Bloga Mwandamizi Nchini Muhidini
Issa Michuzi
Ankal akipongezwa
na Ndesanjo Macha mara baada ya kufungua Michuzi Blog katika ukumbi wa
Finlandia hall jijini Helsinki, Sweden, Septemba 8, 2005.
--
*Kwa Niaba ya Wadau Wote Wa LUKAZA BLOG tunapenda kumpongeza Bloga Mwandamizi Nchini Issa Michuzi kwa kutimizi Miaka 6 ya Libeneke,Daima tupo pamoja Hapo chini ni Ujumbe wa Shukrani kutoka kwa Issa Michuzi Kwa Wadau Wake wote popote pale Walipo
*Kwa Niaba ya Wadau Wote Wa LUKAZA BLOG tunapenda kumpongeza Bloga Mwandamizi Nchini Issa Michuzi kwa kutimizi Miaka 6 ya Libeneke,Daima tupo pamoja Hapo chini ni Ujumbe wa Shukrani kutoka kwa Issa Michuzi Kwa Wadau Wake wote popote pale Walipo
Vitu
vitatu navikumbuka siku Michuzi Blog ilipozaliwa. Kwanza ni kaka Ndesanjo
Macha, aliyenilekeza na kunipa tips muhimu zote za kublog,
aliponishangaza pale nilipomuuliza yeye anawakilisha chombo kipi katika
mkutano huu wa Helsinki Conference? Aliposema yeye anajiwakilisha
mwenyewe kupitia blog yake ya Jikomboe, ghafla nikawa macho kumchuzi kwa
kutomuelewa. Haikuniiingia akilini ni vipi mtu anayeendesha blog
aalikwe kwenye mkutano mkubwa kama huo.
Pili ni pale kaka Ndesanjo Macha
aliponitahadharisha kwamba ukianza kublog ni sawa na kujiambukiza
ugonjwa usiotibika. Yaani mtu unakuwa kama umeehuka na hufikilii jambo
linguine zaidi ya kublog. Macho kumchuzi yakaja tena. Ilikuwa ngumu
kumuamini kwamba haka ‘kaugonjwa ka kublog’ kakikuingia mwilini
hakatoki. Sasa naamini maneno yake maana haipiti dakika bila kuwaza
niwatumikie vipi wadau.
Tatu ni pale kaka Ndensanjo Macha
aliponitahadharisha kuhusu comment moderation. Yaani hii ya kupitia
maoni yote yanayotumwa na kuchuja yanayofaa kusomeka na yasiyofaa, kwa
mujibu wa sera za blogu yako. Macho kumchuzi yakaja tena. Safari hii ni
kwa sababu wakati huo sikuwahi kuwaza kwamba kuna wadau ambao kazi yao
ni kutukana, kujeruhi hisia za watu na kuchafua hali ya hewa. Hakika
sikuwa nimemuelewa hadi baada ya kuanza kupitia maoni takriban 3000 kwa
siku. Nashukuru kwamba kazi hiyo, yenye lawama tele kutokana na baadhi
ya wadau wachache kutaka kutema cheche zao kupitia Globu ya Jamii
kujikuta wakikwama, wakisahau kwamba sera ya Globu ya Jamii
iliyotanabaishwa kila unapotaka kutuma maoni ya 'Angalia usijeruhi hisia
za mtu/watu' inabakia pale pale kwa nia njema hiyo hiyo, na si
vinginevyo.
Mtu mwingine
aliyenitia hamasa kuendeleza libeneka baada ya kuanzisha blog ni kaka
yangu, rafiki yangu na mpiganaji mwenzangu, Fidelis Tungaraza, aka Mti
Mkubwa, aka FIDE. Huyu bwana, ambaye anaishi Helsinki, finland, kwa
miaka kibao sasa, alikuwa daima akinicharuta mimi na waandishi wenzangu
kuwa hatuwatendei haki wadau wa ughaibuni, kwani habari na taswira za
nyumbani walikuwa wanazipata kiduchu mno kiasi kwamba ilikuwa sawa na
kusema hakuna.
Baada ya hapo, na kama wanavyosema wahenga
wetu, kila kitu ni historia. Niliporejea Tanzania nikaanza kufuata
maelekezo ya Fide, kwamba niachane na mikutano, makongamano, warsha na
mengineyo, bali niwaletee mambo ya jamii. Na ni yeye Fide aliyenipa
majina ya Globu ya Jamii na wadau.
Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 2006, nikiwa
jijini New york, nikapata barua pepe toka kwa muasisi wa Globu ya Jamii,
kaka Ndesanjo Macha. Akanipa pongezi na pole kwa kuendelea kuteseka na
ugonjwa wa Ku-blogu. Pia akanikumubusha kwamba comment moderation
nisiache hata siku moja, kwani SERA ya blog inaimarisha blog husika kwa
kuzingatia hayo.
Mambo kadhaa yalijiri kuitambulisha Michuzi
Blog kwa jamii baada ya hapo. Na mambo hayo yote yaliibuka chini ya
kichwa cha habari cha BREKING NYUUUUZZZZZZ……ambapo kila mara hii
ilimaanisha kwamba habari na taswira hizi ni za kipekee, za sasa hivi na
hakuna ambaye anazo zaidi yangu mimi.
Nachelea kutaja BREKING NYUUUZZZ ZZ zote kwa
uhaba wa nafasi, lakini zile za kuuwawa kwa wapendwa wetu Marekani (Nkya
na Mazula), Kifo cha Mh Amina Chifupa na kujiuzuru kwa Waziri mkuu Mh
Lowassa pamoja na kutajwa kwa baraza jipya la mawaziri ni baadhi tu ya
habari moto ambazo Globu ya Jamii iliweza kuwa ya kwanza kutangazia
ulimwengu kabla ya mtu yeyote ama chombo kingine cha habari.
Yooote hayo tisa; kumi ni hii imani na uaminifu
ambayo Globu ya Jamii imejijengea kwa wadua katika miaka hii sita.
Yaani hakuna hata siku moja ambayo imetokea habari iliyokanushwa ama
kuripotiwa kwa makosa. Kwa hili nashukulu weledi wa timu yangu ambayo
daima naiasa kufuata hatua zote muhimu katika tasnia ya habari, hasa
kuuliza tena na tena na tena kabla ya kuchapisha habari. Na kuuliza huko
ni kwa sehemu zote tatu. Yaani sehemu ilipotokea tukio, kuuliza mhusika
na pia kuuliza upande rasmi ama wasemaji wakuu wa tukio husika.
Kama nilivyosema awali, mengine yote ni
historia. Itoshe tu kusema kwamba nitachukua muda mrefu kueleza kila
kitu na nisiweze kueleza robo ya mambo yote. Kwa maelezo hayo naomba
ruksa niishie hapa na kuwaomba wadau mbofye sehemu ya ‘KUMBUKUMBU’ na
kurejea katika posti za nyuma na kuapata hisoria kamili ya Michuzi Blog.
Kila kitu kipo hapo.
Mwisho naomba nisema kwamba Michuzi Blog aka
Globu ya Jamii ni mtumishi wa wadau wote duniani. Haichagui wala
haibagui, kwani atayetuzika hatumjui. Hivyo nawakaribisha wadau wote
tusherehekee siku hii huku nikiwaambia kwamba wakati wa kutimiza miaka
10 (InshaAllah) kutakuwa na MichuziTV na MichuziRadio Online, ambazo
ziko njiani hivi karibuni.
Natoa shukrani kwa mdau aliyetoa wazo la
kubadili jina ili Libeneke liwe la kimataifa, huku nikimhakikishia
kwamba kuwa kimataifa sio lazima lugha iwe tofauti na Kiswahili, kwani
tayari watu takriban milioni 400 wanazungumza lugha yetu ya Taifa ambao
ndio walengwa wakuu.
Ahsanteni sana wadau kwa sapoti yenu katika muda wote
huu na InshaAllah Mola akipenda na panapo majaaliwa MichuziTV na
MichuziRadio Online itaibuka hivi karibuni humu humu ndani ya Globu ya
Jamii kukuletea mambo kwa sauti na taswira zinazotembea. Tuombeane uzima
tu.
Ni vigumu kumshukuru kila mtu aliyechangia mafanikio madogo haya ya Globu ya Jamii. Ila kwa uchache niwashukuru washauri, wachangiaji, walezi pamoja na timu nzima ya Michuzi Blog kwa kufanikisha haya yote.
Nianzie kwa washauri wakuu ambao baadhi ni kama JK, kaka Jeff Msangi wa Bongo Celebrity, Profesa Mark Mwandosya na mama Lucy Mwandosya, Jacob Mwambegele, Freddy Macha, Da'Chemi Chemponda, Balozi Juma Mwapachu, Balozi Peter Kallaghe, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, Da' Maura Mwingira, kaka Charles Hilary, kaka Abubakar Liongo, kaka Abou Faraji, kaka Ayoub Mzee, Da' Flora Nducha, kaka Freddy Maro, Dr Emmanuel Nchimbi, kaka Hilary Bujiku, Mh Zitto Kabwe, Mh. January Makamba, Mh John Mnyika, kaka Max Melo, Dr Prosper Mosha, Dr Blandina Kilama, Bi Ainde Ndanshau, Da' Teddy Mapunda, kaka Baraka Msiilwa, kaka Frank Eyembe, Da' Sporah Njau, Da' Subi, Da' Jestina George, Da' Mishi Marshall, Kaka Imani Kajura, Da' June Warioba, kaka Assah Mwambene, kaka James Shang'a, Dr Ramadhani Dau, Dr Kashilila, Da' Suzan Mzee, Da'Mariam Mungula, kaka Beda Msimbe, Dr John Shoo, Sensei Rumaza na Sensei Malekia, kaka John Mashaka, Profesa John Mbele, Dr Hassan Mshinda, Da' Mindi Kasiga, Ras Makunja 'FFU', Da'Janeth Mtonyi, Mh Mohamed Dewji, kaka Azim Dewji, Da' Mwamvita Makamba, Da' Taggie Daisy Mwakawago, Kaka David Minja, kaka Ephraim Mafuru, kaka Wilna, Dr Faustine Ndugulile na wengineo kadhaa ambao ni wengi mno.
Pia niwashukuru wana Globu ya Jamii wakuu kina Christopher Makwaia 'MK',Francis Dande, Audax Mutiganzi, Woinde Shizza, Muhidin Amri, Othman na Ahmad Michuzi, John Nditi, Prosper Minja, David Owen, Dixon Busagaga, John Mashaka, Dr Hildebrad Shayo,Frank Kallaghe, Othman Mapara, Richard Mwaikenda, Fide Tungaraza, Maggid Mjengwa,Haki Ngowi, Gadna G Habash, Lady JD.
Nawashukuru sana sana sana kwa sapoti yenu. Mie sina cha kuwapa Ila Mola ndiye atayewazawadia kwa wema na ushirikiano wenu.
MICHUZI
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)