KUFUATIA
msiba mkubwa uliotokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander
katika bahari ya Hindi usiku wa kuamkia Jumamosi, Septemba 10, 2011,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete, ameamuru maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu kuanzia
leo tarehe 11 Septemba, 2011 ambapo bendera nchini zitapepea nusu
mlingoti.
Aidha, kufuatia msiba huo,
Mheshimiwa Rais, ameahirisha ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu
nchini Canada ambako alikuwa amealikwa na Gavana Mkuu wa nchi hiyo,
Mheshimiwa David Johnston.
Katika ziara hiyo iliyokuwa
ifanyike kuanzia tarehe 14 – 16 Septemba, 2011, Mheshimiwa Rais
angekutana pia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa Stephen Harper.
Mheshimiwa Rais ameiomba Serikali ya Canada kupanga ziara hiyo kwa
tarehe za baadaye.
Rais alitembelea majeruhi
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, kuwajulia hali, baada ya
ajali hiyo. Akiwa katika ziara hiyo ya majonzi aliarifiwa kuwa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa imechukua maamuzi kadhaa kukabiliana na
hali ya ukoaji wa watu katika ajali hiyo.
Miongoni mwa hatua hizo ni
pamoja na kuchangia kiasi cha sh. milioni 300 ili kusaidia zoezi hilo
ikiwa ni pamoja na kusaidia kusafirisha na kuzika miili ya watu
waliopoteza maisha katika ajali hiyo. SMZ imetoa sh milioni 100 kwa
shughuli hiyo.
Serikali ya Muungano pia
imeamua kukubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili
ya kusaidia kufanya tathmini ya jinsi meli ilivyozama na kuokoa maisha
ya watu ambao watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Aidha leo, Septemba 11, 2011,
Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama itafanya kikao chake mjini Zanzibar
kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya kupata maelezo kamili
kuhusu ajali hiyo, kupokea ripoti ya ajali, kufanya tathmini ya ripoti
hiyo na kutoa maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali ya sasa na hali
ya baadaye ya usafiri wa maji nchini.
Hata hivyo kabla ya kikao
hicho, tayari Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina
kubaini chanzo cha ajili hiyo.Habari Na Father Kidevu
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)