WAZIRI MKUU PINDA ATEMBELEA FAMILIA YA HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WAZIRI MKUU PINDA ATEMBELEA FAMILIA YA HAYATI EDWARD MORINGE SOKOINE


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa na  Wajane wa  aliyekuwa Waziri Mkuu  hayati Edward Moringe Sokoine,  Napono Sokoine(watatu kushoto)na Nakiteto Sokoine(kulia)na Binti yao Nameloki Sokoine ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum katika makabidhiano ya CD yenye wimbo wa Sokoine ulioimbwa na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (wapili kulia) akishirikiana na Mwimbaji wa nyimbo za kizazi kipya, Bushoke (hayupo pichani) baada ya ibada ya kumbukumbu ya Sokoine iliyofanyika kwenye kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Mjini Dodoma leo   Aprili  12, 2011.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
---


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania wana mengi ya kujifunza kutoka aliyekuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine kwa jinsi alivyokuwa kielelezo cha utumishi wa watu na kielelezo cha kupigania wanyonge. Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumanne, Aprili 12, 2011) wakati akitoa salamu za Serikali katika ibada ya kumbukumbu ya miaka 27 ya kifo cha hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mt. Paulo wa Msalaba mjini Dodoma. 

“Marehemu Sokoine atakumbukwa kwa mengi ambayo kwa kweli tukiyaongelea hapa hatutayamaliza; ninachoweza kusema, leo tunamkumbuka mtu ambaye kwetu sisi Watanzania, ni kielelezo bora cha utumishi wa watu, kielelezo cha kujituma, kielelezo cha upendo, kielelelzo cha kupenda haki kielelezo cha kupigania wanyonge na kielelezo cha kumcha na kumtumikia Mungu,” alisema. Alisema katika utumishi wake, Mzee Sokoine alifanya bidii kutetea wanyonge na maslahi yao kwa kupambana na watu wanaohodhi bidhaa (walanguzi na wahujumu uchumi) hadi wakasalimu amri.

“Wakati akitangaza vita dhidi ya walanguzi, nakumbuka alitoa kauli hii: Kama wanasema Serikali ilikuwa likizo, sasa wajue kuwa likizo imekwisha,” alisema Waziri Mkuu akimnukuu hayati Sokoine. “Alitumia muda mwingi kujenga jamii inayochukia rushwa na ulanguzi... Japo hayupo kati yetu kimwili, faraja ninayoipata mimi kama Pinda, tunapoadhimisha kumbukumbu kama hii ni kuwa bado huyu mwenzetu tuko naye kimawazo, kiakili na kubwa zaidi kiroho,” alisema. Waziri Mkuu alisema marehemu Sokoine alikuwa kiongozi wa kipekee kwani aliamini kwamba, kuwajibika kama kiongozi ni kukubali kwa hiari dhamana ya uongozi unayopewa ama kwa njia ya kuomba kwa kura au kwa kuteuliwa Kikatiba au Kisheria.

“Aliamini kuwa Kiongozi lazima akubali kutumia dhamana ya uongozi aliopewa kwa maslahi ya umma na kwa Taifa kwa ujumla.” Waziri Mkuu Pinda alisema: “Marehemu Sokoine amefanya mengi mazuri ambayo tunayakumbuka leo. Hebu tujifunze kutoka kwake kwamba; mazuri tunayoyafanya leo, huwa furaha ya kesho. Tumuige kwa kufanya mazuri ambayo yatakumbukwa daima na vizazi vijavyo,” alisema. “Marehemu Sokoine alikuwa muasisi wa biashara huria nchini wakati tukiwa kwenye itikadi ya Ujamaa. Aidha, alikuwa na wazo zuri la kuanzisha usafiri wa daladala Dar es Salaam. Wakati wake mabasi makubwa ya ofisini yalitumika kubeba watu Jijini Dar es Salaam na hii ni kielelezo cha kuujali umma wa Watanzania,” alisema.

Mapema akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Askofu Gervas John Nyaisonga alisema kumbukumbu ya kifo cha Sokoine iwakumbushe Watanzania ni nini cha kujifunza kutoka kwake kuenzi tunu alizoacha. Alisema alikuwa mtu wa kipekee kwani alijitolea kukatwa asilimia 50 ya mshahara wake ili kuchangia katika mfuko wa nguvukazi ili wananchi wasio na uwezo wa kukopa benki waweze kupata mikopo kutoka katika mfuko huo. 

Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Nyaisonga kwa kushirikiana na mapadri wengine saba ilihudhuriwa na wanafamilia wa Sokoine, Spika wa Bunge, Bibi Anna Makinda, Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Edward Lowassa, Wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, wakuu wa wilaya na waumini mbalimbali kutoka Dodoma, Mvomero na Arusha. Edward Moringe Sokine ambaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 46, aliwahi kuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili cha kwanza kikiwa ni Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na kipindi cha pili kuanzia Februari 23, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki kwa ajali ya gari Wami Dakawa, mkoani Morogoro akiwa njiani kurejea Dar es Salaam kutoka Dodoma ambako alikuwa akihudhuria mkutano wa Bunge.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages