MABOSI WA VODAFONE FOUNDATION KUTEMBELEA MIRADI YA KIJAMII NCHINI TANZANIA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MABOSI WA VODAFONE FOUNDATION KUTEMBELEA MIRADI YA KIJAMII NCHINI TANZANIA

 Wajumbe wawili wa bodi ya udhamini wa mfuko wa huduma kwa jamii wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodafone ya nchini Uingereza wanawasili nchini kesho kwa ajili ya ziara binafsi na ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo ya jamii inayofadhiliwa na Vodacom.

Wajumbe hao Lord Michael Hastings na Elizabeth Filkin wanawasili jijini Dare s salaam leo na watakuwa na ziara ya kutembelea taasisi ya Community Based Rehabilitation In Tanzania – CCBRT, mradi wa kusaidia wanawake wajasiriamali - MWEI,kuzungukia maduka ya Vodacom M-PESA katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es salaam pamoja na kutembelea makao Makuu ya Vodacom Tanzania yaliyopo eneo la Mlimani City Jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa  kampuni ya Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba alisema wadhamini hao watakuwa nchini kwa siku kadhaa ambapo pia watahudhuria uzinduzi wa mradi mkubwa wa uhifadhi wa mbwa mwitu unaofadhiliwa na Vodacom Foundation.

“Hawa ni viongozi wanaotoka katika bodi yenye maamuzi ya juu kabisa ya mfuko wa huduma za Jamii wa Vodafone Group Foundation ambapo Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu wanakuja kuona maendeleo na mafanikio ambayo Vodacom Foundation ya Tanzania inachangia katika ustawi wa jamii nchini”Amesema Mwamvita.

Mwamvita amesema kuwa ujio huo unaweza kuwa wa neema kwa watanzania ambapo kupitia kwao Tanzania huenda ikanufaika zaidi na fedha zinazotengwa na Vodafone kusaidia harakati za maendeleo ya jamii hasa kutokana na mafanikio ambayo Vodacom Foundation imeyafikia.

Vodacom kupitria mfuko wake wa huduma kwa jamii imekuwa kampuni iliyo karibu zaidi na maisha ya watanzania na imekuwa ikichangia pamoja na kuunga mkono juhudi mbalimbali za wananchi zenye kulenga kuboresha maisha yao kwa kujiletea maedeleo na hiyo imekuwa ni sehemu ya fahari ya uwepo wa Vodacom Tanzania.
Amesema akiwa CCBRT mdhamini huyo bi Elizabeth atakutana na menejimenti ya Hospitali na kupata taarifa ya miradi ambayo Vodacom Foundation inaipatia fedha ukiwemo mradi wa kusaidia wanawake dhidi ya ugonjwa wa Fistula na Ujenzi wa hospitali maalum ya wanawake ya Baobab.

Vodacom Tanzania kupitia Vodacom Foundation imechangia zaidi ya shilingi mioni mia saba ili kugharamia matibabu ya wanawake wanaosumbuliwa na maradhi ya Fistula mradi ambao huduma ya M-PESA hutumika kuwatumia nauli wanawawake wagonjwa popote walipo kuja Dar es salaam kwa ajili ya matibabu ambayo nayo hutolewa bila malipo”Alisema Mwamvita.

Aidha Elizabeth atatembelea pia utekelezaji wa mradi wa Vodacom wa kusaidia wanawake wajasiriamali mikopo midogomidogo isiyo na riba uitwao MWEI katika wilaya ya Kisarawe. Mradi huu ambao upo katika majaribio unatekelezwa katika wilaya mbalimbali hapa nchini.

Kwa upande wa mradi wa Mbwa Mwitu Mwamvita amesema Mjumbe wa Mfuko wa jamii wa  Vodafone,Elizabeth atahudhuria uzinduzi wake uliopangwa kufanyika Julai 14, mwaka huu Wilayani Serengeti Mkoani Arusha uzinduzi utakaoongozwa na waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Ezekiel Maige.
“Huu ni mradi unaolenga kulinda mbwa mwitu dhidi ya hatari ya kutoweka inayowakabili kutokana na sababu mbalimbali licha ya kwamba viumbe hawa ni sehemu ya utajiri wa mali Asili na kukuza sekta ya Utalii hapa nchini na mpaka sasa Vodacom Foundation imeshatumia zaidi ya shilingi milioni mia mbili na hamsini katika mradi huu kwa masilahi ya Tanzania.”Alisema Mwamvita

Mfuko Mkuu wa kusaidia Jamii wa kundi la Makampuni ya Vodafone - Fodafone Group Foundation hutoa misaada mbali mbali kwa jamii za kitanzania kupitia Vodacom Foundation misaada ambayo hulenga maeneo ya elimu,afya na mazingira.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages