Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kushoto wake ni Naibu wake, Dkt. Asha-Rose Migiro na kulia Bw. Joseph Deiss, Rais wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa, maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila March 25 yalifanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum
Mwishoni mwa wiki, Umoja wa Mataifa uliadhimisha siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa utumwa na biashara ya utumwa.
Maadhimisho hayo ambayo ujumbe wake kwa mwaka huu ulikuwa “ the living legacy of 30 million untold stories” hufanyika kila March 25 yaliambatana na makongamano, maonesho ya dhana zilizotumika kusafirishia watumwa, ngoma za kiafrika na vyakula vya asili ya afrika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu wa kuendelea kufundishwa kwa historia ya utumwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Ban Ki Moon anasema kwa kufundisha na kujifunza historia ya utumwa na biashara ya utumwa pamoja na madhara makubwa yaliyotokana na biashara hiyo, itakuwa ni njia moja wapo ya kuwaenzi wahanga wa utumwa. Lakini pia kujifunza nini kilipelekea kuanzishwa kwa biashara hiyo.
Akasema kuwa UNESCO imefanya kazi kubwa ya kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na matukio ya kutisha na utumwa na biashara ya utumwa. Lakini anakiri kuwa bado kuna mengi ya kujifuza kuhusu mamilioni ya waafrika walioathirika na biashara hiyo. kwamba kazi hiyo inatakiwa kuendelea mashuleni na katika maeneo mengine.
Katibu Mkuu wa UM, katika mazungumzo yake, amesisitiza kuwa biashara hiyo ya utumwa ilikuwa ni moja ya biashara mbaya sana iliyokandamiza na kuudhalilisha utu na hadhi ya mtu mweusi na kwamba madonda biashara hiyo bado yapo hadi leo hii.
“ kwa kuadhimisha siku hii ya kimataifa, ni sehemu ya kuwakumbuka wahanga wa utumbwa, tunatambua utu wao, heshima yao, kudhalilishwa kwao na mateso waliyoyapata” anasisitiza Ban Ki Moon
Na kuongeza kuwa maadhimisho haya pia yanalenga kutambua mchango wa wale wote waliojitolea mhanga licha ya hatari kubwa iliyowakabilia kuipinga na hatimaye kumaliza biashara ya utumwa.
“ Hili hasa ndio kusudio la maadhimisho ya siku hii ya kimataifa ya watu wa asili ya afrika. Na ndio maana mchakato wa ujenzi wa mnara wa kumbumbu ya biashara ya utumwa unaendelea kama njia moja wapo ya kuendelea kuwaenzi wahanga hao.” Anaeleza zaidi
Kwa Mujibu wa Katibu Mkuu, maadhimisho hayo pia yalikuwa yanalenga kutambua mchango na juhudi za wanaharakati ambao hadi leo hii wanaendelea na kazi ya kupigania na kupinga aina mbalimbali za ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Aidha Ban ki Moona, anasema kuwa ingawa miaka 400 imepita tangu kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, kumeibuka aina mpya ya utumwa, anautaja utumwa huo kuwa ni ndoa za umri mdogo, usafirishaji haramu wa watoto, uuzwaji wa wanawake, na utumwa wa madeni unaowalazimu baadhi ya sehemu ya jamii kufanya kazi kwa muda mrefu kulipia madeni ya familia zao.
“Ni vema tukautambua ukweli wa biadhara ya utumwa, hebu basi na tuwakumbuke wahanga hao. lakini lazima pia tukumbuke na aina mpya ya utumwa unaoendelea katika jamii zetu na tukusanye nguvu za kuukabili utumwa huu mpya” anasisitiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)