Phillip Magadula Shelembi (Ng'wana Byula) 1960-2011
--
Ni saa kumi na mbili asubuhi, mlango wa chumba changu unagongwa, kaka Zitto, kaka Zitto, ndivyo mama yangu Bi. Shida huita wanaye wote wa kiume. Naamka, mama ananiambia "Shelembi ametutoka". Ni kama ndoto hivi maana ni jana yake tu nilitoka kuongea na Katibu wa CHADEMA wa mkoa kuhusiana na hali ya mwenyekiti wake ndugu Shelembi. Baada ya kuzungumza na Dkt. Molekwa wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, nilipata ahueni kwamba mpiganaji wetu atapata matibabu stahili. Mungu hakutaka. Shelembi ametangulia mbele ya haki. Kwa heri. CHADEMA imepoteza mwanachama mahiri, Kiongozi asiyeyumba na mwenye misimamo. Wananchi wa Shinyanga, Kata ya Ndala na wananchi wote wa Manispaa ya Shinyanga wamepoteza Diwani makini mwenye uwezo mkubwa wa kutetea maslahi ya wananchi wake. Familia imepoteza baba mwema aliyependa familia yake.
Taifa limepoteza mmoja wa waasisi wa Mfumo wa Vyama vingi ambapo miaka ya karibuni tumeshuhudia watu wengi waliokuwa wameanzisha vyama hivi vipya wakijiunga na CCM. Pia wengine kutoka CCM ama kwa kupenda sera za vyama vipya au kwa kutafuta fursa za kiuchaguzi wamejiunga na vyama vipya na hata chama chetu cha CHADEMA. Shelembi hakuyumba licha ya changamoto mbalimbali ndani ya chama ambapo wakati mwingine ilidhaniwa angeweza kukata tamaa na kuondoka kwenye chama. Alibaki muumini mkubwa wa chama chetu na hata kupoteza maisha yake akiwa Kiongozi wa chama kitaifa kama Mjumbe wa Kamati Kuu, Kimkoa kama Mwenyekiti wa chama Mkoa na Kiwilaya kama Diwani wa Manispaa ya Iringa. Huu ni usia mkubwa kwetu na hasa vijana kwamba tuwe na uvumilivu wa kisiasa.
Ndani ya chama chetu tulimwita mashine ya kusaga na kukoboa. Kiukweli yeye ndiye alianzisha jina hili wakati anagombea ujumbe wa Kamati Kuu mwaka 2009. Uchaguzi ulikuwa mgumu sana, wanatakiwa wajumbe 3 tu wanaume Bara kati ya wagombea zaidi ya 20. Wasomi kama kina Dokta Kitila Mkumbo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanazuoni mwenzake Prof. Mwesiga Baregu walikuwa katika kundi hili. Kulikuwa na wagombea kama Ndugu Msigwa ambaye sasa ni Mbunge wa Iringa Mjini na wengine wengi. Shelembi, mashine ya kusaga na kukoboa aliongoza katika kundi hili akifuatiwa na Baregu na Kitila Mkumbo. Hii ilionyesha mapenzi makubwa aliyokuwa nayo ndani ya chama chetu. Walioompenda na wasiompenda walimpa kura. Kila mjumbe alipenda misimamo yake kwa mambo aliyoyasimamia. Hakufinyanga maneno wala kumung'unya. Alisema alichoamini, jina hili lilimfaa kabisa.
Shelembi alikuwa tayari kubakia peke yake na msimamo wake hata kama kikao kizima kinampinga. Nakumbuka wakati tumekaa katika kikao cha Kamati Kuu Dodoma tukiwa na changamoto kubwa ya kumsimamisha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Bara marehemu Chacha Wangwe, Ndugu Shelembi alisimama peke yake mpaka mwisho kupinga kusimamishwa kwa Wangwe. Nakumbuka alisimama na kusema kwa lugha yake ya kiswahili cha kisukuma "eeh, kumbe siasa ndio hivi, nimeogopa kabisa, yaani na wewe {akimtaja mmoja wa wajumbe} unakubali makamu asimamishwe wakati tulikuwa wote kupinga hili? Kwa kweli licha ya "tension" iliyokuwepo kikao kiliangua kicheko. Alikuwa na namna yake ya kuwasilisha hoja yake. Alikuwa mzungumzaji mzuri. Hakuogopa kusema mawazo yake. Alisimamia demokrasia ya kweli ndani ya vikao vya chama. Hili ni fundisho kwa wanaCHADEMA tuliobakia. Kuwa na misimamo bila kuathiri uhai wa chama. Kwamba tofauti ya mawazo ndiyo kushamiri kwa demokrasia.
Kuna watu walitaka kujaribu kutumia tofauti kadhaa za mawazo ndani ya chama kumfanya akiasi chama. Alikataa. Alikuwa mwanaCHADEMA kindakindaki. Alikipenda chama sio kinafiki, alichukia unafiki kwa maana ya kuuchukia. Alihakikisha chama kinajengwa katika mkoa wake na hata kutoa Wabunge wengi zaidi wa kuchaguliwa wa CHADEMA kuliko mkoa mwingine wowote Tanzania Bara, na kuufanya Mkoa wa Shinyanga kuwa Mkoa wa Pili kwa kutoa Wabunge wengi zaidi wa Upinzani. Shelembi alikuwa Kamanda Makini na Mahiri. Umetuachia changamoto ya kuendeleza ushindi wetu na kuhakikisha tunabeba majimbo yaliyobakia katika mkoa wa sasa wa Shinyanga ambao umegawanywa kutoa mikoa ya Simiyu na Geita. Ni Changamoto ambayo tupo tayari kuichukua. Tunaweza kama ulivyoweza Shelembi! Umeshatuwekea Msingi imara.
Ndugu Shelembi hakuwa Mwenyekiti wa Mkoa aliyepeleka mbele wapiganaji na yeye kubakia nyuma, hapana. Yeye mwenyewe aligombea jimbo la Shinyanga mjini na pia udiwani kata ya Ndala. Alishinda vyote. Akatangazwa mshindi kwenye udiwani, akapokonywa Ubunge. Kuna mkanganyiko wa kura alizopata, yeye alisema alitangazwa ameshindwa kwa tofauti ya kura moja, Mbunge wa Shinyanga Mjini ndugu Masele Stephen anasema hapana, ilikuwa ni tofauti ya asilimia moja. Hakukubali uchakachuaji huu wa haki yake. Alikwenda Mahakamani. Amefariki akiwa anapigania haki yake mahakamani. Nakumbuka mara ya mwisho nilikutana naye akiwa Dar es Salaam kumwona Wakili Mabere Marando kuhusiana na kesi. Alikuwa ana ari ya kuhakikisha anashinda kesi ili atangazwe kuwa Mbunge halali wa Shinyanga Mjini. Hii ni changamoto nyingine iliyo mbele yetu, kuhakikisha haki hii ya watu wa Shinyanga inalindwa. Kamanda Shelembi, umetangulia. Tutaifanya kazi hii. CHADEMA itaendeleza kazi hii. Chama chako ulichokipigania toka kianzishwe hakitakutupa.
Nikimnadi Ndugu Philip Shelembi Magadula-SHINYANGA MJINI
--
Aliendesha kampeni zake za mwaka 2010 kwa michango ya wananchi. Nakumbuka nilipopita Shinyanga katika ziara yangu ya kunadi wagombea Ubunge, tulipata watu wengi katika mkutano. Kofia na mifuko ya Rambo ilipita mara baada kuzungumza. Michango ilikuwa ni ya shilingi 50, 100, 500 na 1000. Wananchi wa kawaida kabisa waliitikia wito wa kumchangia mafuta aweze kwenda mkutano wa Pili. Tulikusanya zaidi shilingi laki Sita na ushee ndani ya nusu saa tu. Jimbo pekee lililozidi Shinyanga Mjini ya Shelembi ni Jimbo la Sumbawanga Mjini ambapo tulikusanya shilingi Laki Nane na nusu. Shelembi, tangulia. Ulipendwa sio kwa mali zako bali kwa uwezo wako wa kutetea haki za watu wako.
Tuna majonzi tu kuwa hutaona wakati tunachukua Dola mwaka 2015. Naamini utatutumia salam huko ulipo. Nenda. Msalimu Chacha Rasta! Mwambie chama kipo imara. Harakati zinaendelea.
Watu wa Shinyanga walimpenda Shelembi. Hakuwa na ukwasi. Ni mwananchi wa kawaida kabisa kabisa. Ninapoandika makala hii ya kumuaga, ninapata fahari ya mambo mawili. Moja kwamba ndani ya nchi yetu, bila kujali uwezo wa kifedha w mtu bado unaweza kuwa kiongozi. Mbili, kwamba ndani ya chama changu, mtu masikini kabisa na hohe hahe ana fursa ya kutekeleza haki yake ya kidemokrasia. Shelembi alikuwa ni mtu wa daraja la chini, hakuwa middle class, lakini aliweza kutumia haki yake ndani ya chama chetu. Inatia moyo kuwa bado misingi ya waasisi wa Taifa ipo.
Aliendesha kampeni zake za mwaka 2010 kwa michango ya wananchi. Nakumbuka nilipopita Shinyanga katika ziara yangu ya kunadi wagombea Ubunge, tulipata watu wengi katika mkutano. Kofia na mifuko ya Rambo ilipita mara baada kuzungumza. Michango ilikuwa ni ya shilingi 50, 100, 500 na 1000. Wananchi wa kawaida kabisa waliitikia wito wa kumchangia mafuta aweze kwenda mkutano wa Pili. Tulikusanya zaidi shilingi laki Sita na ushee ndani ya nusu saa tu. Jimbo pekee lililozidi Shinyanga Mjini ya Shelembi ni Jimbo la Sumbawanga Mjini ambapo tulikusanya shilingi Laki Nane na nusu. Shelembi, tangulia. Ulipendwa sio kwa mali zako bali kwa uwezo wako wa kutetea haki za watu wako.
Tuna majonzi tu kuwa hutaona wakati tunachukua Dola mwaka 2015. Naamini utatutumia salam huko ulipo. Nenda. Msalimu Chacha Rasta! Mwambie chama kipo imara. Harakati zinaendelea.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)