Katibu Mtendaji wa Bodi ya
Magavana wa Afrika (ACBF) Dkt .Frannie Leautier(katikati) akiongea na
waandishi wa habari leo mjini Arusha kuhusu kuanza kwa Mkutano wa 20
wa Bodi ya Magavana wa Afrika(ACBF) unaotarajiwa kufunguliwa na Rais
wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete siku ya Alhamis (8.9.2011). Kulia ni
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano(ACBF) Audrey Mpunzwana na kushoto ni
Mtaalamu kutoka ACBF George Kararach.Picha na Tiganya Vincent-MAELEZO-Arusha
---
Tanzania
inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF
unaokwenda sanjari na mkutano wa tano wa viongozi waandamizi
utakaojadili jinsi ya kujenga uwezo kwa nchi wanachama zitakazoshiriki.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 07- 09 Septemba, 2011 katika
Hoteli ya Mount Meru mjini Arusha.
Mkutano wa Magavana wa ACBF utafunguliwa na Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzana Dkt Jakaya Mrisho Kikwete siku ya
Alhamisi tarehe 8 Septemba 2011 mjini Arusha.
Mkutano
utawashirikisha Mawaziri, washirika wa maendeleo na wadau wengine
maarufu watakaojadili jinsi ya usimamizi mzuri wa misaada na mikopo
barani Afrika na namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto za ajira
kwa vijana.
Mkutano wa Tano wa viongozi waandamizi utatangulia
mkutano wa 20 wa Bodi ya Magavana wa ACBF ambao utaongozwa na Waziri
wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mustafa
Haidi Mkulo.
Washiriki wa Mkutano wa Bodi ya Magavana wa ACBF ni
Mawaziri wa Fedha, wahisani kutoka nchi wanachama wa Bodi ya
Magavana(ACBF), viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia(WB), Benki
ya Maendeleo ya Afrika(ADB) pamoja na Programu za Maendeleo
zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano wa tano wa viongozi waandamizi, wasemaji
wakuu wanatarajiwa kuwa Katibu Mtendaji wa ACBF Dkt. Frannie Leautier,
Waziri wa maendeleo ya Uchumi, Mipango na Uchambuzi wa Sera Mh.
Marcel De Souza kutoka Benin na Waziri Mkuu Mstaafu wa Mauritania Mh.
Zeine Ould Zeidane ambao wataongoza mjadala juu ya changamoto za
ajira kwa vijana barani Afrika na hatua gani zichukuliwe ili
kukabiliana na changamoto hizo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo Afrika (Africa
Development Institute) Bw. Victor Murinde kwa kushirikiana na
Mkurugenzi wa Sera za Uchumi (SEP) Bi. Sue Szabo, Mshauri wa Utawala
bora wa Benki ya Dunia Bw. Deryck Brown pamoja na Bw. George Kararach
ambaye ni mtaalamu wa ACBF; wataongoza majadiliano kuhusu taarifa ya
viashiria vya uwezo wa Afrika kuelekea mkutano wa Busan, Korea ya
Kusini mwezi Novemba, 2011utakaojadili uratibu, usimamizi na ufanisi
wa misaada.
Mojawapo ya mada itakayojadiliwa katika mkutano wa
viongozi waandamizi hao ni pamoja na hoja ya kujenga uwezo kwa nchi
za Bara la Afrika.
ACBF ni mdau muhimu katika kuimarisha ushirikiano na
bara la Afrika ikiwemo Umoja wa Afrika(AU) pamoja na Shirika la
Maendeleo la Afrika(NEPAD).
Madhumuni ya ACBF na washirika wa maendeleo, ni
kuimarisha nafasi ya Afrika na kuonyesha umuhimu wa kutambua sauti ya
Nchi zinazoendelea katika kujenga uwezo.
Vilevile,
katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ACBF imejiunga na masharika
kama vile Taasisi ya Uchumi na Maendeleo ya Jumuiya ya Ulaya (OECD),
Mtandao wa Mafunzo ya Kujenga Uwezo (LenCD), Wanaharakati wa Masuala ya
Siasa wa Nchi za Kusini, Ushirika wa CD (CD Alliance) ambao hufanya
kazi kwa pamoja kwa kuainisha vipaumbe na mada kuhusu kujenga uwezo kwa
Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha, Katibu
Mkuu wa ACBF Dkt Frannie Leautier alisema kuwa lengo la mkutano huo ni
kujadiliana na kubadilishana taarifa, maarifa, utalaam na uzoefu
kuhusu namna ya uratibu na usimamizi mzuri wa misaada. Alisema kuwa
mkutano huo utasaidia kuboresha ubunifu na utekelezaji wa sera
zitakazosaidia kupata matokeo endelevu.
Dkt. Leautier alisema kuwa hatua ya kuwaleta pamoja
wataalam mbalimbali wanaohusika na uratibu na usimamizi wa misaada ya
wahisani itawasaidia washiriki kujifunza mambo mbalimbali na kupanua
uelewa wa wadau katika eneo hilo kwa lengo la kutaka kuimarisha uwezo
wa Afrika na pia kutoa fedha pale panapohitajika.Aliongeza kuwa mifumo ya utendaji wa wahisani
inapaswa kuendana na kanuni ya uendelezaji na kujenga uwezo.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)