NAPE NNAUYE: WATANZANIA WAPUUZENI WATU WANAOBEZA DHANA MPYA YA CCM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

NAPE NNAUYE: WATANZANIA WAPUUZENI WATU WANAOBEZA DHANA MPYA YA CCM


 Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM taifa Nape Mnauye akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo kikuu cha mabasi cha zamani mjini Singida.
Kikundi cha Uhamasishaji cha kijiji cha Manguanjuki kikitoa burudani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo kikuu cha mabasi cha zamani mjini Singida.Picha zote na Nathaniel Limu
---

Na. Nathaniel Limu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa Nape Mosses Mnauye amewataka Watanzania wawapuuze watu wanaobeza dhana mpya ya CCM ya kuvua ‘magamba’ kama nyoka, kwa madai kwamba watu hao ni mambumbu ambao hawajui faida zinazopatikana baada ya nyoka kujivua gamba.


Nape ametoa wito huo wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa manispaa ya Singida kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo kikuu cha zamani cha mabasi mjini Singida.


Mkutano huo uliitishwa kwa lengo la wajumbe wa sekretarieti ya halmashauri kuu ya CCM kueleza mikakati ya kukiimarisha chama hicho, ambapo amesema nyoka alivyoumbwa ni kwamba anatumia ngozi yake katika kumwezesha kujua hapa apite au asipite, kunusa na kuhisi.

Nape amesema lakini kuna umri fulani ukifika nyoka anapoteza uwezo wake huo na hapo ndipo inapomulazimu kutoa/kujivua  ngozi hiyo iliyozeeka na kutoa nafasi kwa  ngozi mpya.

Akifafanua zaidi amesema akishatoa ngozi hiyo ya zamani na kupata ngozi mpya, uwezo wake unaongezeka mara dufu na kuanza kufaidi maisha kama zamani.


Kwa maana hiyo Katibu huyo amesema umri wa CCM yenyewe ukijumlisha na wa TANU na ule wa ASP, sasa unakaribia kuzidi miaka 50, umri ambao amesema unapelekea kuwepo na mapungufu ya hapa na pale.


Amesema  “Baada ya mikutano yetu tuliyoifanya hivi karibuni pale Dodoma mjini, tulibaini hali hiyo ya kuwepo kwa mapungufu, sasa tumeamua kwa dhati kabisa kuyaondoa mapungufu hayo ili chama kiweze kupata nguvu mpya ya kuwatumikia Watanzania”.

Aidha Katibu huyo amesema kuvua magamba ni kuondoa mapungufu yanayochangia wananchi waanze kukosa imani na chama chao na si kufukuzana ndani ya chama kama ambavyo wapinzani wanajaribu kupotosha.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages