WANAFUNZI SHULE YA SHERIA WADAI FEDHA KWA MAANDAMANO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

WANAFUNZI SHULE YA SHERIA WADAI FEDHA KWA MAANDAMANO

WANAFUNZI wa Shule ya Sheria wamelazimika kufanya maandamano ya amani hadi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba jijini Dar es Salaam kutokana na utata uliojitokeza katika mkopo waliouomba serikalini kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya jengo la Wizara ya Sheria na Katiba, Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule hiyo ya Sheria, Kanani Chombala alisema baada ya kukosa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya wanafunzi walichukua jitihada mbalimbali kukutana na viongozi wa serikali akiwemo Waziri Mkuu Mizengwe Pinda ili waweze kupata mikopo ambayo watalipa pindi watakapoajiriwa.

Chombala alisema mawasiliano hayo yalizaa matunda baada ya kuahidiwa kupata mkopo wa Sh milioni 249 kwa ajili ya kugharamia wanafunzi 240 chakula, malazi na vitabu.

Hata hivyo baada ya kufungua shule waliambiwa kuwa fedha iliyoidhinishwa na Hazina ni Sh milioni 49.

Alisema licha ya tofauti kubwa iliyojitokeza hata kiasi hicho kidogo hakijawafikia wanafunzi jambo ambalo lilisababisha wanafunzi kukosa imani na viongozi wao.

“Sisi viongozi tuliwaeleza wanafunzi kilichotokea lakini hawakutuamini kwa sababu jambo lenyewe linaleta utata hivyo tuliamua kufanya maandamano ya amani na kuomba kukutana na Katibu Mkuu ili kupata ufafanuzi,” alisema Chombala.

Baada ya Katibu Mkuu kukutana na wanafunzi hao aliwambia wavute subira kwa kuwa fedha hizo zitatoka tarehe 18 mwezi huu.

Hata hivyo wanafunzi hao wameingiwa na hofu ya kufeli mitihani kwa sababu wanatarajia kuanza mitihani tarehe 15 mwezi huu na walikuwa wanategemea fedha hizo kwa ajili ya kununua vitabu vya sheria mbambali ambavyo wanatakiwa kutumia kwenye mitihani.

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages