Na Nova Kambota,
Binafsi
nimeshtushwa sana na kauli za baadhi ya wana CCM kuwa chama chao
kimeshajivua gamba , wanatumia mabadiliko ya safu ya uongozi ndani ya
chama hiko yaliyofanyika hivi karibuni huko Dodoma, wakiwa na furaha
kubwa wanadai kuwa hatua ya sekretarieti ya chama chao kujiuzulu huku
ikimtupa nje katibu mkuu Yusuph Makamba na kumwingiza katibu mkuu mpya
Willison Mkama na pia hatua ya kamati kuu ya chama hiko kuvunjika kwa
maana nyingine imewatupa nje wajumbe mbalimbali lakini kati ya hao wapo
wanasiasa wawili waliotawala vichwa vya magazeti hawa ni Andrew Chenge
na Rostam Aziz lakini kujipa matumaini wanaccm wanadai kuwa kuingia kwa
sura mpya tena za vijana kama Nappe Nauye na January Makamba ni ushahidi
kuwa chama chao kimejivua gamba na sasa kipo safi .
Hata hivyo miezi michache
tu baada ya safu mpya ndani ya chama hiko kutangazwa dalili za wazi
kabisa zimeonekana kuwa CCM ilikuwa imeshiba sana kiasi kwamba ilikuwa
vigumu kwake kupenya kwenye tundu jembamba sana hivyo ilipaswa kujivua
gamba ili ipite lakini kwavile gamba la CCM limeshikamana na ngozi basi
kikao cha Dodoma kimehofia maumivu ya kuvua gamba na badala yake CCM
imejidanganya yenyewe kama sio kufanya mchezo wa kitoto wa kutapika
ikidhani kuwa kwa kupunguza ukubwa wa tumbo itaweza kupenya hapo lakini
sivyo inapaswa kujivua gamba! Lakini kwanini nasema CCM imetapika tu na
sio kujivua gamba kama wengi wadhaniavyo?
Kwanza
kabisa wanabiolojia au wataalamu wa elimu ya viumbe wanafahamu kuwa
nyoka hajivui gamba kwa lazima la hasha! Bali gamba lenyewe huelegea na
kujivua au hulegea sana na wakati nyoka akipita kwenye upenyo Fulani
basi gamba huvuka hata pasipo nyoka mwenyewe kufahamu huu ni ukweli wa
kisayansi kabisa lakini cha ajabu sana ni kile kinachoitwa kujivua gamba
kwa ccm ni kwa kujilazimisha ,hakika nyoka hawezi kujivua gamba kwa
kujilazimisha hivyo hata CCM haiwezi kujivua gamba kwa kujilazimisha
badala yake inaweza kutapika kwa kujilazimisha labda kwa kuingiza vidole
kwenye koromeo au kula kitu Fulani kitakachopelekea tumbo kuvurugika
kisha kutapika hivyo kwa mantiki hii ni dhahiri kabisa ilichofanya CCM
ni kutapika tu lakini sio kujivua gamba kama wanavyotaka kuuaminisha
umma wa watanzania.
Pili
ni jinsi CCM ilivyoshindwa kufanya mabadiliko ya kimchakato ndan ya
mioyo ya makada wake nasema hivi kwasababu naona kabisa kile kinachoitwa
migawanyiko au minyukano ndani ya CCM itaendelea kwa maana mpaka sasa
CCM haijafanikiwa kujipambanua kiitikadi na kiimani iwapo ipo pamoja na
wafanyabiashara ambao ni wafadhili wa chama hiko huku wengi wao
wakihusishwa na tuhuma za ufisadi au wapo pamoja na wakulima na
wafanyakazi ambao ndio wenye chama chao lakini sasa wameporwa kiasi
kwamba sasa wenye fedha ndio wenye nguvu na ndio wenye uwezo wa kugombea
na kushinda ndani ya chama hiko kiasi kwamba katibu mkuu wa zamani wa
chama hiko Philip Mangula aliwahi kutamka kuwa CCM itangaze tenda kwenye
kuwania uongozi! Hivyo ni wazi kuwa CCM haijaweza kuwaleta meza moja
Harrison Mwakyembe na Edward Lowassa, pia haijafaulu kuwakutanisha
kimtazamo Samwel Sitta na Rostam Aziz au kuwaimbisha wimbo mmoja Andrew
Chenge na Anne Kilango Malecela wala mabadiliko haya hayawezi
kuwasemesha lugha moja Yusuph Makamba na Shy-Rose Bhanji, CCM ingejivua
gamba haya yasingekuwepo lakini kwavile imejidanganya kwa kutapika tu
siiombei mabaya ila nasema isubiri ione nini kitafuata.
Tatu
CCM ingejia gamba kweli isingejitosa kwenye maji ya moto tena
yanayochemka nasema hivi kwasababu mpaka sasa dalili za wazi zinaonyesha
kuwa CCM haiamini kuwa ipo ndani ya mfumo wa vyama vingi chukulia mfano
wa hoja ya katiba mpya , naona kabisa ukimtoa Prince Bagenda nadhani
wanaccm wengine wote licha ya kutamka kuwa katiba ni hoja ya wananchi
ila mioyoni mwao wanaamini katiba ni hoja ya CHADEMA, CUF, NCCR na
baadhi ya wanaharakati tu kwasababu iwapo kweli CCM inaamini kuwa ipo
kwenye ushindani wa kisiasa kwenye mfumo wa vyama vingi basi kujijenga
kwake kungetegemea katika kuipenda na kuikuza demokrasia badala yake
inategemea nguvu zake , mimi naamini CCM ilipaswa kuwa ya kwanza
kuipinga rasimu ya marekebisho ya katiba kwa jinsi ilivyojaa mapungufu
badala yake inaunga mkono licha ya mapungufu hayo hii inatafsiri gani?
Je CCM inataka kuvikomoa vyama vya upinzani au uhafidhina unaisumbua
CCM? Je CCM ingejivua gamba ingeendeleza uhafidhina wa jinsi hii? au na
yenyewe ingepinga rasimu hiyo? Jibu rahisi ingejivua gamba isingekuwa na
uchafu wa aina hii ila kwavile imetapika tu ndio maana sasa ina njaa ya
kuwakomoa wapinzani lakini niwakumbushe kuwa katiba mpya ni hitaji la
watanzania sio CHADEMA wala CUF.
Nne
CCM walipaswa kufanya mapinduzi ya kimfumo sio watu kama ilivyofanya,
kwangu mimi nilitegemea CCM ingekuja na maazimio ya kukomesha mfumo wa
wafanyabiashara kukimbilia ndani ya chamma hiko na vilevile kukomesha
mfumo wa viongozi wa chama hiko kupendaz kusifia na kusifiwa tu , mimi
nilitegemea kuwa sasa CCM inaandaa mkakati rasmi wa kuwa na tabia ya
kujikosoa ili kulinda staha, tunu na falsafa ya mapinduzi ya chama hiko
lakini sijaliona hili amini nakwambia ndani ya CCM bado ukiwa msemakweli
kama Samwel Sitta,Harrison Mwakyembe na John Magufuli utajikuta
unaongeza maadui kuliko marafiki, mambo haya hayawezi kubadilishwa kwa
kumwondoa Makamba na kumweka Mkama bali kubadili mfumo wa CCM ndio maana
nasisitiza kuwa ilichofanya CCM imetapika tu haijajivua gamba kwa
kuhofia maumivu kwa maana gamba limeshikamana na ngozi.
Tano
nilitegemea CCM ijisafishe kwa dhati kabisa kwenye kila ngazi na
jumuiya zake tena kwa kuwapiga chini viongozi wale wanaoonekana ni mzigo
lakini siamini kama hili litafanyika , hapa sidhani kama UVCCM , UWT na
Jumuiya ya wazazi zitaguswa, labda nitumie wasaa huu kumpa siri Jakaya
Kikwete kuwa hayo anayoita makundi na minyukano ya vigogo wa chama hiko
kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 chanzo chake haswa ni huko kwenye jumuia
hizi na endapo hatazigusa wala kuzitikisa walau kidogo basi hicho
kinachoitwa kujivua gamba litakuwa ni jambo la kufikirika tu kuliko
uhalisia ndani ya chama chake hiko.
Mwishowe
nihitimishe makala haya kwa kuwaasa wanaaccm kuwa bado wana safari
ndefu ya kujivua gamba sio kirahisirahisi hivi kama wanavyodhani tena
hakuna ubishi kuwa kwa gamba lilliloshikamana na ngozi kazi kubwa
inahitajika kulivua, kwa upande wa vijana wa chama hiko wasishangilie
kuingia kwa vijana wenzao January Makamba na Nappe Nauye bali wanapaswa
wajikite zaidi katika mapambano ya ndani ya chama yatakayowawezesha
kukibadili chama hiko kutoka wazee oriented kuwa vijana oriented kisha
wapindue mfumo wa wafanyabiashara na wakirudishe chama mikononi mwa
wakulima na wafanyakazi vinginevyo hiko wanachoita kujivua gamba si
lolote bali ni kutapika tu na hivyo CCM yao haiwezi kupenya kwenye mioyo
miyembamba ya watanzania masikini kwa kujitapisha tu bali inapaswa
ijivue gamba hata kama itapata maumivu makali…Tafakari!
Nova Kambota,
Tanzania, East Africa
Jumamosi, 2 julai 2011
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)