Dk HARRISON MWAKYEMBE: SERIKALI KUANZA KUTUMIA WAKANDARASI WAZALENDO KWENYE UJENZI WA BARABARA NCHINI - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

Dk HARRISON MWAKYEMBE: SERIKALI KUANZA KUTUMIA WAKANDARASI WAZALENDO KWENYE UJENZI WA BARABARA NCHINI

 Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza kwenye kikao na watendaji wa mkoa wa Singida.
 Dk. Mwakyembe (suti nyeusi) akipewa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Singida – Katesh na mkandarasi mshauri.
 Meneja TANROADS mkoa wa Singida Mhandisi Yustaki Kangole akifurahia jambo na Naibu Waziri Dk. Mwakyembe na mkandarasi mshauri (mwenye kofia) wakati wanakagua ujenzi wa barabara ya Singida-Katesh yenye kiwango cha lami.
 Dk. Mwakywmbe akiagwa na uongozi wa mkoa wa Singida mpakani mwa mkoa wa Singida na mkoa wa Tabora.Wa pili kushoto ni meneja TANROADS mkoa wa Singida Yustaki Kangole na wa pili kulia ni mbunge wa jimbo la Tabora mjini Aden Rage.
Mitambo ya kuweka lami kwenye barabara ya Singida – Katesh eneo la Kititimo manispaa ya Singida.Picha zote na Nathaniel Limu
----
Na.Nathaniel Limu, Singida.
Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harrison Mwakyembe (Mb) amesema serikali inaandaa mkakati wa kupunguza gharama kubwa za ujenzi wa barabara zinazotozwa hivi sasa na makandarasi kutoka nje ya nchi.
Amesema kuendelea kulipa gharama hizo kubwa pamoja na kutekeleza masharti yanayotolewa na makandarasi hao hakutafanikisha lengo la serikali la kuwa na barabara nyingi za lami nchini.
Dk. Mwakyembe amesema hayo muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi na uboreshaji wa barabara mkoani Singida iliyotolewa na meneja wa TANROADS mkoa Mhandisi Yustaki Kangole.
Akifafanua amesema makandarasi hao kutoka nje ya nchi wamepandisha mno gharama ya ujenzi wa barabara za lami, kutoka shilingi milioni 350 kwa kilomita moja mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 1.5.
Aidha Naibu Waziri huyo amesema sasa msisitizo mkubwa utaelekezwa katika kuwapatia kazi ya ujenzi makandarasi wazalendo ambao pamoja na mambo mengine wana uchungu na nchi yao.
Katika hatua nyingine Dk. Mwakyembe amesema pamoja na kushughulikia suala la kushusha gharama za ujenzi wa barabara, pia watachunguza na kufanya mabadiliko makubwa katika mikataba ambayo mingi, amedai haiionei uchungu nchi hii.
Wakati huo huo amewataka wafanyakazi waliochini ya wizara ya ujenzi kurejesha uadilifu na weledi ili kazi zinazofanywa na kusimamiwa ziwe bora kwa mujibu wa mikataba husika na ziweze kudumu kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages