Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa
Ubungo, John Mnyika.
*JK
awakubalia CUF kwenda Ikulu
SIKU moja baada ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya Mwaka 2011 kutiwa saini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimeibuka na msimamo mpya kikisema hakitashiriki hatua yoyote
ya kuandika katiba iwapo Rais Jakaya Kikwete, ataruhusu sheria hiyo
kutumika kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kabla haijarudishwa
kwa wananchi ili ijadiliwe na kufanyiwa marekebisho.
Msimamo
huo wa Chadema, ulitangazwa na Kaimu Katibu Mkuu wake, John Mnyika,
alipozungumza na waandishi wa habari, kufafanua mambo yaliyoibuka baada
ya kamati iliyoundwa na vigogo wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti
taifa, Freeman Mbowe, kukutana na Rais Kikwete na ujumbe wa serikali
yake, kwa siku mbili mfululizo Ikulu, kuanzia, Novemba 28, mwaka huu na
kufikia makubaliano.
Mnyika,
ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Katibu wa Wabunge wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, alisema iwapo Rais Kikwete hataruhusu sheria hiyo
kufanyiwa marekebisho, makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo yao,
hayatakuwa na maana.
Alisema
katika mazungumzo hayo, pande zote mbili ziliona sheria hiyo kuwa ina
upungufu, hivyo inahitaji kuboreshwa.
Mnyika
alisema baada ya kuona kwamba kuna haja hiyo, walimshauri Rais Kikwete,
kutumia mamlaka yake ya Kikatiba kutosaini muswada wa sheria hiyo,
lakini ushauri wao huo umepuuzwa.
Hata
hivyo, alisema pamoja na kupuuza ushauri wao wa kutokusaini, Rais
Kikwete amekubaliana kwamba kuna haja ya kuboresha sheria hiyo, ikiwa ni
pamoja na kutoa mwito wa kupeleka maoni juu ya marekebisho hayo.
“Hivyo,
tunataraji Rais hataunda tume ya kukusanya maoni mpaka atakapokamilisha
mchakato wa sheria hiyo kufanyiwa marekebisho. Na hii italeta maana ya
makubaliano tuliyofikia,” alisema Mnyika.
Aliongeza:
“Kabla sheria haijaanza kutumika, irudishwe kwa wananchi ili watoe
maoni.”
Akielezea
sababu za pande mbili za mazungumzo kukubaliana kuwapo mawasiliano na
mashauriano ya mara kwa mara kati ya serikali na wadau mbalimbali juu ya
kuboresha sheria hiyo, Mnyika alisema walizingatia jambo hilo kwa vile
Katiba ni mali ya Watanzania.
Alisema
kama wasingefikia makubaliano hayo, wangekuwa wamefanya makosa
yaliyofanywa na serikali kwa kujifungia ndani na kutengeneza muswada wa
sheria hiyo na kisha kuupeleka bungeni bila kuwashirikisha wananchi.
Alisema
miongoni mwa vipengele wanavyopinga kuwamo kwenye sheria hiyo, ni
pamoja na kinachohusu uanzishwaji wa Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya
kutoa maoni juu ya rasimu ya katiba.
Mnyika
alisema sheria hiyo inakataza mtu yeyote kufanya shughuli ya kukusanya
na kuratibu maoni ya wananchi au kuendesha elimu juu ya mabadiliko ya
Katiba, ambapo alisema adhabu kwa yeyote atakayetiwa hatiani kwa makosa
hayo, ni faini ya kati ya Shilingi milioni tano hadi Sh. milioni 15 au
kifungo cha kati ya miaka mitatu hadi saba au vyote kwa pamoja.
Alisema
masharti hayo ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana madhara makubwa
sana sio tu kwa mchakato wa utungaji wa Katiba Mpya, bali pia kwa haki
za kibinadamu na za kikatiba zinazotambuliwa na kulindwa na Katiba na
sheria za nchi pamoja na sheria za kimataifa, ambazo Tanzania
imeziridhia.
Kuhusu
sheria hiyo kuanza kutumika leo, alisema jambo hilo siyo lazima, kwani
hata mwaka 1984, Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi
kusaini sheria, lakini ilianza kufanya kazi baada ya miaka mitatu.
Alisema
pia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010, haikuanza kufanya kazi
ila baada ya kufanyiwa marekebisho.
Kutokana
na hayo, alitangaza rasmi msimamo wa Chadema akirejea azimio la sita la
Kamati Kuu ya Chadema iliyofanya kikao chake Novemba 20, mwaka huu,
linalosema kwamba ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kupata katiba
mpya uliowekwa na sheria hiyo, utategemea utayari wa serikali kufanya
mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la
kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.
Hivyo,
akasema: “Chadema hatutashiriki mchakato wowote unaotokana na sheria
hiyo iwapo haitafanyiwa marekebisho.”
Alisema
pia kutokana na makubaliano waliyofikia katika mazungumzo na Rais
Kikwete, wamesitisha maandamano, lakini hawajasitisha kazi za chama
kuhusu mchakato wa suala la katiba.
Mnyika
alisema Chadema wataendelea kutoa elimu juu ya ubovu wa sheria hiyo kwa
kufanya mikutano ya ndani na hadhara. “Tunataraji serikali italeta
katika Bunge lijalo marekebisho ya sheria hiyo kwa kuzingatia maoni ya
wananchi,” alisema Mnyika.
JK
KUKUTANA NA CUF
Wakati
huo huo, Ofisi ya Rais, Ikulu, imepokea barua kutoka Chama cha Wananchi
(CUF) kikiomba kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa
iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema
kuwa Rais amekubali ombi hilo la CUF na ameelekeza maandalizi ya mkutano
huo yafanyike mara moja.
CHANZO:
NIPASHE www.ippmedia.com
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)