Rais
wa Zanzibar na Mwenyekitim wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed
Shein,akipokea zawadi kutoka kwa kiongozi wa Madaktari kutoka China
Naibu Mkuu Idara ya Afya katika jimbo la Jiangsu,Zhou Zhengxing,ikulu
mjini Zanzibar,jana ujumbe huo umekuja katika kuimarisha sekta ya Afya.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekitim wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed
Shein,akizungumza na ujumbe wa madaktari kutoka jimbo la jiangsu,nchini
China ukiongozwa na Naibu Mkuu Idara ya Afya katika jimbo hilo,Zhou
Zhengxing,(wa pili kushoto),pia Balozi mdogo wa China anyeishi
Zanzibar,Chen Qiman,aliongoza ujumbe huo,Ikulu Mjini Zanzibar. Picha Na Ramadhan Othman
NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
UJUMBE kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China umeeleza azma yake ya
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya afya
ikiwa ni pamoja na kuanzisha upasuaji kwa njia za kisasa na mradi wa
tabasamu kwa kuwafanyia upasuaji watoto wanaozaliwa na athari za
midomo.
Ujumbe huo ulieleza hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati ulipokuwa na
mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein. Katika mazungumzo, ujumbe huo kutoka
Jimbo la Jiangsu nchini China ukiongozwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Afya
wa Jimbo hilo Bwana Zhou Zhengxing ulieleza kuwa lengo kuu la ujio
wao ni kuendeleza uhusiano na Zanzibar katika sekta ya afya.
Ujumbe huo ambao pia, uliambatana na Balozi Mdogo wa China anayefanyia
kazi zake hapa Zanzibar Bibi Chen Qiman ulieleza kuwa Jimbo la Jiangsu
lina mambo mengi ya kujivunia katika mashirikiano na uhusiano na
Zanzibar. Akitoa maelezo kwa Rais pamoja na mafanikio yaliopatikana
katika Jimbo hilo la Jiangsu kiongozi wa ujumbe huo bwana Zhengxing
alisema kwa mashirikiano ya pamoja Jiangsu ina mpango huo wa kuanzisha
upasuaji wa kutumia njia za kisasa pamoja na mradi huo wa tabasamu
unaohusu upasuaji kwa watoto wanaozaliwa na athari za midomo.
Alieleza kuwa ni imani yake kuwa kutokana na azma hiyo itazidi kupanua
zaidi ushirikiano wa kitaalamu pamoja na kuimarisha ushirikiano katika
kubadilishana utaalamu kwa ajili ya kukuza afya ya jamii.
Kiongozi huyo wa ujumbe huo alieleza kuwa Jiangsu na Zanzibar zina
uhusiano katika uimarishaji wa sekta ya afya kwa takriban miaka 47 hivi
sasa. Alisema kuwa mashirikiano katika sekta hiyo hayakuimarisha
huduma katika sekta ya afya pekee bali yameweza kuimarisha urafiki
mkubwa uliopo baina ya pande mbili hizo. Bwana Zhengxing aliwasifu
watu wa Zanzibar kwa ukarimu wao wanaowafanyia madaktari kutoka China
ambao hufanya kazi zao Zanzibar. ‘Ijapokuwa ni mara yangu ya kwanza
kuja Zanzibar nimeweza kujionea mwenyewe urafiki mkubwa uliopo kati ya
watu wa Zanzibar na China pamoja na Madaktari kutoka China”,alisema
Bwana Zhengxing. Nae Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake hapa
Zanzibar Bibi Chen Qiman alieleza kuwa China inampango wa kujenga
hospitali mpya ya kisasa huko Mkoani Pemba ambayo itakuwa hospitali ya
Rufaa kwa Pemba.
Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa China ina mpango wa kujenga ICU mpya
katika hospitali kuu ya MnaziMmoja mjini Unguja. Aidha, Balozi huyo
alisisitiza kuwa taratibu zote za ujenzi wa miradi hiyo zinatarajiwa
kuanza mapema mwakani. Pamoja na hayo, Balozi huyo alitoa shukurani
kwa Rais Dk. Shein na serikali anayoiongoza pamoja na wananchi wa
Zanzibar kwa kuendeleza mashirikiano makubwa na China pamoja na watu
wake hatua ambayo imepelekea kuimarika uhusiano na udugu.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali
Mohamed Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa ujumbe huo kutoka
Jimbo la Jiangsu kwa kuja Zanzibar ukiwa na lengo la kuzidisha uhusiano
katika uimarishaji wa sekta ya afya. Alisema kuwa tokea aingie
madarani ni mara ya tatu ujumbe kutoka nchini China unaohusiana na
sekta ya afya kufika afisini kwake hali ambayo inaonesha dhahiri kuwa
kumekuwa na uhusiano mwena na wakihistoria kati ya Zanzibar na China.
Dk. Shein alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana katika Jimbo la
Jiangsu sanjari na hatua za kuimarisha uhusiano kati yake na Zanzibar
tokea mara tu baada ya uhuru wa Zanzibar mwaka 1964. Katika maelezo
yake Dk. Shein alieleza kuwa madaktari kutoka Jiansu wamekuwa wakifanya
kazi kwa mashirikaino makubwa hapa Zanzibar na kutoa huduma bora kwa
wananchi hasa huduma za upasuaji. Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati mbali mbali ya uimarishaji wa
sekta ya afya tokea uongozi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu mzee
Abeid Amani Karume ambapo pia, iliwahi kuwa ya kwanza katika kuandaa
baadhi ya mipango ya huduma ya afya kwa bara la Afrika. Sambamba na
hayo Dk. Shein aliueleza ujumbe huo azma ya serikali kuimarisha huduma
za afya kwa kuzikarabati hospitali zake za Mkoa na Wilaya pamoja na
kuzipatia vifaa vya kisasa sanjari na kuanzisha kitengo cha kutoa
huduma za utibabu wa maradhi ya saratani, maradhi ya figo na maradhi ya
moyo.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)