JESHI la polisi mkoa wa Shinyanga leo asubuhi limemkamata na kumhoji kwa muda
saa kadhaa kada wa Chadema, Fred Mpendazoe kufuatia tuhuma za kutishia kwa
bastola pamoja na kumfanyia shambulizi katibu wa UVCCM kata ya Maganzo,
Abdulkadiri Mohammed mwaka jana.
Kukamatwa kwa mpendazoe kumekuja siku tatu
akiwa katika ziara yake ya kwanza mkoani humo tokea alipokihama chama cha
Mapinduzi (CCM) na kuachia ubunge kwa kujiunga na chama cha CCJ na baadaye
kukimbilia Chadema.
Mpendazoe amekamatwa wakati akiwa katika ziara ya Kichama kuimarisha Chadema katika mkoa wa Shinyanga ambapo tokea majuzi amekuwa akifanya mikutano kadhaa ya hadhara katika maeneo ya Maganzo, Kishapu, Mhunze na Shinyanga mjini.
Kukamatwa kwake kunatokana na kosa ambalo alidaiwa kutenda Oktoba mwaka jana la kumtishia bastora na kumshambulia kwa maneno Katibu wa UVCCM, kesi ambayo Mpendazoe alidai kuwa ilikwisha siku nyingi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Diwani Athuman akielezea uamuzi wa jeshi lake alisema Mpendazoe alikamatwa kwa ajili ya kuhijiwa leo kwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili na kisha kuachiwa huru.
“Tulikuwa tukimtafuta toka mwaka jana mwezi Oktoba, lakini
kutokana na makazi yake kuwa jijini Dar tulitumia nafasi hii baada ya kuja
hapa Shinyanga kumtia mbaloni kwa suala lake, na baada ya kumuhoji
tulimwachia” Alisema Kamanda Athuman na kuongeza kuwa kesi hiyo ilitokana na
masuala ya siasa.
Kamanda huyo akifafanua zaidi alieleza kuwa katika
mahojiano yao na Mpendazoe alidai kesi hiyo imeshafutwa ambapo Kamanda wa
polisi alisema kuwa kwa sasa wapo katika jitihada za kumtafuta mlalamikaji
huyo ili aweze kuthibitisha kama kweli walifikia hatua ya kufuta kesi hiyo ili
waweze kulifikisha suala hilo kwenye ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
kwa ajili ya hatua zaidi.
“Siku za kariburi sisi polisi tulisikia
wameelewana, lakini habari hizo hazikuwa zimetufikia rasmi hapo ofisini ndio
tukaamua kumwita na yeye akasema ni kweli, lakini hatutaishia hapo ni lazima
pia tumwite mlalamikaji ili atuthibitishie ili tuweze kulifikisha kwa
mwanasheria kwa hatua zaidi, yeye atajua kama kuna kesi ya kujibu au la”
Alisema.
Hata hivyo akizungumzia kukamatwa kwake, Mpendazoe alielezea kusikitishwa na kitendo hicho cha Polisi kumkamata kwa kesi ambayo anatambua kuwa ilikwisha malizika kutokana na yeye na mlalamikaji kufikia makubaliano.
“Mimi pamoja na mlalamikaji tulikubaliana kumaliza jambo hili nje ya hamakama, na tukaandika makubaliano yetu na mkuu wa upelelezi wa mkoa (RCO) toka mwezi Machi mwaka huu, sasa nashanga leo ninakamatwa,” alifafanua Mpendazoe.
Na Frederick M. Katulanda
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)