KWELI WAHITIMU VYUONI HAWANA SIFA KATIKA SOKO LA AJIRA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

KWELI WAHITIMU VYUONI HAWANA SIFA KATIKA SOKO LA AJIRA


MMOJA wa watu wanaoheshimika sana katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika uendeshaji wa masuala ya biashara, Ali Mufuruki amesema jambo ambalo Watanzania wengi wamekuwa wanakosa ujasiri wa kulizungumzia.
 
Akizungumza mwanzoni mwa wiki wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili ya Umoja wa Watendaji Wakuu wa kampuni na mashirika makubwa yanayoendesha shughuli zake hapa nchini, Mufuruki, ambaye ni mwenyekiti wa umoja huo, alisema bila kutafuna maneno kwamba, vijana wengi wanaohitimu vyuo vikuu wanashindwa kupata ajira kwa kuwa hawana sifa zinazotakiwa katika soko la ajira.
 
Aliwaambia watendaji wenzake – ambao kimsingi ndio waajiri wa vijana wanaohitimu katika vyuo vyetu – kwamba vyuo vingi vinazalisha wahitimu wasio na sifa na ndiyo maana wanashindwa kupata ajira katika soko la ushindani kutokana na ukweli kuwa, mafunzo yao yanaendeshwa kinadharia tu pasipo kufanya mazoezi ya vitendo. Watendaji hao wakuu hukutana kila mwezi kujadili mada mbalimbali zinazohusu biashara na uchumi.
 
Katika chakula hicho cha usiku ambapo Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Marcelina Chijoriga alialikwa na kutoa mada kuhusu  namna gani pande hizo mbili zinaweza kushirikiana katika kutatua tatizo hilo, ambalo Mufuruki alisema linachangiwa pia na mitaala inayotumika kufundisha vitu ambavyo havihitajiki katika mazingira ya sasa ya soko la ajira. Alisema hicho hasa ndio chanzo cha makampuni na mashirika hayo kuajiri watu kutoka nje, tena kwa gharama kubwa.
 
Tunampongeza mwenyekiti huyo na watendaji wenzake katika umoja huo kwa kumvika paka kengele, hatua ambayo tunadhani itasaidia kuzifanya mamlaka husika kuchukua hatua za kuinua kiwango cha elimu nchini ili vijana wanaohitimu vyuoni wakubalike katika soko la ajira. Tunampongeza pia Dk Chijoriga kwa kukiri kuwapo tatizo na kusema shule yake tayari imeanzisha mfumo mpya ambapo wanafunzi watapaswa kufanya mafunzo kwa vitendo kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka sita.
 
Ni vigumu kuelewa kwanini Serikali haichukui hatua kuhakikisha wanafunzi walio vyuoni wanapata pia mafunzo ya vitendo kama ilivyokuwa siku za nyuma. Ni kweli kuwa imelemewa kiuchumi, kutokana na kuwa, hivi sasa idadi ya wanafunzi waliopo katika shule za msingi, sekondari na vyuoni imeongezeka na kufikia milioni 11. Tatizo la Serikali ni kuwa haitaki kulikubali tatizo, bali inalalamika na kufanya tatizo hilo lionekane kuwa ni la watu na taasisi nyingine.
 
Lakini tukubaliane angalao katika jambo moja kuwa, elimu ya nadharia katika shule na vyuo vyetu, pasipo pia kuwapo mafunzo  kwa vitendo ni sawa na sufuri. Kama alivyosema Mufuruki, soko la ajira katika mazingira ya sasa linahitaji zaidi ujuzi na umahiri wa kutenda badala tu ya elimu na maarifa. Ndiyo maana tunaunga mkono vyuo ambavyo vimekuwa vikitumia njia halali kuishinikiza Serikali na viongozi wa vyuo hivyo wakitaka pia wapewe mafunzo kwa vitendo. Inasikitisha kwamba, Serikali imekuwa ikidhani kuwa, kuwafukuza wanafunzi wanaodai kupewa mafunzo hayo ndiyo suluhisho la tatizo hilo.
 
Lazima Serikali na viongozi wa vyuo watambue kuwa, vyuo vikuu katika nchi zilizoendelea vimefanikiwa kulilidhisha soko la ajira kwa kuhakikisha kuwa mitaala ya vyuo hivyo inatayarishwa na kuelekezwa katika hali ya kuitikia  mahitaji ya viwanda na makampuni ya biashara. Hivyo, wahitimu wanajiajiri wenyewe au wanaajiriwa kirahisi kwa sababu tayari wanakuwa sio tu na maarifa na elimu, bali pia wanakuwa na ujuzi na umahiri katika fani husika.
 
Sisi tunakubaliana na Mufuruki na watendaji wenzake katika makampuni na viwanda kwamba, umefika wakati wa kubadilisha mfumo wa elimu kwa kuzihusisha sekta za biashara na viwanda katika kutayarisha mitaala itakayotumika katika kufundisha wanafunzi katika vyuo vyetu, lengo likiwa ni kuelekeza mitaala hiyo katika mahitaji ya sekta hizo.   

Chanzo: MWANANCHI, 16 JUNE 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages