Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Utaratibu huo mpya utakaoanza katika mwaka
wa masomo wa 2011/12 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, ulitangazwa
Ijumaa iliyopita na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa.
Utaratibu huu mpya unaanzishwa kutokana na
mapendekezo yalitolewa na Tume ya Rais ya kuangalia na kutoa
mapendekezo ya namna ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharimiaji,
utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.
Kwa mujibu ya utaratibu huu mpya, fedha
zote za mikopo zitapelekwa vyuoni toka Bodi ya Mikopo ili vyuo viwalipe
wanafunzi baada ya kuwahakiki na kwamba maelekezo na utaratibu
utakaotumika, utaandaliwa na Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na vyuo vya
elimu ya juu na wadau wengine.
TAHLISO: HATUKUBALIANI
Akizungumzia utaratibu huu, Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nchini (TAHLISO) Mathias Kipara,
alisema hakubaliani na utaratibu huo kwa kuwa utaleta matatizo makubwa
kati ya wanafunzi na vyuo wanavyosoma.
“Utaratibu huu wa kupeleka fedha za
wanafunzi moja kwa moja vyuoni na kisha vyuo vifanye kazi ya kuwagawia
baada ya kuwahakiki haukubaliki, kwa sababu endapo huko nyuma kulikuwa
na ucheleweshaji wa kuziingiza fedha za wanafunzi kwenye akaunti zao,
hali iliyosababisha malalamiko na migomo toka kwa wanafunzi, je, sasa
hivi si ndiyo ucheleweshaji utakuwa mkubwa zaidi?” alihoji.
Kipara alisema kwamba kwa mfumo huu mpya
wanafunzi watachelewa zaidi kupata fedha zao, kwa kuwa kituo kipya
kilichoanzishwa katikati yaani vyuo, kitaongeza mlolongo kabla ya fedha
hizo kuwafikia walengwa ambao ni wanafunzi.
Alisema katika wakati huu wa sayansi na
tekinolojia, inashangaza kuona kwamba tume na serikali vinapendekeza
kuanzisha utaratibu wa kuwapanga wanafunzi katika mistari na kuwagawia
fedha mkononi, hali ambayo inaweza kuzalisha matatizo mengine.
Kipara ambaye pia ni Rais wa Serikali ya
Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), alisema kuwa hatua
hii inaweza kutengeneza tamaa kwa baadhi ya viongozi wa vyuo na vyuo
vyenyewe kuziacha fedha benki ili zizalishe faida kwanza na ndipo waje
kuzigawa kwa wanafunzi.
ARDHI WAPINGA
Kwa upande wake mwanafunzi wa mwaka wa
tatu wa Chuo Kikuu cha Ardhi anayechukua kozi ya Usanifu wa Majengo,
Ndeki Godluck, alisema kwamba suala hili limeamuriwa kisiasa zaidi na
halina tija kwa wanafunzi kwa kuwa linaonyesha wazi kwamba bodi
imezidiwa mzigo na hivyo inaurusha vyuoni ili wanafunzi wakamalizane na
vyuo vyao.
“Bodi ilipaswa kuongeza matawi katika
maeneo ya vyuo na hata huko mikoani ili kukabiliana na ongezeko kubwa la
wanafunzi na vyuo kwa kuwa kwa sasa ilikuwa imezidiwa,” alisema.
Alisema mfumo huu mpya ni kama umelenga
kupoteza nguvu ya wanafunzi ya kudai haki yao, pale kunapokuwa na tatizo
la mikopo kwa sababu kwa hivi sasa litakapotokea tatizo la kuchelewa
kuletwa kwa fedha, chuo kitawajibu wanafunzi kwamba Bodi imechelewa
kuleta fedha hizo na wanafunzi watakuwa hawana pa kwenda.
Naye Joseph Godfrey, mwanafunzi wa mwaka
wa pili wa kozi ya Usanifu Majengo katika Chuo hicho Kikuu cha Ardhi,
alisema kwamba jukumu la kutoa mikopo kwa wanafunzi ni la Bodi na ndiyo
inafahamika hivyo na kwamba kuvipa vyuo jukumu hilo ni kuwachanganya
wanafunzi wasielewe ni nani wa kumuuliza pale kunapokuwa na tatizo.
