LHRC YATAKA SERIKALI KUSITISHA UCHIMBAJI WA URANIUM WILAYANI NAMTUMBO. - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

LHRC YATAKA SERIKALI KUSITISHA UCHIMBAJI WA URANIUM WILAYANI NAMTUMBO.


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC kimetoa wito kwa Serikali kusitisha kwanza uchimbaji wa madini aina ya Uranium katika wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma hadi itakapothibitisha kuwa na uwezo wa kuzuia madhara yanayotokana na athari zake kiafya kwa binadamu na kimazingira.

Akisoma tamko la kituo hicho Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho ya Sheria Bw HAROLD SUNGURA amesema licha ya serikali kuanza mchakato wa kuchimba madini hayo ndani ya Mto Mkuju na maeneo mengine ya Bahi na Manyoni hadi sasa haijawashirikisha wananchi ikiwemo kuwaelimisha kuhusu athari zake.


Utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC katika migodi mbalimbali nchini ikiwemo Nzega, Geita na North Mara unaonesha kuwa uchimbaji wa madini umeleta maafa zaidi kwa Watanzania wengi kuliko faida.


Serikali imetakiwa kutazama kwa umakini uwekezaji wa mataifa makubwa hasa yaliyokuwa na mgogoro wa vita baridi katika sekta ya uchimbaji madini aina ya Uranium nchini zoezi linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.


Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho ya Sheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini LHRC Bw HAROLD SUNGURA amesema hatua hiyo italiepusha taifa kutotumiwa vibaya na mataifa hayo kama uwanja wa vita na mapatano kupitia madini hayo na mazingira yatokanayo na shughuli hiyo.


Madini ya Uranium yametajwa kusababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu kama vile saratani ya figo, ubongo, ini, damu, magonjwa ya moyo, kupunguza kinga mwilini, vifo vya watoto, kuharibika kwa mimba na kupunguza nguvu za kiume.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages