WAZIRI
wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja amesema uwekezaji unaoendelea
hivi sasa katika mikoa ya kusini ni kiashiria kizuri juu ya kukua kwa
uchumi wa mikoa hiyo na hasa katika bandari ya Mtwara.
Alikuwa
akitoa ufafanuzi leo mchana (Alhamisi, Julai 07, 2011) kuhusu uamuzi wa
kampuni ya Petrobas ya Brazili kuweka meli yake katika bandari ya
Mtwara wakati ikifanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi katika pwani ya
Mtwara hadi Mafia.
Akizungumza
mara baada ya kutembelea eneo la viwanda vya kujenga meli (ship
building area) na kuikagua meli ya uchimbaji mafuta iitwayo Poisedon
ambayo inajengwa katika bandari ya Geoje, iliyoko kusini mashariki mwa
Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini, waziri Ngeleja alisema uwekezaji huo
utatoa fursa nyingi zikiwemo ajira na biashara ya nchi za nje.
“Kitu
kikubwa tunachotaraji ni kuona ajira zikiongezeka kwa watu wa mikoa ya
Lindi na Mtwara… kutakuwa na ajira nchi kavu, majini na ajira kwa ajili
ya watoa huduma kwenye mahoteli na makazi ya hawa wawekezaji,” alisema.
Alisema
eneo jingine litakalonufaika na uwekezaji huo ni utalii na biashara ya
mahoteli ambalo alisema linaenda sambamba na ukuaji wa miji ya Lindi na
Mtwara na akatoa changamoto kwa viongozi wa mikoa kujipanga vizuri kwa
kusimamia suala la mipangomiji ili uwekezaji huu usiwapite kando.
“Ni
lazima wajipange vizuri kwa kutenga maeneo ya viwanda, maeneo ya
makazi, maeneo ya starehe ili miaka ijayo kusiwe na msongamano kana
kwamba hatukutarajia ukuaji huo. Ukuaji wa kasi wa miji ni dhahiri
mahali popote penye uwekezaji mkubwa,” alisisitiza.
Alisema
kukua kwa bandari ya Mtwara kutainuliwa pia na shughuli nyingine za
uzalishaji ambazo alizitaja kuwa ni uzalisaji wa umeme kutokana na gesi,
kujengwa kwa kiwanda cha mbolea, cha saruji, na uzalishaji wa bidhaa
zinazotokana na gesi (petrochemicals) ambazo alisema zinatumika zaidi
viwandani.
“Kuna
fursa ya uuzaji wa bidhaa nje ya nchi (exportation) kutokana na
uzalishaji wa gesi ya kupikia (Liquified Natural Gas – LNG), tukijipanga
vizuri mikoa ya kusini itabadilika na kuonekana tofauti,” alisema.
Alisema fursa nyingine ni uwepo wa barabara ya Mtwara-Mangaka-Tunduru- Namtumbo-Songea ambazo zimepata fedha katika awamu tofauti na kwamba kazi ya ujenzi iko katika hatua za awali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JULAI 07, 2011.





No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)