Na Andrew Chale,
Blogger team, Tanzania
“KIPAJI
si umri ni
uwezo kwa kila mwanadamu aliyebarikiwa na kutumia kipawa alicho nacho.”
Hivyo ndivyo anavyoanza
kuzungumza Mtunzi wa mashairi Mohamed
Juma Shaaban (20) mkazi
wa mjini Zanzibar.
Mohamed ambaye ameshatoa kitabu cha “If
tomorrow Comes” alisema hayo katika mahojiano na
mwandishi wa makala hii. Anasema
kitabu cha mashairi cha “If tomorrow Comes,” alichokitoa
kwa mara ya kwanza mwaka 2010 jamii imekipokea.
Kupitia kitabu hicho anasema alipokea maoni
mbalimbali ya kumpa moyo ikiwemo ya kuandaa kitabu kipya, maoni ambayo
ameweza kutafanyia kazi kwa kutunga kingine cha “Hope Never Decays.” Mohamed anasema kitabu cha “Hope Never
Decays” chenye mashairi zaidi ya 65, kimejaa mafunzo mbalimbali ambayo
yamegusa jamii na taifa kwa ujumla.
Kitabu hiki
kinatarajiwa kuzinduliwa visiwani Zanzibar huku Agosti 20 na Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ramadhan Abdulla Shaaban ambaye
atakuwa ni mgeni rasmi. Akielezea
histori ya maisha yake, Mohamed anasema yeye ni mtoto wa nne kati ya
watoto watano wa familia ya Mzee Juma Shaaban, na kusema alizaliwa
Agosti 30, 1990 visiwani Zanzibar. Anasema tangu alipokuwa mtoto alikuwa na uwezo mkubwa wa kusoma
vitabu vya watoto.
Mohamed anasema
mwaka 1998 hadi 2002 alipata elimu yake ya awali kwenye Skuli ya Msingi
Mombasa na kisha kuamia kwenye Shule ya High View international
visiwani humo hiyo ilikuwa mwaka 2003, na kusoma darasa la sita hadi la
saba mwaka 2004. Alipokuwa
shuleni hapo alieweza kutumia muda wake mwingi kujihusisha na usomaji
wa vitabu na alipoaingia elimu ya sekondari mwaka 2005 alitumia masomo
yake vema.
Mohamed anasema
akiwa kidato cha nne, alipenda somo la Fasihi, ndipo alipopata msukumo
mkubwa wa kujituma kutunga mashahiri. “Masomo yote niliyapenda ila ili la Fasihi
kidato cha nne nililipenda zaidi kwani nilitumia muda wangu mwingi
kuhakikisha nasongambele ili kutimiza ndoto yangu ya kuwa mtunzi mahiri
Barani Afrika,” anasema Mohamed.
Anasema kwa kutumia elimu ailiyopita na uwezo
alionao, mwaka 2010 alifanikiwa kutoa kitabu cha mashairi kwa mara
ya kwanza kilichojulikana kwa jina la “If tomorrow
comes,” kilichokuwa na jumla ya mashahiri 40. Kitabu hicho anasema kipo kwenye lugha ya
Kiingereza, lakini kilipendwa na watu mbalimbali, hapo ndipo
alipopata msukumo wa kutoa kitabu cha “Hope Never Decays,”
anachokizindua Agosti 20.
Mohamed akikielezea kitabu hicho anasema
mashairi yake yamejaa kila aina ya mafunzo ambapo kimetoa taswira
mbalimbali kwa jamii juu ya kujiamini na kufanya jambo bila kukata
tamaa. “Maana halisi ni
juu ya mtu aliye na mabadiliko kwenye uchumi, kijamii na siasa na
ambaye atakuwa na matumaini, kwani matumaini hayaozi,”anasema.
Akielezea kwa nini amekuwa akitoa vitabu vyake
vya mashairi kwa Kiingereza na sio Kiswahili, Mohamed anasema kutumia
Kiingereza ni kutanua wigo wa kujuilikana kwenye anga za kimataifa kwani
ametoa fursa ya kupata radha tofauti kwa wasomaji ambapo wengi wa
watunzi nchini wamekuwa wakitunga mashairi kwa Kiswahili.
“Watunzi wengi wanatumia lugha ya Kiswahili
kwenye vitabu vyao hivyo nimeona ni bora nitumie Kiingereza ili
kuwafikia watu mbalimbali ikiwemo kuleta Soko la Afrika mashariki,
Afrika na duniani kote… hii itasaidia kuinua soko la
ndani na nje,” anasema Mohamed. Anasema amegundua wengi wa Watanzania wamekuwa wakinunua vitabu
vya mashahiri na hadithi kutoka nchi jirani vilivyo na lugha ya
Kiingereza zikiwemno nchi za Nigeria,Kenya na Ulaya.
Kwa kutumia Kiingereza anasema wasomaji
waliokuwa wanatafuta vitabu vya nje watapata fursa ya kusoma kwa sasa.
Kwenye kitabu cha “Hope
Never Decays,” anasema kuna mafunzo kwa jamii kuacha kuvunjika moyo kwa
matumaini yao mazuri kwani tumaini jema haliozi wala haliaribiki kamwe.
“Kuna shairi linasema kijana asikate tamaa
zaidi andelee mbele kwani mambo ya ulimwengu ni mengi anatakiwa kuachana
nayo bila kuyaweka rohoni hakika atafanikiwa, hii ni pamoja na aliye na
kipaji akiendeleze hakika atafanikiwa,” Mohamed ananukuu mistari ya
baadhi ya shairi hilo.
Katika
kitabu hicho kipya cha mashairi chenye mashairi 65, baadhi ya mashairi
hayo ni pamoja na “Time will tell,” “Tomorrow will come,” “Last coin,” “My
Africa,” “ Some tears,” “Yes I can,” “Beyond your verge,” “Better Dew
the no rain,” “Freedom song” na mengine mengi.
Akielezea kwa kifupi baadhi ya mashahiri hayo,
likiwemo shairi la “Last coin,” anasema ni juu ya mtu aliyebakiwa na
kiasi kiduchu cha fedha ambayo hawezi kuitumia kwa lolote ambayo
haitoshi kununua sumu au kununulia dawa ya kuweza kumsaidia kuishi. Mbali na na shairi hilo kuna shairi la
“Better Dew than no rain,” ambalo linaelezea kuridhika kupata kidogo
kuliko kusubiria kitu usicho na uhakika nacho.
“Shairi ili linaelezea ni jinsi gani mtu
anaweza kuamini kile kidogo alicho nacho kuliko kufikiria kikubwa…bora
matone ya asubuhi kuliko kutegemea mvua ambayo hujui kama itakuja
kunyesha,” anasema Mohamed. Mohamed ana ndoto ya kuwa mtunzi mahiri wa kimataifa wa mashairi
na kuhakikisha anasonga mbele kama walivyokuwa watunzi wakubwa wakiwemo
Shaaban Robert na watunzi mbalimbali wa mashahiri na riwaya
duniani.
“Namshukuru Mungu kwa kunijaria uwezo na hekima ambayo imeweza
kuniongoza siku zote mpaka kufanikisha kukamilisha kazi yangu ya utunzi
wa kitabu cha “Hope Never Decays,” kitachokuwa mwanga kwa
watakaokisoma,” Mohamed anasema.
Kwa wasomaji watakaohitaji kitabu hichi cha
‘Hope never decays’ wanaweza kuwasiliana na mtunzi wa kitabu hichi
Mohemed ‘MJ’ kupitia +255714460595, anapatikana Zanzibar, Tanzania, ama mwandishi na blogger wa Miss
JG, Tanzania, 0719076376 chalefamily@yahoo.com






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)