TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Hivi
karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa
karibu ya asilimia 200, kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000.
Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha bunge kwa siku.
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimefuatilia kwa makini suala hilo la nyongeza ya
posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya
habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dk. Thomas
Kashilila na Spika wa Bunge Anne Makinda.
Kwa
namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kukaa
kulikalia kimya na hivyo imetoa msimamo wake kama ifuatavyo:-
i.
Linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda
kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo
wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani
ya jamii.
ii.
Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza
pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii
yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.
iii.
Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba
sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za
maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo
inasababishahofu na mashaka miongoni mwa Watanzania. Na kwa kweli swali
kubwa kwa Watanzania hao ni je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa
wabunge tu?
Hivyo
basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu
kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na
swala hili, kulitafakari upya jambo hili.
Tunaamini
busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza
kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo
Walimu, askari, Madaktari na wengineo.
Ni
muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa
wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha
ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha
bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo
ambalo ni hatari.
Katika
hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawapongeza sana Watanzania
kwa ujumnla wao, bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kwa kushiriki
kwa amani na utulivu katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania
Bara.
Ushiriki
wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane sana. CCM inaamini
kuwa maadhimisho haya ya miaka 50 yatatumika kuendelea kujenga uzalendo,
umoja na mshikamano wan chi yetu katika kufikia maendeleo.
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
11/12/2011
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)