WABUNGE WAOMBA SERIKALI IWASAMEHE WANAFUNZI WA UDOM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WABUNGE WAOMBA SERIKALI IWASAMEHE WANAFUNZI WA UDOM

Jengo La Chimwaga Lililopo Chuo Kikuu Cha Dodoma

WABUNGE wameiomba Serikali iwasamehe wanafunzi 400 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliosimamishwa masomo kwa muda usiojulikana, kwa sababu ya kufanya maandamano na mgomo kupinga kutopewa fedha za mafunzo kwa vitendo.

Jumatano wiki hii, wanafunzi 400 walipewa saa nne wawe wameondoka chuoni hapo eneo la Chimwaga, kutokana na kukithiri kwa vurugu zilizokuwa zinafanywa na wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula, uamuzi wa kufunga chuo hicho una lengo la kuepusha baadhi ya wanafunzi na majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na baadhi yao kukaidi amri ya kusimamisha mgomo wao ulioanza wiki hii.

Lakini juzi wakichangia hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa Mwaka 2010 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2011/12, wabunge walieleza kuwa Serikali inapaswa kuwasamehe wanafunzi hao na kuhakikisha inawarejesha chuoni, kwa kuwa baadhi yao hawahusiki.

Wabunge wa CCM, Murtaza Mangungu (Kilwa Kusini), Mtutura Mtutura (Tunduru Kaskazini), Amina Makilagi (Viti Maalumu) na wa Viti Maalumu Chadema, Christowaja Mtinda na Sabreena Sungura; ndio waliotoa rai kwa Serikali kuwasamehe wanafunzi hao wa Udom.

Hata hivyo, katika michango yao, Mtutura alisema wanafunzi hao wameponzwa na baadhi ya wanasiasa ambao wamewadanganya, na baada ya kusimamishwa chuo, wamezima simu zao na hawapatikani kutoa msaada wowote.

“Hawa wanafunzi waligoma kwa sababu ya ushawishi wa baadhi ya wanasiasa, lakini leo wamezima simu na sasa wanahangaika hawajui la kufanya. Nawaombea kwa Serikali ya CCM, iwarudishe chuoni na bila shaka watakuwa wamepata funzo,” alisema Mtutura.

Kwa upande wake, Sungura alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa hali ya wanafunzi hao baada ya kusimamishwa imekuwa ngumu, kwani baadhi yao na hasa wasichana, hawana pa kulala na sasa wako hatarini kuingia katika biashara ya kuuza miili yao.

“Kwa kweli hali ni mbaya Mheshimiwa Mwenyekiti kwa wanafunzi hawa … hawana mahali pa kuishi baada ya kufukuzwa chuoni, kwa sababu hawana nauli za kwenda kwao, na kwa wasichana hali ni mbaya zaidi kwa sababu wako katika hatari ya kuingia katika biashara ya kujiuza,” alisema Sungura.

Aliiomba Serikali kusikia kilio cha kuwarejesha wanafunzi hao chuoni, hoja iliyoungwa mkono na mwenzake, Mtinda akisema mtoto akikosea hafukuzwi au kuchapwa viboko, bali hukalishwa chini na kuelezwa matatizo yake, ili kumsaidia kumrekebisha na kumjenga.

Lakini Makilagi alisema hali ni mbaya na kwamba nyumbani kwake alikuwa na wanafunzi 50 ambao miongoni mwao wamesimamishwa kwa sababu tu ya mkumbo; kuingia waliomo na wasiokuwamo.

“Mimi naiomba Serikali sikivu ya CCM, itafakari kwa kina na iwarejeshe chuoni wanafunzi hawa. Mimi nyumbani kwangu nina wanafunzi 50, ambao baadhi yao wamesimamishwa kwa sababu ya mkumbo, si wavurugaji. Hawa wasamehewe, lakini waliohusika Serikali ichukue hatua kali dhidi yao,” alisema Makilagi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).

Mgomo na maandamano hayo ya wanafunzi wa Udom yaliyosababisha kusimamishwa kwa wenzao 400, yanadaiwa kuchochewa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini, na inaelezwa kumekuwapo na uharibifu mkubwa wa mali za chuo baada ya mgomo huo wiki hii.

Chanzo: Habari Leo. 19 JUNE 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages