Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ombeni Sefue akizungumza
wakati wa Mkutano wa Kilele wa Vijana uliofanyika Makao Makuu ya
Umoja wa Mataifa ukiwashirikisha vijana kutoka mataifa mbalimbali,
mawaziri wanaohusika na masuala ya Vijana na Taasisi za kijamii.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano huo, Balozi Sefue amesema
Utandawazi na matumizi ya vyombo vya habari vya kijamii( Social
Media)siyo tu kumewafanya vijana kuwa katika kijiji kimoja lakini pia
vijana wamekuwa na matumaini na mwamko mkubwa kisiasa, kijamii,
kiuchumi na kitamaduni na kwamba kasi waliyonayo vijana hivi sasa
inashindana na kasi ya serikali nyingi katika kuwatimizia mahitaji yao
zikiwamo ajira.
---
Na
Mwandishi Maalum-New York
Imeelezwa
kwamba baadhi ya nchi zitashindwa
kutekeleza kwa kasi matarajio na matumaini makubwa waliyonayo
vijana.Matarajio na matumaini hayo ni yale yanayoletwa na utandawazi
na matumizi mkubwa ya vyombo vya habari vya kijamii.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mwakilishi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi
Ombeni Sefue.Alikuwa akizungumza katika Mkutano wa kilele
wa Vijana uliofanyika Makao Makuu ya
Umoja wa Mataifa.Amesema utandawazi ambao
unaendeshwa na teknolojia unawafanya vijana kuwa
katika kijiji kimoja cha kimataifa. Na
kuwajengea ufahamu mkubwa wa wapi walipo au wapi wanatakiwa kwenda.
Balozi Sefue akaeleza ,
Utandawazi huo umewajengea vijana matumaini
makubwa ya kisiasa, kiuchumi , kiutamaduni na kijamii.“ Lakini, baadhi
ya matarajio hayo hayawezi kutekelezwa na serikali nyingi kupitia
raslimali zilizonazo au sera zilizopo na kwa kasi
wanayoitaka vijana”.
“ kwa maneno mengine, ingawa
Utandawazi unawapa matarajio kwa vijana wetu, lakini siku
zote utandawazi huohuo hautoi nyenzo sahihi za kuwapatia uwezo na
fursa vijana ya kutimiza ndoto zao”.akasisitiza Balozi
SefueAkatahadharisha kuwa kutotimizwa kwa
ndoto hizo za vijana, kunaweza kusababisha madhara makubwa. Madhara
ambayo yanaweza kuvuka mipaka ya nchi.
Kwa hiyo akasema, ni muhimu kuunga
mkono juhudi za serikali za kitaifa na kikanda, za kuujenga
uutandawazi wa haki utakao wawezesha vijana siyo tu kuwa na matumaini
bali pia kuwa na fursa ya kumiliki mali.
Kuhusu matumizi ya vyombo vya habari vya
kijamii ambayo vijana wengi wanajitanabaisha navyo, Balozi Sefue
amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, ingawa vyombo hivyo ni nyezo
muhimu katika kuleta mabadiliko chanya. Kwa bahati mbaya vyombo
hivyo kama havitatumia ipasavyho vinaweza pia kuleta matokeo mabaya.
Mwakilishi huyo wa Tanzania katika UM,
akabainisha kuwa serikali yake inaamini kwamba vijana siyo tu viongozi
wa kesho, kwani wanaweza kuwa viongozi wa leo na kutoa mchango mkubwa
wa kulijenga taifa lao kwa kushirikiana na wazee wao.
Akasema kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa
vijana katika ujenzi wa nchi yao, ndio maana serikali ya Tanzania imepitisha
sera zinazo wawezesha vijana wa kike na kiume kupata nafasi za
uongozi katika vyombo vya utoaji wa maamuzi likiwamo
Bunge.
Mkutano huo ambao ulifunguliwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,
uliwashirikisha mawaziri wanaohusika na masuala ya vijana kutoka nchi
wanachama wa UM. Pamoja na mambo mengine ulijadili changamoto
mbalimbali zinazowakabili vijana duniani kote na namna ya kuzitafutia
ufumbuzi.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na
mamia ya vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani. Pamoja na wawakilishi
kutoka taasisi zisizo za kiserikali. Na ulitoa na
maazimio mbalimbali yakiwamo ya kubuni mbinu mbadala za kushughulikia
matatizo ya vijana zikiwamo ajira.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)