JUMA KASEJA KURUDI YANGA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

JUMA KASEJA KURUDI YANGA


Na Erasto Stanslaus
KLABU ya Yanga ipo mbioni kumsajili tena kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja(pichani) katika usajili wa msimu ujao ili kuimarisha lango lao baada ya Yaw Berko kusumbuliwa na bega mara kwa mara.

Mbali na Yanga, Kaseja ambaye aliwahi kucheza Yanga msimu wa 2008/09 pia anawaniwa na Azam FC ambayo imeshamsajili Obren Curkovic raia wa Serbia kwa msimu ujao.

Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa kipa huyo, klabu hizo zipo katika vita ya kumnasa Kaseja ambaye kwa sasa anaonekana kushuka kiwango kutokana na kutofanya vizuri katika baadhi ya michezo akiwa na Simba.

Rafiki huyo alisema: “Unajua ukisema cha nini wenzio wanasema watakipata lini, Simba wanaona Kaseja ameshuka kiwango lakini wangejua kuwa anawindwa na timu hizo wasingefikiria kusema hayo.

“Kilichopo kwa sasa ni kushindikana kwa dau kwa klabu hizo kwani timu zote zimeshakutana na Kaseja lakini naye anachekecha wapi kuna maslahi zaidi kati ya timu hizo.”

Kaseja alipotafutwa hakupatikana kwani namba yake iliita bila ya kupokelewa lakini Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu alisema: “Siwezi kukataa wala kukubali kuhusu usajili wa Kaseja, tunafanya mambo kwa siri sasa.”

Mwaka 2008, Yanga ilimsajili Kaseja kwa dau la zaidi ya Sh milioni 38 na kuichezea kwa msimu mmoja kabla ya kurejea Simba alikosaini mkataba wa miaka miwili unaomalizika Juni mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages