Warembo
wanaoshiriki shindano la Vodacom Miss Tanzania 2011 wakiwa katika
picha ya pamoja. Warembo hawa wamerejea jana katika jumba la Vodacom
baada ya kumaliza ziara yao ya siku kumi kutembelea mbuga za wanyama za
Mikumi, mji wa Monduli, Ngongoro, Tarangire, Arusha mjini kuhamasisha
utalii wa ndani nchini pamoja na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii
wakiwa katika ziara hiyo.
===================
Vodacom Miss Tanzania wamaliza ziara yao kanda ya Kaskazini
Na Mwandishi Wetu.
Washiriki
30 wa shindano la Vodacom Miss Tanzania waliokuwa kwenye ziara ndefu ya
kimafunzo mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Arusha wamemaliza ziara
hiyo na wamerejea ndani ya jumba lao 'Vodacom House'.
Ziara
hiyo ya mafunzo iliyochukua takribani siku kumi iliwafikisha
walimbwende hao kwenye Hifadhi za Taifa za Mikumi, Ngorongoro, Tarangire
na shule ya wasichana ya Maasai iliyopo wilayani Mbonduli.
Meneja
Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu
aliyataja maeneo mengine waliyotembelea kuwa ni shule ya watoto wa
kimaasai Monduli, Kaburi la hayati Moringe Sokoine, kiwanda cha Bia TBL
tawi la Arusha na mitambo ya simu ya Kampuni ya Vodacom ambao ndio
wadhamini wakuu wa shindano hilo.
Akiielezea
ziara hiyo ya mafunzo aliyoiita ya mafanikio, Nkurlu amesema warembo
hao wamepata fursa ya kujifunza mengi hususani kuhusiana na utalii wa
ndani.
“Tumemaliza
salama ziara hii ya mafunzo iliyowapa zaidi ufahamu walimbwende hawa
kuhusiana na historia na rasilimali zilizopo nchini. Washiriki
wamejionea maeneo mbalimbali ya kitalii ikiwemo Ngorongoro Crater ambapo
wanyama pori na binadamu wanaishi katika eneo moja,” alisema.
Nae
Mkurugenzi wa kampuni ya Lino Agency ambao ndio waandaaji wa shindano
hilo Hashim Lundenga alisema, baada ya kuwasili washiriki hao 30
walipata fursa ya kukutana na ndugu, jamaa na marafiki katika siku ya
familia iliyoandaliwa na Vodacom Tanzania ambao ndio wadhamini wakuu wa
shindano hilo.
“Baada
ya ziara ndefu Morogoro na kanda ya kaskazini, warembo wamekutana na
jamaa zao kwa mazungumzo kabla hatujaingia kwenye hatua ya mwisho ya
kumtafuta mshindi. Ni matarajio yetu wataitumia elimu waliyoipata katika
kuvitangaza vema vitutio vya utalii vilivyopo nchini huko waendako,”
alisema Lundenga.
Kwa upande wake mrembo Jennifer Kakolaki
alisema anajivunia kuwa mmoja wa washiriki wa Vodacom Miss Tanzania
2011 kwani hata baada ya kumalizika kwa shindano hilo anaweza kutumia
elimu waliyoipata kujitafutia ajira kupitia sekta hiyo ya utalii.
“Kiukweli
tumejifunza mengi kwenye ziara yetu, nawashukuru waandaaji na Kampuni
ya Vodacom kwa kuona umuhimu wa kutuandalia ziara hii ikiwemo kutupatia
muda wa kukutana na familia zetu. Kwa niaba ya wenzangu naahidi
hatutawaangusha na tutafanya tulichojifunza,” alisema Kakolaki
Mwaka
huu warembo hao wameingia kambini kwa mfumo tofauti na uliozoeleka
kwani wanaishi kwenye jumba maalum la Vodacom ambapo matukio yao
yatakuwa yakioneshwa kupitia Startv na Clouds TV na watazamaji watapata
fursa ya kupiga kura kuchagua mrembo watakayemuona anafaa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)