SUMAYE ATINGA LOLIONDO - LUKAZA BLOG

All You Want is Here | Chochote Unachohitaji Utakipata Hapa

Habari Mpya

SUMAYE ATINGA LOLIONDO

http://www.habarileo.co.tz/pics/09_10_qhv8yc.jpg
WAKATI mamia ya watu wakiendelea kumiminika kupata tiba ya dawa ya magonjwa sugu kwa mchungaji wa KKKT  katika Kijiji cha Samunge, Wilayani Loliondo, jana ilikuwa zamu ya Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (pichani) kupata kikombe cha babu huyo.

Hatua ya Sumaye ni mwendelezo wa uwazi kwa viongozi wanaokwenda Samunge siku za karibuni tofauti na awali ambao baadhi ya vigogo walidaiwa kwenda kupata tiba hiyo kwa kificho.Lakini, kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa ambaye alifika Samunge, Loliondo siku tatu zilizopita na kunywa kikombe cha Babu, jana Sumaye naye alifika kijijini hapo kunywa kikombe hicho.

Akiongozana na watu kumi wa familia yake, Sumaye alifika kijijini Samunge  saa 7 mchana ambapo alipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Loliondo, Elias Wawalali ambaye kwa kutumia njia maalumu ya viongozi alipelekwa moja kwa moja kwa Mchungaji Mwasapile na kunywa dawa hiyo.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaofika kijijini Samunge kunywa dawa hiyo ya maajabu kwa mchungaji Mwasapile ambaye alisema kuwa anatoa tiba hiyo baada ya kuoteshwa na Mungu.

Mchungaji Loliondo awajibu Kakobe, MwingiraKatika hatua nyingine, Mchungaji huyo jana alivunja ukimya na kuwajibu baadhi ya viongozi wa dini waliomtuhumu kuwa tiba anayotoa ni ya nguvu za giza akisema kuwa waliotoa tuhuma hizo wana mtazamo wa kifedha zaidi na siyo imani.

Miongoni mwa viongozi ambao walitoa matamshi makali dhidi ya Mchungaji Mwasapile, ni Askofu Zakary Kakobe  wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efata ambao walikaririwa na vyombo vya habari wakituhumu tiba hiyo kwamba ni ya nguvu za giza.

Lakini, jana Mchungaji Mwasapile alisema,“..Hao (Kakobe na Mwingira) hawapo kiimani, wana mtazamo wa kifedha zaidi.

Ninachowaomba, wasiwazuie wengine kuja kupata tiba na wao wakitaka waje kupata tiba hii.”Alisema viongozi hao na watu wengine wasifikirie kuwa yeye anatoa tiba hiyo ili kutafuta sifa binafsi, kwa madhehebu, dini au kikundi fulani cha watu bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

Mchungaji huyo pia alitoa tahadhari akiwataka watu kutowatorosha wagonjwa hospitalini kwa ajili ya kuwapeleka kwake wakiwa mahututi.Aliwataka wananchi wajihadhari na utapeli ulioibuka kwa baadhi ya watu kuwa wana dawa hiyo akisisitiza kuwa tiba yake ameoteshwa na Mungu na hakuna yeyote anayetoa bali yeye.

Wakati huo huo, Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba Asilia Tanzania (Chawatiata), kimedai kushangazwa na  viongozi wa Serikali  kupanga foleni  mchana kweupe  kupata huduma ya dawa kwa Mchungaji Ambikilile  Mwasapile wakati wanapoenda kwa waganga wengine wa kienyeji, huenda kwa kujificha.

Kauli hiyo imekuja, siku chache baada ya vigogo wengi serikalini kwenda kwa mchungaji huyo maarufu kwa jina la 'Babu' wakiwamo Mbunge wa  Vunjo (TLP), Augustino Mrema na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Dawa ya mchungaji huyo imejizolea umaarufu wa kutibu magonjwa sugu kiasi cha kuwafanya hata wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja nchini kutibiwa.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi Katibu Mkuu wa Chawatiata, Mittam Magombeka  alisema waganga wa tiba asilia wamekuwa wakidharauliwa na hata kuonekana kuwa ni aibu kupata tiba kwao.Jambo hilo alisema limekuwa likiwafanya baadhi ya wale wanaoamini tiba hizo kwenda kwao kwa siri ili wasionekane na watu.
CHANZO: MWANANCHI MACHI 18, 2011

No comments:

Post a Comment

Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)


Pages