BABU ANUSURIKA KUUAWA NA WANAWAKE TISA - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

BABU ANUSURIKA KUUAWA NA WANAWAKE TISA


Njama za wanawake kutaka kumuua Mchungaji Ambilikile Masapile ‘Babu’  (pichani) nyumbani kwake katika Kijiji cha Samunge, Loliondo zimegundulika.

Akitangaza habari hizo kwenye kipaza sauti nyumbani kwa mchungaji huyo, mmoja wa wasaidizi wake, Frederick Nisajile alisema wanawake hao waliokuwa na njama hizo walikuwa tisa.

“Wapo wanawake tisa ambao walitumwa kutaka kumuua Babu, tumewagundua, wataumbuka,” alisema msaidizi huyo bila kuwataja kwa majina wanawake hao.

Akifafanua zaidi, msaidizi huyo wa Babu alisema wanawake hao walikuwa wanajifanya kutaka kumgusa Babu ili wamdhuru.

“Tulipowahoji  walisema walitaka kumgusa Babu kama enzi hizo mwanamke mmoja aliyekuwa akitokwa na damu miaka kumi na miwili  alivyofanya kwa Yesu kwa kugusa pindo la nguo yake,” alisema.

Alibainisha kuwa Babu sasa haguswi na pindo la mchungaji lipo kwenye kikombe, hivyo anayetaka uponyaji awe kwenye foleni na atakapokunywa dawa, ataponywa.

Hivi sasa Babu analindwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na haijajulikana ulinzi huo unatokana na madai hayo mazito au ni utaratibu wa kawaida uliofanywa na serikali.
Aidha, Babu Masapile ametoa onyo kuwa watu wote watakaoiba simu katika eneo hilo masikio yao hayatasikia na watakuwa viziwi na wale watakaoiba fedha, watapofuka macho.

“Tayari kuna mtu aliiba shilingi 25,000 akapofuka na kwenda polisi mwenyewe kukiri kisha alimuomba Babu kuwa atazirudisha ili aweze kuona tena,” alisema msaidizi huyo.
Mara baada ya hotuba ya msaidizi huyo, Mchungaji Masapile alikamata kipaza sauti na kuwaonya wote wanaoingiza itikadi za vyama vya siasa katika tiba yake.

Alisema amepata habari kuwa kuna baadhi ya watu wanashambulia viongozi wa vyama barabarani wakati wanakwenda kupata kikombe, akawaonya kuwa waache kufanya hivyo kwa sababu Mungu atawaadhibu.

“Kuna malalamiko pia kuwa baadhi ya watu wanaosimamia foleni wanapewa hongo, nawaambia hiyo ni hatari maana utafilisika,” alisema Mchungaji huyo mstaafu wa KKKT.

Aidha, aliwaonya waandishi wa habari wanaoandika habari za uongo kuhusu tiba hiyo. “Msiharibu kazi ya Mungu, nilisoma katika gazeti eti kuna mtu alibakwa hapa, sisi hatujasikia hilo, naomba kama kuna mtu atapatwa na jambo aje kutuambia.

 “Mimi ni mtu mdogo sana ndiyo maana Mungu akanichagua kutoa dawa hii ambayo si kwamba inatibu magonjwa sugu kama inavyotangazwa bali yale ambayo hayana dawa kama vile ukimwi, pumu, kisukari, figo na mengine mengi,” alisema Babu.
Kwa Msaada Wa Global Publishers Tanzania

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages