Mke
wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA Mama Salma Kikwete (kulia)
akimkabidhi vipeperushi vya Taasisi yake Mke wa Rais wa Burundi Mama
Denise Bucumi (kushoto) alipotembelea katika Ofisi za Taasisi hiyo hivi
karibuni
Na Anna Nkinda – Maelezo
Watoto
yatima wametakiwa kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya ufadhili wa
masomo na kuitumia nafasi hiyo kusoma kwa bidii kwani wako wengi kama
wao ambao wanahitaji kusoma lakini hawapati nafasi kama hiyo na hivyo
kuishi katika mazingira hatarishi.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais wa Burundi Dk. Denise Nkurunziza
Wakati akiongea na wanafunzi wa kike ambao ni yatima wa shule ya
Sekondari ya WAMA NAKAYAMA ambayo inamilikiwa na Tasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) iliyopo nyamisati wilayani Rufiki katika mkoa wa Pwani.
Dk.
Nkurunziza aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwatii walimu
wao kwani kwa kufanya hivyo watafanikiwa pia wasiipoteze nafasi
waliyoipata kwani wengine wanapoteza bahati pale wanapoitapa.
“Duniani
kuna watoto yatima wengi sana hata Burundi ni wengi mimi mwenyewe
nyumbani kwangu ninaishi na yatima 15 ambao si ndugu zangu na
ninawasomesha ndani na nje ya nchi hii inatokana na vita, Ukimwi, vifo
lakini mjue kuwa Mungu anawapenda sana watoto yatima kwani akiona
umeachwa na wazazi yeye anakuwa baba na mama yako pia yatima akilia
Mungu anamsikia haraka”, aliwafariji watoto hao.
Mke
huyo wa Rais wa Rwanda aliendelea kuwasisitiza watoto hao wasome huku
wakiangalia mbele zaidi kwa kufanya hivyo watafanikiwa kwani hakuna
anayejua kesho hata wao wanaweza kuwa viongozi wa ngazi ya juu Serikali
kwa kuwa namna utakavyojiandaa leo ndivyo unavyojiandalia maisha yako
ya baadaye.
Dk.
Nkurunziza alisema, “Mjue kuwa mama Salma amejitoa kwa jili yenu,
anawapenda na kuwaandalia maisha yenu ya baadaye ili yawe mazuri jambo
la muhimu mpendane na kuishi kama ndugu na kuwa mfano kwa jamii
inayowazunguka kwani ninyi nyote mnatoka katika mazingira yanayofanana”.
Alimalizia
kwa kuwataka watoto hao kuwa na moyo wa kuwasaidia wengine pale ambapo
watamaliza masomo yao na kupata kazi kwani wao pia wamesaidiwa wa watu
mbalimbali kwa kufanya hivyo watakuwa wameendeleza malengo ya mama
Kikwete ya kuwasaidia watoto yatima wanaoishi katika mazingira
hatarishi.
Akimkaribisha
Dk. Nkurunziza ili aongee na wanafunzi hao Mwenyekiti wa WAMA Mama
Salma Kikwete alisema kuwa dhamira ya kuanzishwa kwa shule hiyo ya
mfano ya sayansi kwa mtoto wa kike ni ndoto aliyokuwa nayo siku nyingi
ya kumkomboa mtoto yatima wa kike ili apate elimu sawa na watoto
wengine.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais alisema kuwa licha ya Taasisi ya WAMA
kujenga shule hiyo pia inafadhili wanafunzi wa shule za Sekondari
katika mikoani yote hapa nchini ambapo mwaka 2010 wanafunzi wa kwanza
walimaliza kidato cha nne ambapo wengi wao hivi sasa wako kidato cha
tano na wengine wamejiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.
“Ninawashauri
ndoto yenu ya kwanza baada ya kumaliza masomo muwe walimu wa sayansi
ingawa kila mtu ana ndoto zake katika maisha kwani kwa kufanya hivyo
mtakuwa mmelisaidia taifa kwa kuwaelimisha watoto wengi zaidi hapo
baadaye pia mkumbuke kuwa bila ya walimu hata nyinyi msingefika hapo
mlipo”, alisema Mama Kikwete.
Aliendelea
kusema kuwa Taasisi ya WAMA imefadhili shule ya sekondari ya Nyamisati
ambayo ina wanafunzi 250 kwa kujenga majengo na kutoa thamani nia ikiwa
ni kuhakikisha kuwa watoto wa kijiji hicho wanapata nafasi ya kujiunga
na elimu ya Sekondari.
Akisoma
risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake Asteria Ndalu alisema kuwa shule
hiyo ambayo imewafungulia milango ya maisha ilianzishwa mwezi wa pili
mwaka 2010 ambapo hadi sasa kuna wanafunzi 167 wa kidato cha kwanza na
cha pili kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.
“Sisi
ni watoto tunaotoka katika mazingira hatarishi lakini hivi sasa tuna
matumaini makubwa kwakuwa Mama Kikwete ameona matatizo yanayotukabili
na kuyatatua, kwani matatizo ni sehemu ya maisha ya binadamu kuna
wakati unaweza kufanikiwa na kuna wakati huwezi kufanikiwa jambo
linalotakiwa ni kupambana na matatizo hayo”,alisema Ndalu
Wanafunzi
hao waliahidi kushirikiana na walimu wao pamoja na jamii
inayowazunguka, kusoma kwa bidii na maarifa ili waweze kutimiza malengo
waliyojiwekea na hivyo kutoziangusha juhudi za Mama Kikwete za
kumkomboa mtoto yatima wa kike.






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)