“Ni muhimu kwa vyuo vikaachwa kufanya kazi
zake za kutoa elimu kwa wanafunzi na si kuviongezea majukumu yasiyokuwa
ya kwake. Vyuo havina miundombinu, havina wataalamu wa masuala haya
sasa kama si kutaka kuanzisha machafuko ni nini?” aliuliza.
DUCE: UTARATIBU MPYA UTALETA MATATIZO
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu
cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Msafiri Kidunye, alisema utaratibu
mpya utaleta matatizo kati ya wanafunzi na vyuo.
“Huko nyuma wakati fedha zilipokuwa
zikichelewa tulikuwa tunafuatilia Bodi ya Mikopo. Sasa kwa utaratibu
huu, inabidi Waziri wa Mikopo afuatilie kwa Mkuu wa Taaluma ambaye ni
mwalimu wake, sasa hapo kutakuwa na shida.
Lakini cha kushangaza wanasema wameongea
na wadau na wakapendekeza hivyo, sasa hao wadau ni wapi, kama sio sisi
wanafunzi. Walikuja lini kwetu na tukapendekeza hivyo,” alihoji.
Alisema ni bora utaratibu wa zamani
ungeendelezwa na kuboreshwa ili fedha zinapopelekwa benki, ziingizwe
haraka katika akaunti za wanafunzi kwa ajili ya kulipwa.
Aidha, alisema kwa utaratibu huu kuna
gharama vile vile za kuweka miundombinu na waajiriwa wapya kwa ajili ya
kufanikisha kazi hilo.
MUCCOBS YAKOSOA
Serikali ya wanafunzi wa Chuo Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS) imepinga utaratibu mpya.
Rais wa MUCCoBS, Geofrey Washoto, alisema
utaratibu huo bado hautatatua tatizo kwani wanafunzi wa mwaka wa kwanza
wamekuwa wakipata fedha hizo kupitia kwenye vyuo na kumekuwa na usumbufu
mkubwa kwani kiini cha tatizo ni fedha kucheleweshwa kwa uzembe wa watu
wa chache.
“Sijaafiki utaratibu huu mpya kwani si
kiini cha tatizo, tatizo lipo kwenye Bodi ya Mikopo kuchelewesha fedha.
Pia najiuliza iwapo wanafunzi watagawiwa fedha hizo vyuoni itachukua
muda gani kuwapatia fedha hizo,” alisema.
Waziri wa Mikopo wa chuo hicho Kishiriki
cha Chuo Kikuu Sokoine cha Kilimo (Sua), Emmanuel Clemence, alisema
kufanya hivyo ni serikali kukimbia tatizo kwa kuzitwisha menejimenti za
vyuo mzigo huo.
“Serikali ina wajibu wa kuhakikisha
wanafunzi wanapata fedha stahili kwa wakati ili waweze kusoma kwa
utulivu badala ya kutumia muda mwingi kutafuta fedha, kuipa kazi hiyo
chuo si kutatua tatizo kwani kuna tatizo la uwajibikaji kwenye Bodi,”
alisema.
SMMUCO: TATIZO KUONGEZEKA
Rais wa serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu
Kishiriki cha Kumbukumbu ya Mtakatifu Stephano Moshi (SMMUCO), Godfrey
Mwengwa, alisema utaratibu huo utazidisha tatizo kwani kuna vyuo vina
wanafunzi wengi.
“Ni vyema jukumu hilo likabaki kwenye Bodi
husika huku ikitakiwa kuwajibika kikamilifu kwa kuhakikisha fedha hizo
zinawafikia wanafunzi kwa wakati. Kinachowafanya wanafunzi kugoma ni
fedha kuchelewa, sasa kwa utaratibu huu zitachelewa zaidi,” alisema Rais
huyo wa Chuo hicho Kishiriki cha Tumaini. Alisema pia usalama wa fedha
hizo nao utakuwa mdogo kwani chuo kinaweza kupewa zaidi ya Sh. milioni
90 na ikajulikana hivyo na siku ya kuzigawanya ikatokea la kutokea kwa
majambazi kuvamia na kupora na hivyo kuzua maswali iwapo chuo kitalipa
fedha hizo au serikali.
