MASHINDANO YA DAR SECONDARY SCHOOL CUP YAZINDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

MASHINDANO YA DAR SECONDARY SCHOOL CUP YAZINDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM

Waratibu wa Mashindano ya Dar Secondary School Cup Jeremiah Makwabi na Annick Verstraelen kutoka UYODEO ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo wakitoa maelekezo kwa shule shiriki kabla ya kuzinduliwa kwa mashindano hayo.
Shafii Dauda kutoka  Jarida la  Number 10 akihimiza wanafunzi kuonyesha vipaji vyao katika mashindano hayo na kuahidi kuwaendeleza zaidi kimichezo.
Timu ya Shule ya Sekondari Makongo.
Timu ya Shule ya Sekondari Kinondoni Muslim katika picha ya pamoja.
---
Na.Mwandishi wetu
Mashindano ya mchezo wa soka ya DAR SECONDARY SCHOOL CUP yanayoshirikisha vijana wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam wenye umri chini ya miaka 16 yamezinduliwa rasmi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar – UDSM.

Mashindano hayo yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Upendo Youth Development Organization – UYODEO lenye makao yake makuu huko Kilwa – Masoko.Akizungumza na MO BLOG Mjumbe wa Heshima wa UYODEO na Mratibu wa mashindano hayo Annick Verstraelen  amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwakutanisha pamoja wanafunzi kutoka shule mbali mbali chini ya kauli mbiu ya ‘TUCHEZE PAMOJA’ ili waweze kufahamiana, kushiriki michezo pamoja na kujenga uhusiano.

Amefafanua kuwa mashindano hayo pia yanalenga kutafuta, kukuza na kuvitumia vipaji miongoni mwa wanafunzi ili waweze kujitambua wakiwa bado katika umri wa kukua.

Mashindano hayo mwaka huu yamehusisha timu za shule sita (6) kutoka wilaya ya Kinondoni, lakini ni matarajio ya UYODEO kupanua wigo ya mashindano hayo na kufanyika pia katika wilaya za Ilala na Temeke.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kuandaa na kufanikisha mashindano hayo, Annick amesema uhaba wa fedha umekuwa ni kikwazo kikubwa kutokana na gharama za maandalizi kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wa shirika hilo, hivyo ametoa wito kwa wadhamini kujitokeza ili kuwezesha mashindano hayo kufanikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa.

Aidha Annick ametoa wito kwa wazazi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia mashindano hayo, ili waweze kujionea nini watoto wao wanafanya uwanjani na kuweza kuwapa moyo na kuwaunga mkono ili waweze kutimiza malengo yao katika michezo, kwani michezo ni afya.

Shule za Sekondari za wilaya ya Kinondoni zinazoshiriki mashindano hayo ni Kinondoni Muslims, Salma Kikwete, Makongo Sekondari, ESACS, Mtakuja Beach na DIS.
Shule hizo zimepangwa katika makundi mawili yenye timu tatu kila moja, ambapo kila shule itapaswa kucheza mechi mbili katika mfumo wa ligi. 

Kundi la kwanza lina timu za shule za Mtakuja Beach, DIS na Kinondoni Muslim wakati kundi la pili lina timu za Salma Kikwete, Makongo na ESACS. 

Mechi za ligi ya mashindano ya DAR SECONDARY SCHOOL CUP zitafanyika tarehe 30 April na tarehe Mosi Mei 2011.

Kwa upande wa udhamini makampuni yaliyojitokeza kudhamini kwa namna moja ama nyingine kuwezesha ufunguzi wa mashindano hayo ni pamoja na Aurora Premium Outlet Security (T) Ltd, Image Masters, Continental, MO BLOG –More Benefits, PPF na Azam Football Club.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages