Naibu Spika Wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai akiongea na waandishi wa habari.
Mbunge wa Bariadi Mashariki Mh.
John Cheyo akijibu maswali kwa waandishi wa habari.
Mbunge wa Viti Maalum ambae pia ni
Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala Mh. Angellah
Kairuki akijibu swali toka Kwa Baraka Baraka.
Mbunge wa Ilala Mh. Zungu akijibu
maswali.
Picha ya pamoja Baada ya Mkutano na
waandishi wa habari.
--
Wabunge wanne waliokuja Uingereza kuzungumzia
mgogoro wa pesa za kampuni inayouza vifaa vya ulinzi –BAE Systems
wamefafanua namna zitakavyotumiwa. Wakiongea katika Ubalozi wetu
Uingereza mjini London, Ijumaa mchana, viongozi hao walihimiza
wanachofanya ni kufuatilia matokeo ya mahakama ya sheria inayochunguza
rushwa (Serious Fraud Office-SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo
riba inaongezeka.
Wabunge walikutana
na House of Lords ambao ni maofisa na viongozi wa ngazi za juu sana
wenye usemi mzito katika masuala ya kisiasa Uingereza.
Mwezi Desemba mwaka
jana SFO iliiamuru kampuni ya BAE kulipa faini paundi laki tano na
kuipa serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni sawa na shilingi 75.3
bilioni za kitanzania kama pesa za kujisafisha uso. Toka tamko hilo
litokee miezi sita iliyopita imezuka migogoro kadhaa.
Upande mmoja BAE system
wanataka fedha zisipewe serikali ya Tanzania bali kwa mashirika ya
fadhila toka nchi za nje upande mwingine uongozi wa Tanzania unasisitiza
serikali inao mfumo imara utakaohakikisha fedha zitawafikia wahusika.
Mgogoro ulianza
mwaka 1999 wakati Tanzania ilipotaka kununua vifaa vya kusaidia ulinzi
wa viwanja vya ndege toka kampuni ya BAE. Ilidaiwa kuwa mfanya biashara
Shailesh Vithlani wa kampuni ya Merlin aliyefanya dili kati ya BAE na
Tanzania alipewa asilimia 30 ya pesa ya mauzo kama hongo. Pesa hizo
ziliwekwa katika akaunti yake ya benki Uswisi. Wahusika wengine ni
aliyekuwa Wakili wa Serikali, Andrew Chenge na Gavana wa benki kuu,
Idriss Rashid. Wote hawajashtakiwa na Vithlani anadaiwa kujificha
Uswisi, ilhali SFO imetoa tamko afikishwe mahakamani.
Akijibu swali
kuhusu kutokuelewana huku, mwenyekiti wa msafara Mbunge Job Ndugai
ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, alisema si vizuri BAE
kutuingilia au kutueleza nini cha kufanya na pesa hizo ambazo ni maslahi
yetu .
“Sisi tunafahamu
mfumo gani utakaohakikisha pesa hizo zinatumika sawasawa, zikienda kwa
mashirika ya ufadhili ni kama zimetolewa kwa watu wa nje.”
Mbunge mwingine,
John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na
Hesabu za Umma, aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi
toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika
na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika
kujenga elimu,” alisema Mbuge huyo wa Bariadi Mashariki.
Toka SFO ilipoamuru BAE
Systems ilipe faini kwa mahakama na fidia kwa Tanzania yametokea pia
madai kwamba wapo walioandikia BAE barua pepe kuwa wasiilipe serikali ya
Tanzania pesa hizo.
Wabunge
wanasisitiza pesa zitaendeleza elimu.
Mbunge Maalum,
Angellah Kairuki ambaye ni pia Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Haki na Utawala, alielezea kwamba ingawa pesa hizo zinaonekana nyingi
lakini hazitasuluhisha matatizo yote ya elimu nchini, mathalan, kuongeza
mishahara ya waalimu.
Alitoa mifano ya ukosefu wa madaftari, vyoo na vitabu vya
kusaidia waalimu kufundisha. Mifano hiyo inayolenga shule za msingi na
sekondari inatokana na matizo makubwa ya wanafunzi kujisaidia porini na
kukosa vifaa muhimu vya elimu.
Mbunge Mussa Zungu
wa Ilala, na vile vile Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika
na Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, alikumbusha kwamba tatizo
halikuanzwa na Watanzania. “Ni suala lililoamuliwa na mahakama ya
Uingereza; sisi tuchohitaji ni kuendeleza elimu.”
Habari imeandikiwa na Freddy
Macha akishirikiana Jestina George pamoja na
URBAN PULSE
CREATIVE.
MUNGU
IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)