Na Nova Kambota,
Rais wa awamu ya tatu Mzee Benjamin Mkapa aliwahi kusema kuwa maisha
bila vipaumbele ni ujinga mtupu, bilashaka hili halina ubishi kabisa
taifa lolote linaloishi bila vipaumbele hugeuka taifa la wahuni,
waporaji, mafisadi, wajinga,duni na zaidi huwa taifa legelege na
dhaifu.
Wageni mbalimbali kutoka Ulaya, Marekani ,Asia
na sehemu nyingine za ulimwengu waliowahi kufika nchini huwa
wanashangazwa sana na umasikini wa kutisha unaowaandama wananchi wa
taifa hili. Wageni wanatushangaa sana na wataendelea kushangaa kuanzia
Mlima Kilimanjaro,Mlima Meru, Udzungwa, Usambara, Ziwa Tanganyika, Victoria, Bahari ya Hindi mbuga nzuri za wanyama kama Mikumi na Ngorongoro lakini pia misitu ya kumwaga tu,mito mingi, mabonde ndiyo usiseme na ardhi yenye rutuba na
ya kutosha lakini bado miaka hamsini baada ya uhuru mamilioni ya watanzania bado ni masikini wa kutupwa.
Kwa mtiririko huu wa mantiki hapa ndiyo inaibuka hoja kuwa watanzania
hawafanani na nchi yao hata kidogo kwa maana ni watu mafukara
waliozungukwa na utajiri wa kutisha , hakika kuna utofauti mkubwa kati ya watanzania na utajiri wa taifa lao,
hata ukifika pale mbuga ya Ngorongoro wanyama wanacheza na kufurahi na
ndege wanarukaruka kwa furaha kubwa, nenda kandokando ya bahari ya
Hindi uone mawimbi yanavyopanda na kushuka kwa furaha kisha angalia
samaki walivyo na furaha kisha sasa rudi katika maisha ya walalahoi wa
nchi hii, kweli inahuzunisha kuona wanyama wana furaha kushinda watanzania, inauma sana!
Kuna kisa kimoja cha kuhuzunisha sana ambacho nadhani watoto wetu
wanapaswa kufundishwa madarasani. Inaelezwa kuwa mwaka jana 2010 wakati
wa uchaguzi mkuu mwangalizi mmoja wa kimataifa kutoka nje alitembelea
Tunduru akaona watu wanavyoogelea kwenye umasikini wa kutisha kisha
akatupa macho kwa mbali akaona misitu mizuri na mto Ruvuma kisha akahoji
kuwa inakuwaje watu hao ni masikini sana? Wananchi hawakuwa na la
kujibu baadaye mzungu huyo akasema kuwa “siamini kabisa na hainiingii
akilini kuwa CCM huwa inashinda kihalali kwa maana haiwezekani watu
masikini kama hawa waichague CCM”
Hivi nani atanishawishi kuwa CCM inashinda kihalali? Hapa uhalali unaozungumzwa sio wa kura tu bali
hata wa kuwaacha watu huru, kwa maana haiwezekani watu wanakuwa
masikini, wanafanywa wajinga na mifumo mibovu kiasi kwamba hawajui
umuhimu wa kura halafu wanajiandikisha watu milioni 19 kupiga kura
lakini siku ya kupiga kura wanajitokeza milioni 5 na CCM wanashinda!
Kisha uniambie hapo kuna ushindi? Ushindi gani? wakati milioni 14 nzima
hawajapiga kura? Idadi hii inaweza kubadili matokeo, kwa maana nyingine
yule mwangalizi wa kimataifa yupo sahihi kabisa kuwa watanzania
hawaichagui CCM badala yake inajichagua yenyewe na kujipa madaraka,
ajabu sana!
Watanzania wanalia kwa mengi, heri wote wangekuwa masikini lakini kuna
wenzao “wajanja wachache” wanaishi kama wafalme kwa jasho la
watanzania. Cha ajabu katika umasikini huu wa kutisha wa watanzania
kuna baadhi ya watanzania wachache wamejigeuza “miungu watu”
wamejimilikisha utajiri wote huu wakisaidiana na waporaji mabeberu
kutoka Ulaya na Marekani, hawa hawajui njaa ni nini? hawafahamu
masikini anafananaje? Wenyewe wanajua kuvaa suti na tai na mwisho wa
mwaka wanaenda kwenye maduka makubwa ya nguo huko London na Dubai ili kuwafanyia “shopping” wake zao na watoto wao wapendwa.
