Na Nova Kambota,
Naam! kwa hili
siwezi kukaa kimya, siwezi kukubali linipite kirahisi rahisi hivi ndivyo
navyoanza uchambuzi wangu huu wa leo ambao unalenga kujadili kwa undani
kuhusu hotuba ya Rostam Aziz aliyoitoa juzi tarehe 13 siku ya jumatano
mwezi huu mwaka 2011 huko Igunga wakati akitangaza rasmi
kujiuzulu Ubunge na ujumbe wa kamati kuu ndani ya CCM.
Nitamulika
kipengele kimoja baada ya kingine kwanza kwa lengo la kuwaelewesha
wasomaji wangu mtazamo wangu lakini pili ni kumtumia ujumbe Rostam na
wafuasi wake kuwa watanzania tupo macho tunafatilia siasa za nchi yetu
mwisho wa yote kwa vile hotuba ya Rostam ilikuwa imejengwa kwa misingi
ya hoja, mantiki na ufundi mkubwa wa fasihi nami nitatembea kwa mapigo
hayohayo ya hoja, mantiki na fasihi.
UTANGULIZI
Katika sehemu hii
ya hotuba ya Rostam anasema kuwa ameamua kuzungumza na “wazee wa Igunga”
, hapa kuna jambo linajificha, tena kuna utata mkubwa sana wa Rostam
kuamua kuzungumza na wazee, kuzungumza na wazee ni style aliyokuwa
anaitumia Mwalimu Nyerere wakati akizungumza mambo mazito na wazee wa
Dar es salaam, kwa maana nyingine mantiki ya Rostam kuzungumza na wazee
wa Igunga inalenga kutuhabarisha kuwa alikuwa akizungumza mambo mazito?
Sasa je kujiuzulu kwake ni jambo zito kwa nani? kwa wana Igunga? Wazee
wa Igunga? WanaCCM? Au watanzania? Kwanini liwe jambo gumu? Mbona hata
Nyerere na Kawawa waliwahi kutoka kustaafu uongozi CCM? je Rostam ni
nani ndani ya CCM? je upi uzito wa Rostam?
YATOKANAYO
Hapa Rostam
anaonyesha wazi yeye ni mtu wa namna gani? tena anasisitiza kwa maneno
haya “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa
jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya serikali ya Awamu
ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani mwaka
2005, tumekuwa tukiyapuuza na kuendelea kufanya kazi kwa bidii”, sasa
hapa Rostam anasema alikuwa anayapuuza matukio yale, hebu tujiulize
kwanini mtu anapuuza kitu? Mtu makini ni yupi anayepuuza au anayechukua
tahadhari? Je tukisema dharau na kupuuza kwake leo hii kumemlazimisha
kutema ubunge na ujumbe wa NEC tutakuwa tumemwonea? Labda niseme wazi
kuwa Rostam siyo kwamba alikuwa anapuuza bali kinachoonekana minyukano
ya kimakundi ilipamba moto na kujikuta wenzake wamemzidi kete kiasi
kwamba hata utetezi wake ungepuuzwa, kwani mara ngapi alijaribu
kujitetea? Au tupige kura tubaini watanzania wangapi wanamwona Rostam
msafi? Kupuuza haimaanishi ni msafi ila wakati mwingine yaweza kuwa ni
tuhuma za ukweli kiasi kwamba mtu anashindwa hata kujitetea.
KUJIVUA GAMBA
Hapa Rostam
anaonyesha jinsi gani anavyokwepa ukweli, anaacha kusema waziwazi kwa
mhusika anawageukia Nape na Chiligati, hivi Rostam anataka tuamini kuwa
wanachokifanya Nape na Chiligati hakina baraka za Kikwete? Hivi ndo
tuseme Nape na Chiligati ni waropokaji majukwaani? Hawajatumwa na
Kikwete? Tukiamini hivi tutakuwa kama tunakimbia ukweli ambao ni lazima
tutakutana nao mbele tu, kwa kifupi Rostam alikuwa anamsuta swahiba wake
Kikwete kwa mgongo wa Nape na Chiligati. Kwanza kabisa Rostam
anamaanisha kuwa Kikwete anang’ata na kupuliza kwa maana yeye hakusema
kwenye kamati kuwa “magamba” lazima waondoke ndani ya siku 90 lakini
wakati huohuo Rostam hajasema iwapo Kikwete aliwahi kuwaonya Nape na
Chiligati kuwa waache kujitungia maneno yao hivyo Rostam anamaanisha
kuwa Kikwete alikuwa nyuma ya Nape na Chiligati hivyo Rostam anaonesha
jinsi gani swahiba wake Kikwete amemwacha asombwe peke yake na mawimbi
ya minyukano na makundi ndani ya chama.
MAAMUZI YANGU
Hapa ndipo ambapo
Rostam kaniacha mdomo wazi na imani sio mimi peke yangu bali wengi
wameshangaa kauli zake zilizojaa ubinafsi. Rostam anasema kuwa hana
ameamua kuacha uongozi kwasababu siasa za kupakana matope zinamjeruhi
kibiashara, hivyo Rostam kaona bora biashara zake kuliko wananchi wa
Igunga halafu “eti nimesikia wanamlilia” ajabu sana , hapa kuna mambo
mawili matatu yaliyojificha, la kwanza ni kuwa Rostam kwake biashara
kwanza na kuwatumikia wananchi ni kiporo tu, pili tunarudi kulekule
wafanyabiashara wengi wanawania ubunge ili kulinda maslahi yao ya
kibiashara na si vinginevyo na tatu laana ya baba wa taifa inatuandama
aliwahi kutuonya kuwa makini na matajiri wanaojichomeka kwenye siasa
tuwahoji mara mbilimbili nia yao , sasa nadhani watanzania wameona kuwa
wafanyabiashara huwa wapo kimaslahi na wanapoona hawapati basi hawaoni
kazi kuchukua uamuzi wowote hata ikibidi kujiuzulu.
HITIMISHO
Naomba nihitimishe
kwa kutoa mapendekezo kadhaa;
Kwanza kabisa mpaka sasa Rostam hajaonyesha kupinga
shinikizo la Nape la kumtaka kung’atuka, hivyo amekubali kosa , siwezi
kujadili maneno yake kuwa hakubaliani na shinikizo kwasababu ikiwa
anapinga shinikizo la Nape na Chiligati basi hakupaswa kujiuzulu badala
yake alipaswa kwenda mahakamani kupinga kudhalilishwa au angewataka
wanaomtuhumu kumfikisha mahakamani.
Pili Rostam aache
kuwafanya watanzania watoto eti kwa kauli kuwa ataendelea kuwa
mwanachama mwaminifu wa CCM, nani kasema? Nasema labda Nape na Chiligati
waondoke vinginevyo ni swala la muda tu ila misuguano itaendelea tu.
Tatu natoa wito
kwa Kikwete ajivalishe nafasi ya Nyerere, je angekuwa Nyerere angefanya
nini? je angevumilia mazingaombwe “CHAPA KUJIUZULU” au angeongeza na
“CHAPA TAIFISHA MALI ZAO” , Naam nasema tena “vision 2015” itazidi
kuiyumbisha CCM , naona wapigane na mfumo mbovu ambao usiwe na mipaka
hata ikibidi serikali kung’oka naona ing’oke tu ili kunusuru nchi
vinginevyo kwa mbali naanza kuamini utabiri wa baba wa taifa aliposema
“CCM watakapoanza kugawanyika mjue itaanguka” na huu kama si mgawanyiko
ni nini basi? Tafakari!
Nova Kambota
Mwanaharakati,
Tanzania, East Africa
Ijumaa, 15 julai,
2011.






No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)