UFUNDI ARUSHA WAPONGEZA
Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Ufundi
cha Arusha imepongeza utaratibu mpya na kusema kuwa utawarahisishia
kufuatilia fedha zao vyuoni pindi zitakapokuwa zimechelewa. Hata hivyo, wameiomba serikali isichelewa kutuma fedha hizo kama Bodi ilivyokuwa ikifanya ili kuwaondolea usumbufu. Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo
hicho, Reuben Sebastian, alisema jana kuwa: “Itakuwa ni nzuri zaidi,
kwani zikipelekwa moja kwa moja vyuo itakuwa rahisi kufuatilia tofauti
kwani utaratibu wa mwanzo ulikuwa ni mrefu kufuatilia fedha wakati
zinapochelewa kutumwa. Kwa sasa mlolongo hautakuwa mkubwa.”
Lakini baadhi ya wanafunzi ambao hakupenda
kutaja majina yao licha ya kupongeza uamuzi huo walitoa angalizo kwa
wakuu wa vyuo kutowakata wanafunzi madeni yao kabla ya kuwapa. “Ni uamuzi sahihi, lakini tatizo
litakuwepo kwani vyuoni wakati mwingine kuna kutokuelewana kati ya
wanafunzi na walimu, fedha hizo zisikatwe na chuo kama mwanafunzi ana
deni,” alisema mwanafunzi mmoja chuoni hapo.
MHADHIRI SAUT APONGEZA
Hatua ya Serikali ya kupeleka mikopo ya
wanafunzi wa vyuo vikuu vyuoni moja kwa moja imeungwa mkono na Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha St. Augustine cha jijini Mwanza, Protas Rubaba,
aliyesema kuwa ni jambo zuri na litapunguza usumbufu kwa wanafunzi. Rubaba alisema pamoja na Bodi ya Mikopo
kuwapa wanafunzi fedha za ada pamoja na vitabu, lakini wanafunzi wengi
walikuwa wanazitumia vibaya fedha hizo kwa matumizi tofauti, lakini sasa
wanaweza kulazimishwa kuzitumia kwa kununulia vitabu na vifaa vingine
vya kufundishia.Naye mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Mass
Communication wa St. Augustine (SAUT), Erick Shampume, alisema ni wazo
zuri, lakini liandaliwe kwa umakini mkubwa kwani baadhi ya vyuo wanaweza
kuzitumia vibaya fedha hizo na kuwaletea usumbufu wanafunzi.
Shampume alisema hatua hiyo itawapunguzia
wanafunzi usumbufu wa kufuata mikopo jijini Dar es Salaam na badala yake
watakuwa wakizipata fedha hizo huko vyuoni kwao. Hata hivyo, mwanafunzi huyo alitoa
angalizo kuwa menejimenti za vyuo kuwa inabidi ziwe na kitengo maalum na
sio fedha hizo zishughulikiwe na mkuu wa chuo au msaidizi, kwani wana
kazi nyingi na huenda wakaleta urasimu mkubwa.
UDOM: MIGOMO ITAONGEZEKA
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Dodoma (Udom) walisema utaratibu mpya utasababisha vyuo vingi kuwa na
migomo ya kila mara. Mmoja wa wanafunzi hao, Jumanne Hasan, alisema
kuingiza pesa za wanafunzi katika akaunti za vyuo ni kosa kubwa ambalo
litawaghalimu wanafunzi wengi kukosa masomo yao kwa shindwa kupata
mahitaji yao kwa wakati mwafaka. Aliongeza kuwa serikali haina budi
kujadili kwanza suala hilo kabla ya kulitekeleza kwani linaweza kuleta
malalamiko mengi kwa wanavyuo kuliko ilivyo sasa.
“Hivi sasa pesa zinaingia moja kwa moja
katika akaunti zetu, lakini bado kuna utata je, itakuwaje zikianza
kuingizwa katika akaunti za vyuo?” alihoji. Aliongeza kuwa serikali haina budi kubaki
katika mfumo ule wa kwanza na kuufanyia marekebisho madogo madogo ambayo
yataboresha upatikanaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Dar; Salome Kitomari, Moshi; Cosmas Mlekani, Mwanza; John Ngunge, Arusha na Paul Mabeja, Dodoma.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)