Shirikisho la umoja wa muziki wa taarabu nchini limetoa muda wa siku tatu za maombolezo ya wamamuziki wa kundi la Five Star waliofariki katika ajali ya gari, kuanzia juzi kwa kusimamisha maonyesho yote ya muziki wa taarabu katika jiji la Dar es Salaam.
Wakati Shirikisho hilo likisimamisha maonyesho yake, baadhi ya watu wasiojulikana waliibuka na kujipenyeza katika eneo la Bar ya Equator Grill Temeke juzi wakati wa shughuli za kupokea na kuaga miili ya waliokuwa wanamuziki wa kundi la five star na kuanza kutoza viingilio kwa wananchi waliofika eneo hilo kwa lengo la kuaga miili hiyo.
Watu hao wamedaiwa kuwa walikuwa wakitoza kiasi cha kati ya Sh.5,000 hadi 15,000, kwa baadhi ya waombolezaji walifika katika ukumbi huo kuwaona majeruhi wa ajali hiyo na kupokea miili ya wasanii hao 13 waliokufa katika ajali ya gari mkoani Morogoro wakiwa njiani kutoka mkoani Mbeya kuja jijini Dar.
Mmoja kati ya waombolezaji anayedaiwa kutozwa kiingilio, aliyejitambulisha kwa jina la John Mussa (50) mkazi wa Singida, alifika ukumbini hapo kwa ajili ya maombolezo na kushiriki mapokezi ya majeruhi na maiti za wasanii hao ila ambapo alikutana na vijana mlangoni na kumtoza kiingilio cha shilingi 10,000 na vijana hao, walidai kuwa kuingia ukumbini humo ni kwa pesa na kiasi walichonitajia.
"Mimi nilikuwa ni miongoni mwa watu wa kwanza kwanza kufika eneo hilo na kutokana na ugeni niliwauliza vijana waliokuwa nje ili kunionyesha ukumbi huo, walinipeleka hadi mlangoni mwa ukumbi wa bar hiyo ya EquatorGrill na kabla ya kuingia ndani niliambiwa nisogee pembeni kwanza tukubaliane kuingia.
Tukiwa pembeni kidogo waliniambia ukumbi huo ili kuingia na pesa wakubwa shilingi 15,000 na watoto 5000 kutokana na kutokuwa na pesa hiyo walinipunguzia hadi shilingi 10,000 ndipo nilipoonyeshwa mlango wa kuingia ndani huku wakinitaka niwahi nafasi ya mbele ili kuweza kuona vizuri" alisema John
Alisema mzee huyo na kudai kuwa katika safari yao walikuwa wawili na mwenzake alitozwa shilingi 5000 kwa kuwa ni kijana wa miaka 20 kwa madai kuwa ni mtoto.
Hata hivyo alisema baada ya kufika ndani kutokana na msongamano uliokuwepo hakufanikiwa kuona vizuri na baada ya kuhoji mmoja kati ya waombolezaji aliyekuwa jirani na eneo alilokaa ili kujua wamemtoza kiasi gani na kujua eneo la viti maalum (V.I.P) ndipo alipobaini kuwa ameingizwa mjini baada ya kuelezwa kuwa huu ni msiba na hakuna kiingilio na wote wameingia bure.
"Duh! baada ya kusikia hivyo nikajiona mjinga na kujua kuwa tayari imekula kwangu na ikabidi niuchune tu lakini jinsi ilivyoniuma imebidi nikwambi ndugu mwandishi ili uwajulishe watu, na wengine wasijefanyiwa kama mimi" alisema John
No comments:
Post a Comment
Tafadhari Maoni Yenye Matusi Hayatakuwa Publish Tutoe Maoni Bila Kuumiza Wala Kujeruhi Hisia Za Mtu.....@(Sponsored By Lukaza Blog)