ya matukio hayo kama yalivyotokea katika vyuo vikuu mbalimbali vya umma mwaka huu

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Februari nne mwaka huu, askari wa jeshi la Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na hata risasi za moto kuwakabili wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU)   waliokuwa wakijibu mapigo ya mashambulizi ya wanafunzi hao waliokuwa wakiwarushia mawe.

Vurugu hizo zilizosababisha mmoja wa wanafunzi kupoteza ujauzito, zilitokana na wanafunzi hao kufanya  maandamano kuelekea Ikulu wakishinikiza nyongeza ya fedha ya posho wanayopewa na Serikali kutoka Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa siku.

Taarifa zinasema maandalizi ya maandamano hayo  yalianza kusukwa siku moja kabla  katika hosteli za Mabibo.

Kesho yake saa mbili asubuhi, wanafunzi walikuwa wamefika kampasi kuu ya  Mlimani (sasa kampasi ya Mwalimu Nyerere)  kwa ajili ya maandamano hayo, kabla ya kusambaratishwa na askari katika mapambano yaliyodumu kwa karibu saa moja.

 Katika kujaribu kusuluhisha migogoro chuoni hapo,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alijikuta katika wakati mgumu baada ya gari alilokuwamo kunusurika kuvunjwa vioo na wanafunzi wa chuo hicho ambao hawakuridhika na jinsi alivyokuwa akishughulikia madai yao.

Wanafunzi hao ambao walikuwa wameungana na wenzao kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) walikusanyika katika eneo la uwanja wa mpira kumsubiri Waziri huyo aliyetarajia kujibu hoja nne zilizohusu madai yao.

Kwa mujibu wa wanafunzi madai hayo yalijumuisha ongezeko la fedha za kujikimu kutoka Sh5,000  hadi 10,000 na Serikali itoe fedha za dharura kwa wanafunzi wote kiasi cha Sh 100,000 kwa ajili ya kujinusuru na njaa hadi hapo mitihani ya kumaliza muhula.

Madai mengine yaliyotolewa na wanafunzi hao ni kumtaka Waziri  kutoa tamko la kufuta kesi iliyokuwa ikiwakabili   wanafunzi wenzao waliokamatwa awali kwa kosa la kuishinikiza  Serikali kufanyia kazi madai yao.

Hatima ya migomo na vurugu za mara kwa mara chuoni hapo, zikasababisha Novemba 14, wanafunzi 50 kufikishwa katika mikono ya sheria huku 22 wakisimamishwa masomo kwa kudaiwa kuwa vinara wa vurugu zilizotokea Novemba 11.

Kama haitoshi, Desemba 14 uongozi wa chuo hicho kikongwe nchini ukatangaza kuwafukuza chuo wanafunzi 43, huku ukitangaza kuendelea kufuatilia nyendo za wengine tisa, baada ya kubainika kuwa walihusika katika matukio mbalimbali ya vurugu na uhalifu chuoni hapo.

Kati ya wanafunzi hao, wanane walikuwa  wamesimamisha masomo kwa muda wa miezi tisa na 35 walisimamishwa ili kusubiri kumalizika kwa kesi zao zilizopo mahakamani.

Chuo Kikuu cha Dodoma

Japo chuo hiki bado kigeni, lakini  ndani ya muda mfupi wa uhai wake, kimekuwa kikikabiliwa na vurugu za mara kwa mara kati ya wanafunzi na uongozi wa chuo.Baadhi ya nyakati vurugu hizo huhusisha pia wanafunzi na Serikali hasa kuhusu masuala ya mikopo na madai mengine.

Juni 13 mwaka huu, wanafunzi hao wakazua taharuki kubwa  katika viwanja vya bunge baada ya  mabomu kusikika karibu  na ukumbi wa bunge ambapo kikao cha tatu katika mkutano wa nne wa Bunge kilikuwa kikiendelea.

Hali hiyo ilitokana na Polisi kupiga mabomu kwa ajili ya kuwazuia wanafunzi wa chuo hicho  ambao walitaka kuvamia ukumbi wa bunge kwa ajili ya kuonana na Waziri Mkuu ili wafikishe kilio chao.

Lengo la maandamano hayo lilikuwa kumshinikiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa wajiuzulu kwa kile walichodai kuwa wamewadanganya.

Awali, Januari  mwaka huu,wahadhiri wa chuo hicho  waligoma kufundisha kutokana na madai mbalimbali ikiwemo kutaka maslahi bora.

Aidha, wahadhiri hao walidai mmoja wa viongozi wa juu wa chuo alikuwa akizichakachua fedha zao,madai yaliyomfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwenda Udom kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za chuo.

Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili

Desemba 15,  Uongozi wa  Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), ulitangaza kuwasimamisha masomo wanafunzi 66 kwa tuhuma za kuwa vinara wa vurugu chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo alisema  wanafunzi waliosimamishwa ni wale waliohusika katika vurugu zilizotokea chuoni hapo Desemba 8 mwaka huu wakati wa sherehe ya utafiti na Desemba 10 wakati wa mahafali.

Profesa Pallangyo alisema wanafunzi hao wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana hadi hapo uchunguzi utakapokamilika, na kwamba matokeo ya uchunguzi huo ndio yatakayoamua kama wanafunzi hao waendelee na masomo ama la.Credits MWANANCHI NEWSPAPER

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages