MBUNGE wa Wawi Hamad Rashid Mohammed atunishia msuli CUF - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MBUNGE wa Wawi Hamad Rashid Mohammed atunishia msuli CUF


MBUNGE wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) ameigomea Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho kumhoji na kumjadili kuhusu tuhuma zinazomkabili za kukiuka Katiba, akidai hana imani na wajumbe wake.  Pia ameigomea kwa kudai kuwa tayari alishafahamu kwamba Kamati hiyo ilikuwa na maamuzi ya kumfukuza uanachama, kupitia barua pepe aliyoinasa ikitoka kwa Katibu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwenda kwa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mh Hamad ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF alisema alipokea barua ya kuitwa kuhojiwa kwa tuhuma za kwenda kinyume cha Katiba ya CUF, Desemba 23, mwaka huu na kikao hicho kilifanyika rasmi jana. 

Alisema baada ya kuhudhuria kikao hicho, alilazimika kukigomea kuendelea kumjadili kutokana na kutokuwakubali wajumbe watano kati ya wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali na Katibu wake Hamis Hassan.

Alisema viongozi hao wawili amewakataa kutokana na ushiriki wao katika kumtuhumu. Alisema hana imani na Machano baada ya kiongozi huyo kuahidi kumshughulikia katika kikao kilichofanyika hivi karibuni bila ya kumpa nafasi ya kusikiliza upande wake. 

Aidha, kwa upande wa Hassan, Hamad alisema Katibu huyo alimtuhumu kwa kumuandikia Lipumba barua na kumtuhumu kuwa (yeye) ni chachu ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa ndani ya chama na kwamba pamoja na washirika wake, wamekuwa wakifanya mbinu za chini kwa chini kumuondoa Lipumba kwenye nafasi yake. Alisema pia katika Katiba ya CUF hakuna kipengele chochote kinachozungumzia Kamati ya Nidhamu na maadili hivyo alikuwa na sababu ya kuikataa Kamati hiyo. 

Pamoja na hayo, pia alisema sababu iliyomfanya aigomee Kamati hiyo ni baada ya kufahamu kuwa tayari wajumbe wake walikuwa na uamuzi wa kumfukuza uanachama kupitia barua pepe ya Maalim Seif kwenda kwa Lipumba.  Aliinukuu barua pepe hiyo ambayo ilisema “Nimeshauriana na Makamu tumeona kuna ahadi ya jamaa yako (Hamad) na genge lake kuitwa kwenye Kamati ya Nidhamu kuhojiwa, ushahidi wa kutosha umekusanywa dhidi yake…Kamati hiyo italeta taarifa kwa Kamati Kuu ya Taifa. 

“Kamati Kuu ya Taifa ifanye uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uongozi vinara wao na wengine kupewa karipio, Kamati hiyo ifikishe taarifa yake katika kikao kitakachofanyika Februari mwakani... muono wetu tumfukuze kwenye chama na akienda mahakamani, ikitoa uamuzi wa kumpendelea, mwache awe Mbunge wa Mahakama kama akina Asha Ngede na Naila Majid,” Hamad alinukuu barua pepe hiyo. 
Aidha, alisema katika barua pepe hiyo, Maalim Seif alimshauri Lipumba kuwa ikiwezekana na Hamad Rashid aachwe hata akienda Chadema, CCM au aendelee na urafiki wake na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. 

“Jamani hii ni dhambi kubwa anayoifanya Maalim Seif, mimi namheshimu sana na ndio maana nataka ajipime mwenyewe kwani haya ndio yaliyomfanya Jumbe ajiuzulu,” alidai mwanasiasa huyo mkongwe. 
Alisema hana ukaribu wowote na Lowassa zaidi ya kusalimiana kawaida kama watu wengine. Alisema amezushiwa mambo mengi, ameitwa muasi na anataka kukibomoa chama, wakati amekuwa kiungo muhimu baina ya Wazanzibari na Wabara ndani ya CUF.  Aidha, alisema amesaidia kampeni hadi ya Lipumba wakati wa uchaguzi na kufadhili baadhi ya wabunge tofauti na Maalim Seif, aliyedai hajawahi hata kufungua mkutano mmoja wa chama Bara. 

“Namuomba Maalim Seif kwa hali iliyofikia kama anataka kujisafisha na kuheshimika, basi afuate nyendo za aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela na Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere,” alisema. 
Alisema hali ya chama hicho ni tete kwa kuwa hakiendeshwi kwa haki na mambo mengi ya kusingiziana na kuzushiana huku fedha nyingi zikitumika bila maelezo na iwapo watu wakihoji wanaitwa waasi. 
Alihoji inakuwaje chama hicho kimekaa zaidi ya miaka mitatu na CCM kujadili muafaka wa Zanzibar na kushindwa kukaa hata kikao kimoja kujadili na kufikia muafaka kuhusu mgogoro unaoendelea.  Naye mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Doyo Hassan Doyo, alisema wanachokitaka kwa sasa ni kukirejesha chama hicho katika hali inayokubalika kwa pande zote Bara na Visiwani ikiwemo kuhakikisha fedha za ruzuku za chama zinafikia maeneo yote. 

“Sisi tunapata kwa mwezi Sh milioni 124 na michango ya fedha za wabunge takribani Sh milioni 60, jumla ni Sh milioni 190 hadi 200 lakini fedha hizi zinaishia makao makuu, huko wilayani watu wanazisikia tu, tukihoji tunaitwa waasi,” alidai Doyo. Kwa sasa sakata hilo, baada ya Hamad Rashid kuigomea Kamati ya Nidhamu na Maadili linasubiri kuwasilishwa wakati wowote mbele ya Baraza Kuu la CUF kwa majadiliano zaidi.
Chanzo: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages