Taarifa ya
TBC imeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amepokea kwa furaha ombi la
viongozi wa CHADEMA la kutaka kuonana naye ili kuzungumzia sheria ya
mchakato wa uandaaji wa katiba, na amewaagiza maafisa wake kuandaa
mkutano huo. Kwangu mimi naona hii ni busara kubwa ambayo Rais
ameonesha tofauti na baadhi ya watu ambao wangependa Rais akatae. Wapo
pia wale ambao hawakupenda viongozi wa CHADEMA kutoa ombi hilo kwa
Rais, wangependa mara moja maandamano yaanze bila ya nafasi yoyote ya
kufanya mazungumzo.
Kwangu mimi, kama dhamira yetu ni kupata katiba iliyo nzuri, na
hakuna hila upande wowote nyuma yake, tuna haki ya kumpongeza Rais JK
na viongozi wa CHADEMA kwa kuruhusu mazungumzo kwanza kabla ya jitihada
nyingine zozote.
Ombi langu kwa Rais na kwa viongozi wa CHADEMA waende
katika mjadala huo kwa dhamira moja kubwa - YA KUPATA KATIBA ILIYO
BORA. Dhamira ya viongozi wa CHADEMA na RAIS iwe ni kupata katiba iliyo
bora kabisa Afrika, kwa sababu hilo linawezekana kama tukinuia. Kusiwe
na mawazo ya kutafuta ushindi, na kila upande uwe tayari kuusikiliza
upande mwingine, kila upande ukiamini kuwa wote wana dhamira njema.
Siyo mjadala wa mashindano kati ya Rais na CHADEMA au CCM na CHADEMA,
uwe ni mjadala wa kupata katiba iliyo bora kabisa katika Taifa letu.
Nawashauri Jukwaa la Katiba, nao wachukue kwanza njia hii ambayo
CHADEMA wameamua kuichukua kuliko kwenda kwenye maandamano bila ya kuwa
na uhakika kuwa matakwa yao Rais anaweza kuyasikiliza au la. Tufahamu
kuwa bado haijawa sheria, itakuwa sheria tu baada ya Rais JK kuweka
saini yake. Rais toka Mwanzo amechukua msimamo tofauti kuhusu suala la
katiba.
Tukumbuke kuwa Waziri wa sheria alikataa, mwanasheria mkuu
alikataa, na wengi ndani ya CCM walitamka hakuwezi kuwa na katiba mpya.
Rais JK akatamka wazi kuwa Tanzania itapata katiba mpya.
Nina imani Rais kama binadamu yeyote, baada ya baadhi ya viongozi
wenzie kusema hakuna haja ya kuwa na katiba mpya, na yeye kutofautiana
nao, hatakuwa tayari kuwapa nafasi wale waliokuwa wakipinga waonekane
kuwa walikuwa sahihi. Nadhani Rais atapenda jambo hili lifanikiwe.
Kwa
JK hii ndiyo itakuwa 'legacy' yake kubwa katika Taifa hili, itakayodumu
kwa miaka mingi.
Namshauri Rais, katika hili la katiba ashirikiane na mtu yeyote
mwenye nia njema ya kupata katiba nzuri bila ya kujali mtu huyo ana
itikadi gani. Na wale wote tunaolalamikia katiba iliyopo, na sheria
iliyopitishwa hivi karibuni ili kupata katiba mpya, kwa kuwa inaonekana
Rais yupo tayari kutoa nafasi kwa yeyote ya kusikilizwa, tuitumie
nafasi hii vizuri, tukijadiliana na kushauriana kwa dhamira njema.
Tundu Lisu, ni mwanabidii, na yupo kwenye ile kamati ya kwenda
kuonana na Rais, tunawaombeni mkaitumie nafasi hii vizuri, dhamira
ikiwa ni kupata katiba bora na wala siyo kutafuta mshindi kati ya
CHADEMA na Rais au CHADEMA na CCM.
Tunawaombeeni wote, ili muongozwe na hekima katika mjadala wenu
maana inawezekana kabisa kupata katiba nzuri kwa amani na maelewano.
HONGERA RAIS, HONGERA CHADEMA KWA KUFUATA NJIA YA MAZUNGUMZO.
Taifa letu na watu wake ni muhimu kuliko mtu yeyote, kuliko chama
chochote.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)