Nchi imekuwa ya matabaka kiasi kwamba mpaka taifa linayumba . Leo hii
imefika mahali kuna watu wana nguvu za kutisha kwenye nchi mpaka
mkurugenzi wa TAKUKURU anakiri kwenye mtandao wa Wikileaks kuwa Tanzania
kuna “untouchables” hawagusiki hawa. Katika mazingira haya bado CCM
inahubiri usawa, usawa gani? hata mtoto mdogo hawezi kushawishika kuwa
kuna hata chembe ya huo usawa kwenye nchi hii, labda kidogo CCM waje na
hoja ya kuwa na nchi mbili za kimatabaka kwenye taifa moja ndiyo! Kuna
Tanzania ya tabaka la juu na Tanzania ya tabaka la chini.
Huu ndiyo ukweli wa mambo , na matabaka haya mwanzo wake ni kuwa kuna
wale walioshikilia utajiri wa taifa na wale waliotengwa na utajiri huo.
Cha kusikitisha zaidi serikali inapigia chapuo mpasuko huu wa kitabaka
kiasi kwamba imejenga shule za kata maalumu kwa masikini ili wakafeli
na kuna mashule ya kimataifa yenye ubora haya ni maalumu kwa ajili ya
watoto wao na maswahiba zao. Serikali haijaishia hapo tu sasa hivi
Tanzania fedha iko juu ya sheria , nani asiyefahamu ukiwa na fedha nchi
hii unaweza kupindisha sheria? Zaidi ya yote kuonyesha kuwa serikali
yetu ni legelege ni jinsi inavyozitekeleza hospitali za serikali kiasi
kwamba ni kama majengo tu bila dawa na ili kuonyesha kweli ubaguzi ni
mfumo rasmi kwenye nchii hii hakuna “mkubwa” anaayekwenda kwenye
hospitali za serikali huko ni kwa kapuku na walalahoi, ubaguzi wa
kutisha!
Viongozi hawaishii hapo tu kwenye juhudi zao za kuwafukarisha wananchi na kuwaibia mali
zao, sasa wameanzisha soko huria la kura na wapiga kura na mnada kila
baada ya miaka mitano. Hivi kwanini viongozi wasiwaache huru
watanzania? Kwanini wasiwaache wakajichagulia watu wanaowaamini ni
viongozi bora? Huu kama sio ujambazi wa haki za masikini ni nini? yaani
hao walioko madarakani mwaka jana tu walipambana kununua kura kama sio
kwenye ngazi ya chama basi
kwenye uchaguzi kamili lakini ndiyo hivyo ukweli ni kuwa wamenunua
kura kwa pesa nyingi na sasa wapo madarakani wanashindana kupora mali
za wavuja jasho.
Taifa limekosa vipaumbele , limehalalisha rushwa, uporaji na ufisadi,
taifa linapepesuka kwa uhuni na tamaa za viongozi , dola imedhoofika
sana hata kamanda mkuu Rais Jakaya Kikwete analifahamu hili lakini
tatizo “kupe” wamejaa kuanzia huko CCM mpaka serikalini. Kile
alichokitabiri Mwalimu Nyerere sasa kinatokea kweli, Mwalimu aliwahi
kusema “serikali isiyojali wananchi wake haina uhalali hata kama
imepigiwa kura” sitaki kuamini kuwa serikali ya CCM haina uhalali ila
nashawishika kuwa haijali wala kuthamini wananchi wake hivyo kwa maana nyingine imeanza kupoteza uhalali wake.
Imefika sehemu sasa watanzania wanapaswa kufanana na utajiri wa nchi
yao, viongozi inabidi wafahamu kuwa watanzania hawana sababu ya kuwa
masikini kama walivyo sasa. Watanzania lazima wafanywe kujivunia
utanzania wao tofauti na hivi sasa ambapo kuna watanzania wanajilaani
kwa kuwa watanzania yote kwasababu ya ubabaishaji wa viongozi wao ambao
badala ya kuwatumikia wananchi wao wako “busy” kutumikia matumbo yao
na familia zao.
Lakini kama kawaida ya viongozi wetu wana tabia ya kuweka pamba
masikioni hawataki kusikia bilashaka hata hili watapuuzia lakini nawapa
angalizo kuwa watanzania wanafahamu kuwa hawakuumbwa walivyo bali
umasikini wao umetengenezwa hivyo ni swala la muda tu lakini siku
ikifika uvumilivu utakapowashinda basi watawang’oa wababaishaji wote
wanaojineemesha na mali zao tena kwa njia yoyote ile, hizi ni zama za
ukweli na uwazi ni wakati sahihi wa kuwa na mgawanyo sawa wa keki ya
taifa…..Allutacontinua!
Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Tanzania, East Africa
07/07/2011, Alhamisi






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)